Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-02 19:12:42    
Satellite ya ChangE ya kuchunguza sayari ya Mwezi yaongoza maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini China

cri

Mwaka 2007 maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini China yalikuwa yanang'ara duniani. Mafanikio ya satellite ya Chang E ambayo ni satellite ya kwanza ya kuchunguza sayari ya Mwezi ya China yamekuwa tukio muhimu kabisa katika mwaka 2007, na mafanikio hayo yameongoza maendeleo ya sayansi na teknolojia kupiga hatua kubwa.

Tarehe 24 Oktoba, satellite ya Chang E ilirushwa kwa mafaniko na kuelekea kwenye sayari ya Mwezi!

"Satellite ya Chang E No.1 imefanikiwa kupunguza mwendo kwa mara ya kwanza na kuingia kwenye njia yake ya kuzunguka sayari ya Mwezi kwa saa 12, na itaendelea kutekeleza kazi kama mpango wa kawaida uliowekwa."

Tarehe 5 Novemba, Satellite ya Chang E No. 1 ilifanikiwa kupunguza mwendo kwa mara ya kwanza ilipokuwa inakaribia sayari ya mwezi, na kuwa satellite ya kwanza ya China ya kuzunguka sayari hiyo.

Tarehe 26 Novemba, China ilitangaza sauti na nyimbo zilizotumiwa duniani na satellite hiyo kutoka kwenye njia yake ya kuzunguka sayari ya Mwezi iliyoko kilomita laki nne kutoka kwenye sayari ya dunia, na pia ilionesha picha ya kwanza ya sayari hiyo iliyopigwa na satellite hiyo.

Mpaka sasa, satellite ya Chang E No.1 imeweza kutimiza ndoto ya watu wa China kufika kwenye sayari ya mwezi ambayo haikutimizwa katika miaka elfu kadhaa iliyopita, na mafanikio hayo yamekuwa ya kwanza kwa China kuchunguza sayari nyingine kwa karibu. Mkurugenzi wa kamati ya viwanda vya sayansi na teknolojia za ulinzi ya China Bw. Zhang Qingwei alisema:

"katika muda wa miaka mitatu wa utafiti wa mradi huo, wanasayansi wa China wamevumbua teknolojia nyingi muhimu zikiwemo usanifu wa njia ya kuzunguka sayari, udhibiti wa urukaji na mawasiliano kutoka mbali, na China imekuwa na teknolojia nyingi zenye hakimiliki."

Namna ya kudhibiti kwa usahihi satellite ya Chang E No.1 iliyoko kilomita laki nne kutoka duniani ni suala lililopaswa kuhakikishwa kwanza. Kabla ya hapo China haikuwa na uzoefu wa kudhibiti satellite iliyoko zaidi ya kilomita elfu 70 kutoka duniani. Mkurugenzi wa kituo cha udhibiti wa safari za anga ya juu cha Beijing Bw. Zhu Mincai alisema, ili kutatua suala hilo, wanasayansi wa China walitumia mitandao ya aina tatu ya udhibiti, kuvumbua software maalum ya udhibiti yenye mstari zaidi ya milioni moja kwa mujibu wa satellite hiyo, na kufanya upimaji wa aina elfu 40 kuhusu hali ya ndani ya satellite hiyo. Bw. Zhu Mincai alisema:

"tulibadilisha njia za satellite mara nne, kurekebisha njiani mara moja na kupunguza mwendo wa satellite mara tatu, kila mara tuliidhibiti satellite kwa usahihi na kuinua kiwango cha usahihi wa udhibiti wa njia yake kufikia tatu kati ya elfu 10 kutoka asilimia 1.7."

Ili kutimiza malengo ya kisayansi yaliyowekwa, satellite ya Chang E No.1 ilibeba vifaa vya aina nane vya kisasa ambavyo vyote vilivumbuliwa kwa mara ya kwanza nchini China hata kote duniani.

Mbali na hayo, ili kuhakikisha upokeaji wa data zinazotumwa na satellite hiyo, China ilijenga antenna mbili Beijing na Kunming, ambazo mpaka sasa ni kubwa kabisa nchini China. Antenna hizo pia zimeweka msingi kwa uchunguzi wa sayari katika siku za baadaye.

Kutokana na matumizi ya teknolojia za kisasa, picha ya kwanza ya sayari ya mwezi iliyotumiwa duniani na satellite ya Chang E ni safi sana, mashimo yenye ukubwa na maumbo tofauti kwenye sayari hiyo yanaonekana wazi.

Picha hiyo ni uthibitisho wazi wa maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia za China. Serikali ya China imesifu mafanikio ya satellite hiyo kuwa alama muhimu nyingine kwenye njia ya maendeleo ya shughuli za safari za anga ya juu za China, baada ya mafanikio ya satellite ya kwanza ya kuzunguka dunia na vyombo vya safari za anga ya juu vilivyobeba wanaanga. Mafanikio hayo yameonesha wazi kuimarika kwa uwezo wa jumla wa China na kuinuka kwa uwezo wa kufanya uvumbuzi na kiwango cha sayansi na teknolojia nchini China.

Kuanzia mwanzoni mwa mwaka jana, China imerusha kwa mafanikio satellite nyingi, zikiwemo satellite ya upashanaji habari ya Xinnuo No. 3 na satellite ya pili ya uchunguzi wa bahari ya China. Urushaji kwa mafanikio wa Setellite ya upashanaji habari ya Nigeria iliyosanifiwa na China umesaidia shughuli za safari za anga ya juu za China ziimarishe zaidi hadhi yake kwenye soko la kimataifa. Aidha, mradi wa usanifu wa ndege kubwa ya abiria uliosimamishwa kwa miaka mingi umeidhinishwa mwaka huu na serikali ya China. Mhandisi mwandamizi wa kampuni ya viwanda vya safari ya anga ya China Bw. Guan Liwei alisema, China inatazamiwa kuweza kutengeneza ndege kubwa za abiria zenye hakimiliki ifikapo mwaka 2020. Bw. Gan Liwei alisema:

"kama tunaweza kukamilisha usanifu wa ndege kubwa ya abiria ifikapo mwaka 2020, uwezo wa jumla wa China utaimarishwa kidhahiri, na pia zitasukuma mbele maendeleo ya sekta mbalimbali za China."

Mbali na shughuli za safari za anga ya juu, mwaka huu mafanikio ya sayansi na teknolojia yaliyopatikana nchini China katika utafiti wa sayansi za kimsingi, utafiti wa teknolojia za kisasa na utafiti wa teknolojia za kunufaisha umma pia yamesifiwa na jumuiya ya kimataifa. Kwa mfano, mabaki ya dinosaur mkubwa kabisa duniani anayefanana na ndege kwa sura ambayo yaligunduliwa mwezi Juni mwaka huu na wanasayansi wa China huko Mongolia ya ndani hivi karibuni, yamesifiwa kuwa ni moja ya ugunduzi kumi muhimu wa kisayansi kwa mwaka 2007 na gazeti la Times ya Marekani.

Aidha, China pia imekuwa na uwezo wa kuongoza, kupanga na kutekeleza mradi mkubwa wa ushirikiano wa sayansi na teknolojia wa kimataifa. Hivi karibuni serikali ya China imeanzisha rasmi mpango wa ushirikiano wa kimataifa kuhusu nishati endelevu na nishati mpya.

Mafanikio ya sayansi na teknolojia yaliyopatikana nchini China mwaka huu yameifanya serikali ya China itambue wazi kuwa China inapaswa kuinua uwezo wa jumla wa nchi kwa uvumbuzi wa kujitegemea. Kwenye sherehe ya kusherehekea mafanikio ya mradi wa kwanza wa kuchunguza sayari ya mwezi iliyofanyika hivi karibuni, rais Hu Jintao wa China alisema wazi kuwa, China itaongeza zaidi uwekezaji kwa uvumbuzi wa kujitegemea. Rais Hu Jintao alisema:

"China itaongeza zaidi uwekezaji kwa shughuli za uvumbuzi wa kujitegemea, kuhamaisha uchangamfu na kuimarisha msukumo wa kufanya uvumbuzi, ili kuifanya China iwe na teknolojia muhimu na teknolojia zenye hakimiliki katika maeneo muhimu na maeneo kadhaa ya maendeleo ya teknolojia za kisasa."