Mwanadiplomasia mmoja wa Marekani tarehe mosi Januari aliuawa nchini Sudan. Hili ni tukio la kwanza kwa mwanadiplomasia wa nchi za nje kuuawa nchini Sudan katika miaka ya karibuni. Tukio hilo lilitokea saa kumi alfajiri, wakati huo gari la ubalozi wa Marekani nchini Sudan lilipokuwa likipita kwenye barabara kuu mjini Khartoum lilishambuliwa kwa risasi na watu wenye silaha, dereva alikufa papo hapo na ofisa mmoja wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani alipigwa risasi kadhaa na alikufa baada ya kukimbizwa hospitali. Mpaka sasa hakuna jumuyia yoyote na mtu yeyote iliyotangaza kuwajibika na tukio hilo.
Vyombo vya habari vinaona kuwa tukio hilo ni kama msumari wa moto kwenye kidonda na kuufanya uhusiano mbaya uliopo kati ya Marekani na Sudan uzidi kuwa mbaya. Tokea miaka ya 90 ya karne iliyopita, uhusiano kati ya Sudan na Marekani ni wa baridi. Marekani inaishutumu serikali ya Sudan kuunga mkono ugaidi wa kimataifa na kufanya mauaji wa kikabila katika sehemu ya Darfur, lakini serikali ya Sudan inakanusha kabisa shutumu hizo. Mwaka 1998 kutokana na kisingizio cha kupambana na ugaidi, Marekani ililipua kiwanda kimoja cha kutengenezea madawa kilichopo kaskazini mwa Sudan, kisha ilijaribu kudhibiti uongozi wa kulinda amani ya Darfur. Tarehe 29 Mei mwaka 2007 Rais wa Marekani Bw. George Bush alitangaza kuchukua hatua za kuikwamisha Sudan licha ya vikwazo vilivyochukuliwa hapo kabla. Hatua hizo za Marekani zimefanya watu wa Sudan wawe na chuki dhidi ya Marekani, na mara kwa mara walifanya maandamano dhidi ya Marekani kuingilia kati mambo yao ya ndani na kuiwekea vikwazo nchi yao. Kadhalika, maofisa wa serikali ya Sudan pia kwa mara kadhaa walisisitiza kwamba hatua za Rais George Bush ni "kitendo cha ufidhuli", na wakati hali ya Darfur inapoanza kuwa nzuri, hatua za Marekani dhidi ya Sudan ni kitendo cha kuharibu amani ya Darfur, lakini serikali ya Sudan kamwe haitasujudu kwa shinikizo la Marekani.
Cha kustahili kufuatiliwa ni kwamba katika siku kabla ya tukio hilo, Rais George Bush kwa mara nyingine tena alisaini idhini kwa makampuni ya Marekani yanayohusika na sekta ya nishati nchini Sudan kusimamisha kuwekeza, na makampuni ya uwekezaji ya Marekani yasimamishe mikataba ya kibaishara na Sudan. Hatuna uhakika kama tukio hilo la mauaji linahusiana na uamuzi wa Marekani kuzidi kuiwekea vikwazo Sudan au la.
Lakini baada ya kuuawa kwa diplomasia huyo wa Marekani vyombo vya habari vingi vilidhani kwamba pengine tukio hilo linahusiana na kundi la Al-Qaida, vinasema mkuu wa kundi la Al-Qaida Osama bin Laden na msaidizi wake Ayman al-Zawahri waliwahi kutangaza kuanzisha vita vya jihadi dhidi ya nchi za Magharibi nchini Sudan. Mwaka 2002 tukio la kuuawa kwa diplomasia wa Marekani lilitokea mjini Amman, mji mkuu wa Jordan, baadaye tukio hilo lilithibitishwa kuwa ni kitendo kilichopangwa na kundi la Al-Qaida. Mwaka jana, tawi la Al-Qaida nchini Sudan lilitangaza kuwajibika na tukio la kumwua mhariri wa gazeti moja.
Lakini wizara ya mambo ya nje ya Sudan ilipotangaza taarifa kuhusu kifo cha mwanadiplomasia wa Marekani ilisema, tukio hilo sio la ugaidi bali ni "tukio lisilo na uhusiano na siasa, na halitaathiri hali ya siasa nchini Sudan na uhusiano kati yake na nchi za nje." Taarifa inasisitiza kuwa serikali ya Sudan siku zote inatilia maanani usalama wa watu wa nchi za nje wanaoishi nchini Sudan na hasa wanadiplomasia, na itaendelea kuwahakikishia usalama wao. Serikali ya Sudan imeanza kulifanyia uchuguzi tukio hilo, na muuaji ataadhibiwa kisheria.
|