Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-31 21:13:29    
Utamaduni wa asili wa mkoa wa Qinghai wastawishwa

cri

Qinghai ni mkoa ulioko kwenye Uwanda wa Juu wa Qinghai-Tibet, mkoani humo wanaishi watu wa makabila mengi. Kutokana na hali yake ya kijiografia na kuwa na makabila mengi, utamaduni mkoani humo una mvuto wa aina yake. Lakini kutokana na kushamiri kwa utamaduni wa kisasa, utamaduni wa asili miongoni mwa wakazi umekuwa unapungua, serikali na wasanii wenyeji wamefanya juhudi nyingi kukabiliana na hali hiyo, ili kuuwezesha utamaduni wao wa asili ustawi.

Mliosikia ni wimbo aina ya "ua" unaojulikana sana katika sehemu ya Hehuang mkoani Qinghai. Nyimbo za aina ya "ua' zinaimbwa sana miongoni mwa watu wa makabila ya Wahan, Wahui, Wa-tu, Wasala na Watibet katika mikoa ya Qinghai, Gansu, Ningxia na Xinjiang. Ingawa nyimbo za aina hiyo zinafahamika zaidi miongoni mwa wenyeji, lakini kadiri jamii inavyoendelea haraka utamaduni huo umekuwa ukitoweka siku hadi siku na kuwa kwenye hali ya kutoweka kabisa.

Hali hiyo imepewa uzito na idara za utamaduni mkoani Qinghai. Mkurugenzi wa idara ya utamaduni wa jamii mkoani humo Bi. Li Xiaoyan alieleza kuwa hivi sasa serikali ya mkoa imeanza kukusanya nyimbo za aina hiyo ili kuzihifadhi na kuwafundisha waimbaji vijana. Alisema,

"Kazi ya serikali ya mkoa ni kuwapatia watu fursa za kuonesha nyimbo hizo na kuandaa warithi vijana. Kila mwaka serikali inaandaa mashindano ya kuimba nyimbo za aina hiyo na kujitahidi kuwachagua waimbaji hodari. Waimbaji waliopata tuzo wanashirikishwa na kuonesha nyimbo zao katika vyuo vikuu na sehemu za makazi mjini Beijing. Kwa kutumia njia hiyo kazi ya kuandaa waimbaji vijana na kuimarisha utamadui huo wa asili inakuwa na mafanikio."

Sambamba na hatua hizo, idara ya utamaduni ya mkoa wa Qinghai imeweka mafaili ya waimbaji mashuhuri mkoani. Mahadhi pamoja na maneno ya nyimbo pia zinaboreshwa hatua kwa hatua na kuzifanya nyimbo hizo ziambatane zaidi na maisha ya wenyeji. Hivi sasa nyimbo za aina ya "ua" zimeorodheshwa kwenye orodha ya urithi wa utamaduni wa taifa la China.

Mbali na nyimbo za aina ya "ua", sanaa ya uchoraji iitwayo Tangka ni aina nyingine ya utamaduni wa asili mkoani Qinghai. Tangka ni picha zilizochorwa kwenye kitambaa cha hariri kwa kueleza hadithi za dini ya Buddha. Katika historia aina hiyo ya picha ilijulikana sana duniani na kusifiwa kuwa ni "sanaa inayotakiwa kuangaliwa kwa lenzi ya kukuzia"

Mwalimu Niangben mwenye umri wa miaka 36 amechora picha za Tongka kwa miaka zaidi ya 20. Ili kuandaa warithi mwezi Aprili mwaka 2007, mwalimu Niangben alianzisha shule ya uchoraji wa picha za Tangka kwa pesa zake, wanafunzi zaidi ya 40 kutoka mikoa ya Sichuan na Tibet wanafundishwa katika shule hiyo. Kwa mujibu wa maelezo ya mwalimu Niangben, mwanafunzi anatakiwa kufundishwa kwa miaka mitatu hadi saba, na wanafunzi wanaotoka sehemu zilizo nyuma kiuchumi wanasamehewa ada. Mwalimu Niangben alisema,

"Ni matumaini yangu kuwa mwalimu wa uchoraji wa picha za Tangka. Kabla mwalimu wangu hajafariki aliniomba nitukuze utamaduni wa kabila letu na kuandaa warithi wengi wa utamaduni huo."

Ili kuenzi uchoraji huo, serikali ya mkoa wa Qinghai ilifanya maonesho ya picha na kuanzisha kazi ya uchoraji huo katika chuo kikuu na kuwapa watunzi cheo cha utaalamu kwa kuwafanyia mitihani. Mtibet aliyechora picha za aina hiyo kwa miaka 55 Bw. Xi Hedao ni mchoraji mashuhuri, mwaka 2006 alichaguliwa kuwa "msanii mkubwa wa China". Kuhusu urithi wa sanaa hiyo alisema kwa uhakika,

"Kiwango cha kuandaa wachoraji vijana kimekuwa kinainuka siku baada ya siku, sera za serikali za kuhifadhi na kustawisha utamaduni wa asili wa kikabila zimewekwa. Hatuna wasiwasi kwamba utamaduni wetu utastawi."

Mzee Xi Hedao anaona kuwa sanaa ya picha za Tangka, sio mali ya Uwanda wa Juu wa Qinghai-Tibet tu, bali pia ni mali ya taifa la China na hata dunia. Sanaa hiyo inayoeleza upendo na masikilizano inasaidia kuleta hali ya kuishi kwa amani na urafiki duniani.

Nyimbo za aina ya "ua" pamoja na sanaa ya picha za Tangka ni sehemu moja tu ya utamaduni wa asili mkoani Qinghai, serikali ya mkoa wa Qinghai imefanya kazi nyingi ili kuhifadhi na kustawisha utamaduni wa aina nyingine za asili. Mkuu wa idara ya utamaduni ya mkoa wa Qinghai Bi. Cao Ping alieleza,

"Kuhusu shughuli za utamaduni usioonekana, serikali ya mkoa ina kikundi cha uongozi, kamati ya wataalamu na ofisi za utekelezaji, na vyombo hivyo pia viko katika kila ngazi mkoani."

Naibu mkuu wa mkoa wa Qinghai Jidimaja alipozungumza na waandishi wa habari alisema, serikali ya mkoa inazingatia sana kazi ya kuhifadhi utamaduni usioonekana, kwa upande mmoja inahimiza kazi ya kurithisha utamaduni huo na kwa upande mwingine imeandaa sera za kulinda utamaduni huo. Alisema,

"Mkoani Qinghai kila kabila lina sanaa yake, na sanaa hizo ni sehemu muhimu katika sanaa za asili za kikabila za taifa la China. Utamaduni ni msingi wa kujenga jamii yenye masikilizano, kazi ya kujenga utamaduni unaoleta masikilizano ya jamii ni jambo muhimu sana."