Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-09 16:48:30    
Uwekezaji kwa mwaka 2007 duniani ulikuwa mkubwa kuliko miaka yote iliyopita

cri

Shirika la Maendeleo na Biashara la Umoja wa Mataifa, UNCTAD, tarehe 8 lilitoa taarifa ikisema, thamani ya uwekezaji duniani kwa mwaka jana ilifikia dola za Kimarekani trilioni 1.538, huu ni uwekezaji mkubwa kabisa kupataikana kuliko wa miaka yote iliyopita.

UNCTAD ni shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia maendeleo na biashara duniani. Shirika hilo liliundwa mwaka 1964 na makao yake makuu yako Geneva, lengo la shughuli zake ni kuzihimiza nchi zote wanachama na hasa nchi zinazoendelea ziendeleze uchumi na biashara na kwa kadiri inavyowezekana kuziletea nchi zinazoendelea fursa za biashara na uwekezaji, na kuzisaidia nchi hizo kukabiliana na changamoto ya utandawazi duniani. Kila mwaka shirika hilo linatoa ripoti ili kuzisaidia nchi wanachama kutunga sera za uchumi.

Shirika hilo linatoa "ripoti kuhusu uwekezaji duniani" katika robo ya nne kila mwaka kueleza hali na mwelekeo wa uwekezaji duniani. Ingawa ripoti iliyotolewa tarehe 8 ni takwimu za mwanzo, lakini kimsingi imeonesha hali ya uwekezaji duniani.

Ripoti inasema, mwaka 2007 ulikuwa ni mwaka wenye uwekezaji mkubwa, na jumla ya uwekezaji ulifikia dola za Kimarekani trilioni 1.538, ambalo ni ongezeko la dola bilioni 130 kuliko mwaka 2000 ambao uwekezaji wake ulikuwa dola za Kimarekani trilioni 1.4.

Mwaka jana Marekani iliendelea kuwa ni nchi iliyopokea mitaji mingi duniani kutoka nchi za nje, ambayo ilifikia dola za Kimarekani bilioni 193, hilo ni ongezeko la 10% kuliko mwaka 2006. Ripoti inasema, katika nusu ya pili ya mwaka jana Marekani ilikumbwa na msukosuko wa mikopo, lakini hali hiyo haikuathiri uwekezaji kutoka nchi za nje, bali kushuka kwa thamani ya dola ya Marekani kumevutia mitaji mingi zaidi kutoka Ulaya na Asia.

Kati ya mitaji yote duniani, zaidi ya nusu iliwekezwa kwenye nchi zinazoendelea, na China inaongoza kati ya nchi hizo ambayo ilipata uwekezaji wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 67.3. Licha ya China, nchi nyingine kama Indonesia na Malaysia pia zilivutia mitaji mingi. Tukizingatia kasi ya ongezeko la uwekezaji kutoka nchi za nje, Russia ni nchi inayopata kasi kubwa ya ongezeko la uwekezaji. Mwaka jana ongezeko lake la uwekezaji lilikuwa 70% kuliko lile la mwaka 2006 na kufikia dola za Kimarekani bilioni 48.9.

Ripoti ilifafanua kwamba kuna sababu nyingi zilizohamasisha uwekezaji duniani, moja ni faida za makampuni zilikuwa zimeongezeka, fedha zilizokuwa kwenye mzunguko zilikuwa za kutosha, na manunuzi ya makampuni ya kimataifa yalichangamka.

Kuhusu hali ya mwaka 2008 ulioanza hivi karibuni shirika hili halioni hali ni nzuri. Ripoti inasema mwaka 2008 pengine utakumbwa na hali ya kushuka kwa kasi kwa uwekezaji duniani. Uchumi wa Marekani pengine utazorota kutokana na msukosuko wa mikopo mibaya na kuathiri uchumi duniani. Isitoshe, maendeleo ya uchumi yasiyo na uwiano, kupanda kwa gharama za bidhaa za kimaisha, mfumuko wa bei na kiwango kisichotulia katika ubadilishaji wa fedha, yote hayo yatakwamisha uwekezaji.

Idhaa ya kiswahili 2008-01-09