Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-07 15:10:04    
Sehemu ya Xishi yenye mandhari nzuri mjini Hangzhou, China

cri

Hangzhou ni mji maarufu wa utalii nchini China, ziwa Xihu ni mahali ambapo watalii wa nchini na wa kutoka nchi za nje hawakosi kutembelea. Kila siku kuna halaiki ya watalii wenye furaha; lakini kuna sehemu moja ya ardhi oevu, ambayo ina umbali wa chini ya kilomita 5 kutoka ziwa Xihu, ambayo ni nzuri na haina kelele, sehemu hiyo inaitwa Xishi. Xishi ni bustani ya kwanza yenye ardhi oevu ya ngazi ya taifa, na pia ni ardhi pekee oevu iliyoko kwenye mji nchini China.

Mara tu baada ya kuingia kwenye bustani ya Xishi yenye ardhi oevu, watu wanaweza kuona mara moja mandhari ya mazingira ya sehemu ya vijiji yenye vijito ya kusini mwa China: mianzi inaota kando ya ziwa, na kama wakitazama mbali wanaweza kuona misitu minene, hata mtu anaweza kuona sungura pori kwenye mitelemko ya mlima yenye majani mangi.

Maji ni roho ya Xishi, vijito, mabwawa madogo, ufukwe na visiwa vingi vidogo, vinaunda mandhari nzuri ya ardhi oevu ya Xishi. Bi Zhao Wenjuan ni mtalii aliyetoka mji wa Ningpo, mkoani Zhejiang, anayependa sana mazingira hayo. Alisema,

"Picha ya kwanza niliyoipata kichwani mwangu kuhusu sehemu hiyo ni kuwa inaburudisha sana, kuna maji kila mahali, na kila mahali ni pa starehe na penye unyevunyevu. Mazingira ya asili ya hapa yamehifadhiwa vizuri sana."

Sehemu ya Xishi ina vivutio viwili vikubwa, yaani maua ya matete na miti ya plamu. Mwezi Novemba, ni wakati mzuri wa kuangalia maua ya matete. Kama ukipanda kwenye mashua inayokwenda kwa nguvu ya betri, ambayo haina kelele wala kutoa vitu vya kuchafua mazingira, unaweza kuona matete yenye maua yakiyumbayumba kwa upepo, na maua ya matete yanapeperushwa hewani na upepo, Xishi inaonekana kama michoro safi ya sehemu moja ya vijijini.

Kwa kawaida maua ya mti wa plamu yanachanua katika majira ya baridi, ingawa kuna wakati huwezi kuona maua ya mti wa plamu, lakini unaweza kuona matunda mengi ya Persimmon ya rangi nyekundu yanayoonekama kama moto kwenye mitelemko ya milima, na yameongeza rangi nyekundu ya kupendeza kwenye rangi ya kijani ya mitelemko ya milima.

Mabaki ya kiutamaduni pia ni moja ya ummaalumu wa kuvutia kwenye ardhi oevu ya Xishi. Katika enzi za Ming na Qing, sehemu ya Xishi ilikuwa mahali pa kuvutia wasomi waliotaka kuishi mafichoni. Kuna vivutio kadhaa ndani ya bustani hiyo, ambavyo ni pamoja na mahekalu ya watawa wa kike ya Qiuxue na Boan, kijiji cha mlimani cha Meizhu, na banda la kusomea la Xishi, sehemu hizo zilikuwa mahali walipopenda kukaa wasomi na washairi hapo zamani za kale, na waliandika makala na kutunga mashairi mengi yanayofahamika sana. Hata mfalme Kangxi wa enzi ya Qing aliwahi kufika huko kumtembelea waziri wake wa karibu Gao Shiqi, tena alitunga shairi moja kuhusu kijiji cha mlimani cha Xishi. Mwongoza watalii Bi Chen alikariri shairi hilo lililotungwa na mfale Kangxi.

Shairi hilo linasimulia mazingira nadhifu ya Xishi yenye vijito vingi vilivyopindapinda, wakulima waliofuga mabuu wa nondo wa hariri, mianzi na maua ya mti wa plamu, ambayo wasomi wa kale walipenda kuishi.

Katika muda wa miaka karibu 100 iliyopita, Xishi ilikuwa kimya kama ilisahauliwa na kutelekezwa na watu. Lakini tokea mwaka 2003, ardhi oevu ya Xishi ilianza kuvutia watu tena. Mji wa Hangzhou ulichukulia ardhi hiyo oevu kama mafigo ya mji, umekuwa ukijitahidi kuihifadhi na kuiendeleza kwa kuanzisha ujenzi wa mradi wa kipindi cha kwanza na cha pili, hadi mwezi Oktoba mwaka huu, ujenzi wa kipindi cha tatu pia utakamilishwa, ambapo eneo la ardhi oevu ya Xishi litapanuka na kuzidi kilomita kumi za mraba.

Pamoja na kurekebishwa kwa mazingira, sehemu ya Xishi imekuwa na vivutio vingi, ambavyo vimefanya idadi ya watalii wanaoitembelea kuongezeka kwa mfululizo. Mwenyeji wa huko, Bw. Liu Po alisema, mazingira mazuri ya huko yanafanya maisha ya watu yawe na raha zaidi.

"Ninaona sehemu hiyo ni ya kuvutia sana, vijia vinavyoelekea mahali pa ndani pasipo na kelele, maji yanayotiririka chini ya vidaraja, naona mandhari hiyo ni nzuri sana."

"Ukingo wa kijani" ni kivutio kinachopendwa na watalii wengi. Ukingo huo uliojengwa kwa vioo vya umbo la pembe mraba vyenye urefu wa mita 137, upana wa mita 3 na kimo cha mita 1 hadi 3. kwenye kando mbili za ukingo imepandwa mimea ya majini aina karibu 700. Watalii wanaweza kufika chini ya maji kwa kupitia ukingo huo na kuangalia mizizi ya mimea ya majini na viumbe wanaoongelea majini.

Maji ya sehemu ya Xishi ni mazuri. Ndani ya bustani ya ardhi oevu kimejengwa kituo cha kupima sifa ya maji, tena idara ya usimamizi ya bustani inatumia mbinu ya kuboresha maji kwa mimea ya majini. Mwongoza watalii, bi Chen alionesha kwa kidole chake aina moja ya mmea unaoota kwenye bwawa lililoko kando ya njia, akisema,

"Mmea ule unaochanua maua ya rangi ya zambarau ni water hyacinth, ingawa mmea huo unazaliana kupita kiasi, lakini tukiupunguza kila baada ya muda, unaweza kudumisha sifa ya maji. Maji ni tofauti kati ya yale yenye mmea huo na yasiyo na mmea huo. Kila baada ya muda maalumu tunaupunguza, lakini maji yanaweza kuwa safi zaidi."

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii, watu wameanza kuwa na wasiwasi kuwa, huenda maendeleo ya utalii yataleta athari mbaya kwa mazingira ya ikolojia. Mfanyakazi wa ofisi ya bustani ya ardhi oevu ya Xishi. Bw. Liu Xiang alisema, ofisi ya bustani hiyo imethibitisha kuendeleza utalii wa Xishi kuwa utalii wa ikolojia, na kutilia mkazo hifadhi ya mazingira, alisema,

"Sisi tumeweka kanuni ya kudhibiti idadi ya watalii, ambayo isizidi 3,000 kwa siku ili kupunguza shinikizo dhidi ya mazingira ya asili."

Licha ya kudhibiti idadi ya watalii, ofisi ya bustani imejenga mahali panapofaa kuishi kwa viumbe vya aina nyingi. Hivi sasa aina za mimea kwenye ardhi oevu ya Xishi zimeongezeka hadi kuwa 262 kutoka aina 221, samaki na viumbe wengine wa majini wamefikia aina 50, ndege wameongezeka hadi aina 126 kutoka aina 89, wakichukua nusu ya jumla ya idadi ya ndege wa mjini Hangzhou.

Bw. Liu Xiang alisema, mpango wa bustani hiyo katika siku za usoni ni kuendeleza utalii wa mapunziko, na kujenga eneo la makazi ya mapumziko chini ya hali ya kupunguza kadiri iwezavyo athari mbaya ya majengo kwa mazingira ya ikolojia. Aidha, ofisi ya bustani hiyo imeweka mpango wa kujenga jumba la makumbusho ya ardhi oevu ya China la Xishi, ambalo litafunguliwa rasmi kwa watalii kuanzia mwaka 2009.

Idhaa ya kiswahili 2008-01-07