Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-07 14:45:07    
Filamu za kusherehekea mwaka mpya zaoneshwa kila mahali nchini China

cri

Siku Wachina wanapokamilisha na kusherehekea mwaka mpya, filamu nyingi za burudani zilioneshwa kila mahali nchini China.

Filamu hizo zilizopigwa kwa nia ya kuchangia furaha ya mwaka mpya, zilianza kuoneshwa miaka kumi iliyopita. Tokea mwaka 1997 filamu za kuchekesha na kuoneshwa katika siku za mwaka mpya zimepigwa nyingi zikiwa ni pamoja na filamu za "Upande wa A na B katika Mkataba wa Kibiashara", "Simu ya Mkononi" na "Hakuna Mwizi Duniani", lakini mwaka huu filamu zinazooneshwa katika siku za mwaka mpya licha ya filamu za burudani pia kuna filamu halisi ya vita iliyopigwa kwa kuongozwa na mwongozaji mkubwa wa filamu Bw. Feng Xiaogang. Filamu hiyo inayoitwa "Tarumbeta ya Kukusanyika Pamoja" inasimulia vita vilivyotokea katika miaka ya 40 ya karne iliyopita. Kamanda wa kampeni moja alipata amri ya kuwazuia maadui, kabla ya kwenda vitani alikubaliana na kamanda wa rejimenti kuondoka vitani baada ya kukusanyika pamoja baada ya tarumbeta kupigwa. Wakati vita vikiendelea alikufa askari mmoja baada ya mwingine, na mwishowe alibaki kamanda mmoja tu. Baada ya vita kamanda huyo alikuwa na wasiwasi kama tarumbeta ilipigwa au la, alipiga nia kutafuta ukweli. Filamu hiyo inaonesha ukatili wa vita na huku inaonesha heshima ya utu. Mazingira ya vita yanatetemesha moyo. Profesa wa Chuo Kikuu cha Filamu cha Beijing Bw. Chen Shan alisema,

"Hii ni fulamu iliyotengenezwa kwa aina ya kipekee, nusu ya kwanza ilipigwa kwa kuelekezwa na mwongozaji wa Korea ya Kusini ambayo kiwango chake kinaweza kulingana na filamu maarufu za kivita duniani, na sehemu ya pili ilielekezwa na mwongozaji mkubwa wa China Bw. Feng Xiagang, ambayo inaeleza zaidi hatima ya kila askari na kuwafanya watazamaji waone masikitiko kwa thamani ya uhai wa binadamu, mwongozaji ameunganisha vizuri hamasa za kupata matumaini na kuonesha ushupavu, filamu iliyounganisha sehemu hizo mbili imeifanya filamu hiyo ivutie kwa kiwango cha juu cha sanaa."

Filamu nyingine iliyooneshwa katika siku za mwaka mpya ni "Ugomvi kati ya Ndugu Watatu wa Kiapo". Hii ni filamu iliyotengenezwa kwa mujibu wa hadithi iliyosimuliwa kwa miaka mingi miongoni mwa Wachina, ikieleza kuwa kutokana na kugombea mwanamke mmoja, ndugu watatu walikuwa na uhasama. Mwongozaji wa upigaji wa filamu hiyo kutoka Hong Kong Bw. Chen Kexin alisema,

"Hii ni filamu inayolenga watazamaji wa China tu, watu hutamani kupata mambo ambayo hawawezi kuyapata kamwe, kwa sababu hali waliyo nayo ni mbali na wanayotamani, kwa hiyo ni lazima wakubali ukweli wa mambo."

Lakini mwaka huu pia hazikosi filamu za kuchekesha, moja katika filamu hizo ni "mabadiliko ya majaaliwa", kwamba kutokana na watu watatu waliotumia aina moja ya simu ya mkononi kila mmoja alikosea kutumia simu ya mwenzake. Wakati walipopata ujumbe wa kukutana kwa miadi mahali Fulani, kila mmoja alimwona mtu ambaye hakupanga kuonana naye, na kutokana na mazungumzo yao kila mmoja ameelewa siri ya mwenzake na kusababisha vichekesho. Mwishowe, hao watatu walielewa kwamba hayo yalitokana na kubadilishana simu ya mkononi bila wao kujua.

Filamu nyingine ya kuchekesha ni filamu inayoitwa "Filamu Mbili" ikieleza kuwa, kwa kuwa na tamaa ya kutajirika watu wawili mume na mke waliopoteza mapenzi yao waliyokuwa nayo mwanzoni mwa ndoa, walipiga filamu moja iitwayo "Mwongozo kwa Waliooana Karibuni". Katika siku za kushughulikia upigaji wa filamu hiyo hao wawili walioishiwa na mapenzi wamerudisha tena mapenzi yao. Aliyeongoza upigaji wa filamu hiyo Bw. A Gan alisema,

"Katika filamu hiyo tunazingatia zaidi kueleza hadithi yenyewe na kichekesho ni kitu cha pili. Filamu hiyo imehaririwa kwa mujibu wa filamu ya Hispania ambayo ilitengenezwa na kuigizwa na mume na mke wao wenyewe, ni filamu ya kuchekesha na ya dhihaka."

Filamu nyingine inaitwa "Mto Changjiang Nam. 7". Hii ni filamu iliyoigizwa na mwigizaji mashuhuri wa Hong Kong Bw. Zhou Xingchi, ni filamu inayochekesha na kusikitisha, ikieleza kwamba baba mmoja aliyekuwa maskini sana, ili ampatie mtoto wake riziki alikwenda kufanya kazi ya kibarua katika sehemu ya ujenzi, aliokota kitu kimoja cha ajabu kwenye jalala na alimpa mtoto wake kama ni kitu cha kuchezea, kwa bahati kitu hicho kilikuwa ni chombo cha kupasha habari cha watu wa nje ya dunia. Mwongozaji alisema, filamu hiyo inawafanya watazamaji washangae. Alisema,

"Watazamaji wa China wanatakiwa kulinda upendo wa familia, hii ndio sababu yangu ya kupiga filamu hiyo. Mambo yaliyomo kwenye hadithi ya filamu hiyo inatokea sana miongoni mwa watu wa kawaida wa China, lakini maana yake si ya kawaida."

Wanafilamu wanasema, filamu za kusherehekea mwaka mpya zimekuwa na maendeleo ya miaka kumi, na zimepevuka katika uchaguzi wa mambo ya kuoneshwa na sanaa ya upigaji. Mwaka huu filamu za kusherehekea mwaka mpya ziko za kuchekesha, za kufurahisha na kuhuzunisha, na pia ziko filamu za kuvutia huruma, watazamaji wana nafasi nyingi za kuchagua wanayopenda.

Idhaa ya kiswahili 2008-01-08