Kutokana na usuluhishi wa kimataifa, tarehe 7 kiongozi wa chama cha ODM Bw. Raila Odinga alitangaza kufuta maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 8, na hali ya Kenya inaelekea kuwa ya utulivu. Hapo kabla, Rais Mwai Kibaki aliyeshinda uchaguzi mkuu tarehe 3 alitoa hotuba akisema, ghasia zikitulia atafanya mazungumzo na chama cha upinzani. Ingawa Bw. Odinga alijibu kwa hasira lakini alitoa masharti mawili ya kufanya mazungumzo, moja ni kuwa Rais kibaki ajiuzulu, pili ni kufanya usuluhisho kupitia upande wa tatu. Tarehe 4 Bw. Odinga alitoa sharti jingine yaani kuunda serikali ya muda na kurudia tena uchaguzi katika muda usiozidi miezi mitatu chini ya uangalizi wa kimataifa, lakini huku alisema anakubali mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika, Rais wa Ghana John Koffour kufanya usuluhishi. Tarehe 5 Rais Kibaki kwa mara nyingine alionesha ishara ya kutaka amani kwamba alipokutana na msaidizi wa waziri wa mamabo ya nje wa Marekani anayeshughulikia mambo ya Afrika Bi. Jendayi Frazer, akisema anakubali kuunda "serikali ya mseto" na kuunganisha nguvu zote za makundi ya kisiasa ili kumaliza mgogoro wa mauaji. Ingawa Bw. Odinga alikataa kuundwa kwa serikali ya mseto, lakini alisisitiza kwamba mgogoro wa kisiasa hauwezi kumalizika bila kupitia usuluhishi wa upande wa tatu. Bw. Odinga alisema mazungumzo yanaweza kuanzishwa mara tu baada ya mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika, rais wa Ghana John Koffour, kufika nchini Kenya. Mwanzoni Rais Kibaki aliona kuwa hakuna haja ya kuomba msuluhishi, kwa sababu Kenya haiko katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, lakini sasa ametuma mjumbe wake kwenda Ghana kumweleza Bw. Koffour hali ilivyo nchini Kenya. Habari zilizopatikana zinasema Bw. Koffour alipanga kuwasili Nairobi tarehe 8 asubuhi. Yote hayo yameonesha kuwa pande zote mbili hazijafunga kabisa mlango wa mazungumzo. Lakini kwa nini?
Kwanza hali hiyo inatokana na shinikizo kutoka nchini na nchi za nje. Tokea machafuko yalipozuka watu wa Kenya mia kadhaa walipoteza maisha na laki kadhaa wamepoteza makazi yao, isitoshe uchumi umeathirika vibaya, thamani ya Shilingi imeshuka, biashara ya kahawa na chai imesimama, bei ya hisa imeshuka na idadi ya watalii imepungua sana. Hivi sasa wananchi wanalilia viongozi wa makundi ya kisiasa wafanye mazungumzo ili kumaliza haraka machafuko. Duniani, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Marekani na Uingereza zote zinafanya juhudi za kuzikutanisha pande mbili kwenye mazungumzo. Hali kama hiyo ni lazima izingatiwe na Bw. Kibaki na Bw. Odinga.
Pili, mazungumzo yananufaisha pande zote mbili. Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa bunge yaliyotangazwa, chama cha upinzani ODM kimepata viti 99 ambavyo ni karibu nusu ya viti vyote na vinazidi kwa kiasi kikubwa viti 43 kilivyopata chama cha PNU. Kutokana na hali hiyo Bw. Kibaki akitaka kuunda serikali yenye utulivu ni lazima apate ushirikiano wa vyama vya upinzani. Kwa upande wa Odinga, hali kama hiyo ikiendelea licha ya kutoweza kutimiza tumaini lake la kuwa rais, hata maisha yake ya kisiasa yataathirika vibaya. Kwa hiyo, kupata suluhisho kupitia mazungumzo kutazinufaisha pande hizo mbili.
Katika siku hizi mbili, hali ya machafuko nchini Kenya imeanza kuelekea kwenye utulivu, shughuli za biashara na usafiri katika miji mikubwa zimeanza kurudi, idara za serikali zimeanza kuwajibika, shughuli za makampuni na mashirika zimekuwa kawaida, barabarani magari na wapita njia wamekuwa wengi. Lakini ukungu uliotanda nchini Kenya unasubiri kuondolewa na viongozi kwa kufanya mazungumzo, kwa kupitia usuluhishi wa kimataifa hali ya machafuko itaelekea kuwa ya utulivu.
|