Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-04 19:21:54    
Machafuko nchini Kenya

cri

Tarehe 3 Januari maandamano makubwa ya kushirikisha watu milioni moja hayakufanyika huko Nairobi kama yalivyopangwa, na hakuna dalili yoyote ya kupungua kwa machafuko yanayoikumba Kenya.

Uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwaka 2007 ni sababu moja kwa moja ya kuzuka kwa vurugu hizo. Katika uchaguzi wa urais, rais wa sasa Mwai Kibaki na mpinzani wake mkubwa Bw. Raila Odinga kutoka chama cha ODM walipata kura zinazolingana. Matokeo ya mwanzo ya kura yalionesha kuwa Bw. Odinga aliongoza, lakini matokeo rasmi yaliyotolewa na Tume ya uchaguzi ya Kenya yalitangaza kuwa Bw. Mwai Kibaki ni mshindi. Chama cha ODM na wafuasi wake walikataa kukubali matokeo hayo ambayo yalikuwa kinyume na matarajio yao. Zaidi ya hayo Tume ya uchaguzi ilichelewesha kutoa matokeo rasmi, ndiyo maana upande wa upinzani ulishikilia kuwepo kwa udanganyifu na kuwahamasisha wafuasi wake waende barabarani kufanya maandamano.

Lakini watu wakichambua kwa undani wanaona kuwa, kuna sababu nyingine muhimu za kutokea kwa machafuko hayo. Kihistoria katika muda mrefu madaraka ya Kenya yalikuwa yanashikwa na Wakikuyu ambao ni kabila lenye idadi kubwa ya watu kuliko makabila mengine ya Kenya, hali ambayo ilikuwa inasababisha malalamiko kutoka kwa watu wa makabila mengine. Rais Mwai Kibaki wa sasa na rais wa kwanza wa Kenya Bw. Jomo Kenyatta wote ni Wakikuyu, ambao kabila lao ni robo ya idadi ya watu wa Kenya, na kwa jumla marais hao wawili walikuwa wamekuwa madarakani kwa miaka karibu 20. Bw. Raila Odinga anatoka kabila la Wajaluo ambalo pia ni kabila kubwa nchini Kenya, lakini mkoa wa Nyanza wanapoishi Wajaluo ni miongoni mwa sehemu zenye hali duni ya kimaendeleo nchini Kenya, ndiyo maana Wajaluo wana malalamiko makubwa dhidi ya Wakikuyu. Tangu mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita uchaguzi wa vyama vingi ulipoanza kutekelezwa nchini Kenya, migongano kati ya makabila mbalimbali imekuwa ikizidi kuwa mikubwa.

Mbali na hayo umaskini umesababisha mazingira ya kuzuka kwa vurugu. Ingawa katika miaka ya hivi karibuni tangu rais Mwai Kibaki aingie madarakani, uchumi wa Kenya uliongezeka kwa kasi, na mwaka 2006 ongezeko hilo lilifikia asilimia 6.1, lakini idadi ya watu wenye uwezo mdogo wanaoishi kwa kutegemea chini ya dola moja ya kimarekani kila siku, bado inachukua karibu nusu ya watu wote wa Kenya.

Watu wengi maskini wanaona kuwa hawajanufaika na ongezeko la uchumi wa taifa, kwa hiyo wana hamu kubwa ya kuleta mabadiliko, na wao pia ni waungaji mkono imara wa chama cha upinzani ODM. Mara baada ya tume ya uchaguzi ya Kenya kutangaza ushindi wa Bw. Mwai Kibaki, watu maskini wasio na ajira au wasio na ajira ya kudumu walihamaki, walipora maduka na kuchoma moto magari wakionesha malalamiko yao dhidi ya jamii na serikali. Na majambazi pia walijinufaisha kwenye uporaji huo.

Tangu kuzuka kwa machafuko, rais Kibaki alikuwa ameomba vyama mbalimbali vifanye mazungumzo ili kutatua msukosuko wa hivi sasa. Pia aliwataka watu waache kufanya vurugu, na kuwataka watu wa Kenya washikamane katika ujenzi wa taifa. Habari nyingine zinasema, rais Kibaki ataweza kutoa nyadhifa ya serikali kwa upande wa upinzani ili kupunguza migongano. Lakini Bw. Odinga alikataa kufanya mazungumzo na Bw. Kibaki kabla ya yeye kukubali kushindwa kwenye uchaguzi wa urais.

Wachambuzi wanasema kutumia nguvu ya wananchi katika kuvutia ufuatiliaji wa jumuiya ya kimataifa na kuiwekea serikali shinikizo kunamsaidia Bw. Odinga, lakini jumuiya ya kimataifa inapenda kuona Kenya yenye utulivu, na sio hali ya nchi hiyo izidi kuwa mbaya. Ndiyo maana mazungumzo na kurudi nyuma ni njia pekee inayotakiwa kufuatwa na vyama mbalimbali nchini Kenya. Tume ya uchaguzi ya Kenya imesema itatangaza hadharani haraka iwezekanavyo matokeo ya hesabu ya kura ya kila kituo cha upigaji kura, ili kuondoa wasiwasi kwa watu wa Kenya.