Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-03 19:22:09    
Wageni wanavyotimiza ndoto zao nchini China

cri

Tangu China ianze kufanya mageuzi na kufungua mlango, maendeleo ya kasi ya uchumi wa China na utamaduni wanaong'ara wa Mashariki unawavutia wageni kutoka nchi mbalimbali. Wageni hao wanakuja nchini China kufanya kazi, kusoma, kutalii na hata kuweka makazi yao nchini China. Ingawa wageni hao wanakabiliana na vizuizi mbalimbali vikiwemo tofauti ya utamaduni, na mawasiliano ya lugha, lakini wengi wamefanikiwa kufanya mambo yao. Leo kwenye kipindi hiki cha Tazama China, tutawaeleza kuhusu mgeni mmoja aliyetimiza ndoto yake nchini China.

Zaidi ya miaka minne iliyopita, Bw. Fabien Colombo kutoka Switzerland alikwenda huko Yangshuo, mji mdogo wa wilaya wenye mandhari nzuri mkoani Guangxi, nchini China. Huko Yangshuo, Bwana Fabien alikuwa mwalimu mchangamfu wa lugha ya kiingereza kwenye kijiji kimoja, ambapo anafanya kazi vizuri na kuishi huko kama mwenyeji.

"Mandhari ya Guilin inajulikana nchini kote, lakini mandhari ya Yangshuo ni nzuri zaidi kuliko Guilin", watu wengi wanaona Yangshuo ni sehemu yenye mandhari nzuri kabisa nchini China. Mlima wa Mwezi na Mto Yulong unawavutia watu. Kwa Bw. Fabien, Yangshuo ni sehemu ambayo alianza kutafuta nafasi ya kutimiza ndoto yake.

Bw. Fabien alieleza maoni yake wakati alipofika huko Yangshuo mwaka huo.

"Nilifika Yangshuo mwaka 2001, wakati huo nilikuwa nimechoshwa na kazi yangu nchini Switzerland, hivyo niliamua kuchapa kazi kwa mwaka mmoja ili kupata fedha za kutosha, halafu nipumzike kwa miezi sita."

Kuanzia mwishoni mwa karne iliyopita, uchumi wa China umekuwa unaongezeka kwa hatua madhubuti, nafasi za ajira zilizo za kutosha, mazingira ya maisha yenye utulivu na athari ya China inayoongezeka kidhahiri duniani, yote hayo yanawavutia wageni wengi kuja China. Bw. Fabien pia alipenda kutalii nchi hii ya kale na yenye miujiza. Baada ya kupata fedha za kutosha, Bw. Fabien alipanda ndege na kuja China. Alisema:

"nilifika Hong Kong kwanza. Nilishangaa sana, kwa sababu kuna watu 800 tu kwenye maskani yangu. Lakini mji wa kwanza niliofika baada ya kuondoka Ulaya ni Hongkong, ni wenye majumba mengi na wakazi zaidi ya milioni 7!"

Lakini baada ya kuwasili Yangshuo, Bw. Fabien alivutiwa na maisha yenye utulivu na uchangamfu. Kuna wageni wengi huko Yangshuo, Bw. Fabien alijiona kama anaishi kwenye kijiji cha kimataifa.

Kwa kulinganishwa na hali ya mwanzoni mwa kufunguliwa kwa mlango na kufanga mageuzi nchini China, hivi sasa wageni wanaoishi nchini China hawachukui miji mikubwa tu kama Beijing na Shanghai. Katika miaka ya karibuni, serikali ya China imeweka sera nyingi za kuwawezesha wageni kuishi na kufanya kazi nchini China kwa urahisi, na kuzifanya hatua za kuishi na kusoma kwa wageni zinazozingatia desturi za wageni na kufuata desturi za duniani. Zamani wageni walikuwa wanapaswa kuishi kwenye hoteli au nyumba za wageni zilizoamuliwa na serikali tu, na hawakuweza kuchagua makazi kama wanavyopenda, wageni hapa Beijing walipaswa kuwa na kitambulisho cha ukazi wa muda. Mwaka 2003, Beijing iliondoa vizuizi hivyo ili kuwapa urahisi wageni wanaoishi nchini China. Yangshuo pia ilitumia fursa ya sera hiyo kuwavutia wageni wengi.

Bw. Fabien alifurahia muda alioishi huko Yanshuo. Lakini muda wa furaha ulipita kwa haraka. Kutokana na sera ya Switzerland, alipaswa kurudi Switzerland na kutoa huduma kwa jeshi la nchi hiyo kwa wiki tatu. Lakini hakuweza kusahau Yangshuo. Alisema:

"Nilipoishi Yangshuo, nilikutana na marafiki wengi na tulipenda kubadilishana uzoefu wetu. Lakini baada ya kurudi Switzerland, niliona kila mtu anaishi kipekee na hafuatilii na watu wengine. Nilifikiri kila siku, na kuona kuwa nilikuwa na furaha kubwa huko Yangshuo. Hivyo niliamua kufanya kazi kwa bidii kwa mwaka mmoja ili nipate pesa za kutosha na kurudi China!"

Mwaka 2003, Bw. Fabien alikuwa mmoja kati ya wageni lakini 1.8 waliokuwa wanafanya kazi nchini China. Alikwenda tena Yangshuo na kuwa mwalimu wa lugha ya kiingereza. Kuanzia wakati huo, hakuondoka tena Yangshuo. Alipokuwa akifanya kazi na kuishi huko, alikutana na msichana ambaye akawa mchumba wake.

Bibi Tang Jing ni mwenyeji wa Yangshuo na anafanya kazi kwenye mkahawa. Bw. Fabien alivutiwa naye kutokana na uchangamfu wake, nywele ndefu na kicheko chake. Alisema:

"Kwanza niliona msichana huyo, alimchukulia kila mtu kwa usawa, bila kujali anafanya kazi gani. Hii inaonesha kuwa yeye ni mkarimu na mwenye moyo wa dhati."

Ingawa vijana hao wawili ni wa nchi mbili zenye utamaduni tofauti, lakini kila mmoja anatilia maanani zaidi sifa na desturi za mwingine waote hao ni watu wema, wadhaifu na kufanya kazi kwa bidii.

Bw. Fabien ni mtoto pekee kwa wazazi wake, na wazazi wake hawaungi mkono yeye kuishi nchini China, na hawajawahi kuja China na wanaifahamu China kutokana na magazeti au filamu za magharibi.

Wageni wengi wanaijua kidogo China. Chombo kimoja cha habari cha China kilishirikiana na vyuo vikuu hapa Beijing na kuwauliza wageni zaidi ya 200 mijini Beijing, Shanghai na Guangzhou. Matokeo ya uchunguzi yalionesha, 36% ya wageni baada ya kuja China waliona kuwa China siyo nchi yenye makazi au majengo ya kale tu, 22% ya wageni walidhani kuwa kila mchina anaweza kucheza Gong-fu, 22% ya wageni baada ya kuja China waliona siyo kila mchina anaweza kuandika kwa kalamu ya brashi, na 11% ya wageni walidhani kila mchina anaweza kuimba opera ya Kibeijing.

Mwaka 2006, wazazi wa Bw. Fabien walikuja China na kuona Yangshuo inayomvutia mtoto wao. Bw. Fabien alisema:

"wazazi wangu walikuja China majira ya joto mwaka jana. Hilo lilikuwa ni jambo zuri, kwni waliweza kuona kuwa mimi sikupoteza wakati bure katika nchi nyingine. Hii ilikuwa ni mara yao ya kwanza kutembelea China, waliona kuwa mtoto wao anaishi nchini China kwa usalama na kwa furaha."

Wazazi wa Bw. Fabien walimpenda Bi Tang jing sana. Bw. Fabien alisema:

"walipomwona Tang jing walifurahi sana, kabla ya kuja China walikuwa na wasiwasi kuhusu mchumba wangu mchina, lakini walipoona Tang jing ni msichana mwema, walibadilisha maoni yao."

Bw. Fabien anafundisha lugha ya kiingereza kwenye shule ya lugha za kigeni huko Yangshuo, na anafanya kazi kwa makini. Mkurugenzi wa shule hiyo Bw. Ou Shensong ni rafiki mzuri wa Bw. Fabien. Alipozungumzia Fabien, alisema:

"anafundisha kwa makini, kila siku anafanya maandalizi ya masomo. Wanafunzi wanampenda sana, yeye anawafundisha lugha ya kiingereza na pia anawafundisha desturi za nchi za nje, ili kupanua upeo wao."

Bw. Fabien anajifunza utamaduni wa nchi ya kale ya Mashariki huko Yangshuo, anapenda kuwasiliana na watu wengine na kupenda kuwa na marafiki mapya wakiwemo wachina au watalii kutoka nchi mbalimbali. Kwa kuwa yeye anafanya kazi vizuri, ameteuliwa kuwa msimamizi mkuu wa mafunzo ya shule.