Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-09 17:15:59    
Hatua za serikali ya Qinghai zawahimiza wafugaji wa makabila madogo madogo kuongeza mapato kupitia kushiriki kwenye shughuli za utamaduni

cri
Kikundi cha Aisaimai kilianzishwa mwaka 2004, waimbaji na wachezaji wa kikundi hicho wengi ni wa makabila ya Watibet na Wamongolia. Katika miaka mitatu iliyopita, kikundi hicho kilifanya maonesho kwenye sehemu mbalimbali nchini China, idadi ya waimbaji na wachezaji wa kikundi hicho iliongezeka na kufikia 520 kutoka 66, na mapato yao pia yaliongezeka kwa kiasi kikubwa. Mwanzilishi wa Kikundi cha Aisaimai Bw. Wang Xuande alisema, baada ya kuanzishwa, kikundi hicho kilifanya maonesho ya kuimba nyimbo na kucheza ngoma za makabila ya Watibet na Wamongolia, na kiliwafurahisha sana watazamaji, alisema,

"Waimbaji na wachezaji ngoma wanaweza kupata mapato ya Yuan elfu 12 kwa kufanya maonesho kwa siku kadhaa, na wao pamoja na jamaa zao wanafurahi sana."

Mkoa wa Qinghai ni sehemu ya kuhifadhi vyanzo vya maji nchini China. Kwenye mkoa huo kuna maeneo makubwa ya ufugaji. Katika miaka ya hivi karibuni, mazingira ya mkoa huo yaliharibiwa kutokana na sababu za kimaumbile na wingi wa kupita kiasi wa mifugo. Mwaka 2003, serikali ya mkoa wa Qinghai ilianza kutekeleza sera ya kuacha kutumia mbuga kwa malisho na kuwahimiza wafugaji wa makabila ya Watibet na Wamongolia wahamie mijini. Ili kuwasaidia kuzoea maisha mapya mijini, serikali ya Qinghai iliwapatia makazi, kuwafundisha kazi mbalimbali za ufundi za kumudu maisha ikiwemo kuendesha magari na kilimo, aidha serikali ilichukua hatua ya "kuongeza mapato ya wafugaji kwa kupitia shughuli za utamaduni" yaani kuwashirikisha wafugaji hao kwenye shughuli za utamaduni ili kuongeza mapato, kwa kuwa watu wa makabila ya Watibet na Wamongolia ni hodari katika kuimba nyimbo na kucheza ngoma.

Ili hatua hiyo ifanikiwe, serikali ya mkoa wa Qinghai ilitunga mpango maalumu, na kuanzisha semina bila malipo kuhusu kucheza ngoma kwa vijana wa makabila ya Watibet na Wamongolia. Wakati huo huo, hatua hiyo pia iliungwa mkono na makampuni. Semina ya mwaka 2007 ya kucheza ngoma ya makabila madogo madogo iliandaliwa na kampuni binafsi ya Dawutai. Je, ikiwa kampuni yenye madhumuni ya kupata mapato, kwa nini iliandaa semina hiyo bure? Meneja wa kampuni hiyo Bw. Wang Xiaobo alisema,

"Mkoa wa Qinghai una utamaduni unaong'ra wa makabila mbalimbali wa nyimbo na uchezaji ngoma, tunapaswa kuuendeleza. Kuwafundisha watu wa makabila hayo sio tu kunaweza kuwasaidia kuongeza uwezo wa kufanya shughuli za utamaduni, bali pia kunaweza kuendeleza utamaduni wa mkoa wa Qinghai."

Si rahisi kwa watu waliokuwa wafugaji wa kawaida kujifunza kucheza ngoma. Kutokana na mpango wa serikali ya mkoa wa Qinghai, watu hao walijifunza kucheza ngoma za aina kadhaa katika mwezi mmoja. Bw. Tsekong Thar mwenye umri wa miaka 24 anatoka eneo la ufugaji kwenye uwanda wa juu, yeye ni mwimbaji na mchezaji hodari wa ngoma wa kabila la Watibet, sasa yeye ni mwalimu wa semina zinazoandaliwa na serikali kwa ajili ya kuwafundisha wafugaji kuimba nyimbo na kucheza ngoma za kikabila. Bw. Tsekong Thar alisema anawataka wanafunzi wake waeneze utamaduni wa makabila yao wakati wanapoongeza mapato kwa kupitia kufanya maonesho ya michezo ya sanaa. Bw. Tsekong Thar alisema,

"Baada ya kujifunza kuimba nyimbo na kucheza ngoma, watakwenda mijini kufanya maonesho ya michezo ya sanaa ya makabila yao. Maonesho hayo yatawafanya watu wengine waelewe zaidi mambo ya kitibet."

Wakisaidiwa na walimu, wanafunzi wa semina wana matumaini makubwa kwa mustakabali wao. Bi. Chimo Tso kutoka sehemu iliyo chini ya Mlima Tanggulashan alisema, ndoto yake ni kucheza ngoma na kuwaoneshea watu wote duniani, na kuwaambia watu wengine kutoka kwenye maskani yake washiriki kwenye semina hizo ili kubadilisha maisha yao.

Mbali na kuwaandalia semina za kuimba nyimbo na kucheza ngoma, serikali ya mkoa wa Qinghai pia inawahimiza watu wa makabila madogo madogo waliokuwa wafugaji kujishughulisha na utengenezaji wa vitu vya sanaa za makabila yao ikiwemo uchoraji picha, utengenezaji wa sanamu, na nakshi, ili kujiongezea mapato. Takwimu zinaonesha kuwa hadi sasa idadi ya watu wanaojishughulisha kwenye shughuli hizo za utamaduni imezidi elfu 50, na mapato yao kwa mwaka yamefikia Yuan elfu 2.2.

Kutokana na juhudi za serikali pamoja na wakazi wa mkoa wa Qinghai, shughuli za utamaduni zinaendelea kwa kasi siku hadi siku. Shughuli hizo sio tu zinawasaidia watu waliokuwa wafugaji kuongeza mapato, bali pia zinatoa mchango kwa ajili ya kuhimiza ujenzi wa utamaduni na maendeleo yenye masikilizano kwenye sehemu ya ufugaji mkoani Qinghai. Naibu mkuu wa mkoa wa Qinghai Bw. Jidima anatoka kabila la Wayi, alisema,

"Kuendeleza shughuli za utamaduni sio tu kunahimiza urithi wa utamaduni wa makabila mbalimbali tu, bali pia kunawasaidia wafugaji kuongeza mapato. Huu ni utaratibu mzuri unaounganisha utamaduni na soko. Shughuli za utamaduni zinapaswa kutoa mchango zaidi kwa maendeleo ya uchumi mkoani Qinghai katika siku zijazo."

Idhaa ya kiswahili 2008-01-09