Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-10 15:40:04    
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika aanza kusuluhisha mgogoro wa kisiasa nchini Kenya

cri

Msuluhishi wa mgogoro wa kisiasa nchini Kenya ambaye pia ni rais wa Ghana na mwenyekiti wa muda wa Umoja wa Afrika Bw. John Kufour, tarehe 9 alifanya mazungumzo na rais wa Kenya Mwai Kibaki na kiongozi wa Chama cha ODM Bw. Raila Odinga kwa nyakati tofauti, lakini kila upande haukutoa taarifa yoyote baada ya mazungumzo. Wachambuzi wanaona kuwa ingawa hali ya vurugu nchini Kenya imeanza kutulia, lakini mgongano wa kisiasa unaendelea.

Bw. John Kufour aliwasili mjini Nairobi tarehe 8 jioni na kuanza juhudi zake za usuluhishi. Rais wa Kenya Mwai Kibaki alikwenda kumpokea Bw. Kufuor kwenye uwanja wa ndege. Lakini kabla ya kwenda uwanjani bila matarajio ya watu alitoa hotuba kwa njia ya televisheni na redio akitangaza kuteua wajumbe wapya 17 wa baraza la mawaziri na kati ya mawaziri hao aliowateua, hakuna hata mmoja aliyetoka Chama cha ODM. Kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana kiongozi wa Chama cha ODM-Kenya Bw. Kalonzo Musyoka aliyepata nafasi ya tatu ameteuliwa kuwa makamu wa rais. Bw. Mwai Kibaki alisema, atawateua nusu nyingine ya mawaziri hapo baadaye.

Bunge la Kenya lina wabunge 224, kati ya hao wabunge wanaochaguliwa kwa kura ni 210. kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa bunge yaliyotangazwa hivi karibuni, Chama cha ODM kina viti 99, yaani karibu nusu ya viti vyote vya bunge, na hii ni idadi kubwa ya kuzidi idadi ya viti 43 vya Chama cha PNU kinachoongozwa na Rais Mwai Kibaki. Kwa hiyo itakuwa ni vigumu kwa Rais Mwai Kibaki kuunda serikali yake bila kushirikisha vyama vya upinzani, hata serikali ikiundwa utendaji wa serikali hiyo utakumbwa na matatizo mengi kutokana na vyama vya upinzani kuwa na viti vingi bungeni, kwa hiyo inampasa Rais Mwai Kibaki atafute uungaji mkono kutoka chama kingine wakati anapounda serikali. Chama cha ODM-Kenya kina viti 16 kwenye bunge, kwa kuwateua wanachama wa chama hicho kuwa makamu rais na mawaziri Bw. Mwai Kibaki kwa kiasi fulani ametimiza mapendekezo yake ya kuunda serikali ya mpito.

Lakini Chama cha ODM chenye viti vingi hakikushirikishwa kwenye serikali hiyo, serikali yenyewe haitakuwa ya mseto kamili. Kwa hiyo kuhusu uteuzi wa Mwai Kibaki Chama cha ODM kinasema, kinakataa matokeo ya uchaguzi mkuu na pia hakitambui mawaziri walioteuliwa, na kinaona kuwa uteuzi wa Mwai Kibaki utaharibu juhudi za usuluhishi wa kimataifa.

Msemaji wa ikulu ya Marekani Bw. Sean McCormack tarehe 9 alisifu uteuzi wa Mwai Kibaki kuwa ni "hatua ya juhudi", alisisitiza kuwa cha muhimu ni kufanya mazungumzo kati ya vyama vya upinzani na serikali bila vikwazo.

Wachambuzi wanaona kuwa sababu ya Bw. Mwai Kibaki kuteua karibu nusu ya idadi ya mawaziri ni kumshinikiza Raila Odinga na kumwashiria kwamba kama mgongano kati yao unaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo, nusu nyingine ya idadi ya mawaziri itasalia kwa Chama cha ODM. Tarehe 7 Rais Mwai Kibaki kwa mara nyingine tena alimtolea Odinga ishara ya kutaka amani akimwalika kwenye mazungumzo yatakayofanyika tarehe 11 kwenye ikulu ya Kenya. Mwanzoni Bw. Odinga alipinga, lakini baadaye alisema mazungumzo lazima yamshirikishe msuluhishi wa kimataifa Bw. John Kufour.

Kutokana na takwimu zilizotangazwa na serikali ya Kenya, vurugu za uchaguzi mkuu nchini Kenya zimesababisha vifo vya watu wasiopungua 486 na wengie laki 2.5 kupoteza makazi. Wachambuzi wanaona kuwa ingawa hali ya vurugu imeanza kutulia, lakini mgongamo wa kisiasa bado ni mkali. Vyombo vya habari vinasema, mgongano hausaidii utatuzi wowote wa suala hilo ila tu kufanya mazungumzo. Kutokana na usuluhishi wa kimataifa pande mbili zinazovutana zitaweza kufanya mazungumzo au la na matokeo ya mazungumzo yatakuwaje, tutaendelea kufuatilia.

Idhaa ya kiswahili 2008-01-10