Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-11 16:39:05    
Mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel bado yakabiliwa na changamoto

cri

Rais wa Marekani George Bush tarehe 9 na tarehe 10 alifanya ziara nchini Israel na Palestina akijaribu kufufua mazungumzo yaliyosimama kwa karibu mwezi mmoja kati ya Israel na Palestina.

Alipokuwa ziarani, Rais George Bush alifanya mazungumzo na waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert na mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas, matatizo matatu ambayo ni muhimu kwa mazungumzo ya amani yote yaligusiwa. Kabla ya hapo vyombo vya habari viliona kuwa ziara ya Rais George Bush ilikuwa ni kujitukuza tu, lakini kwa kweli katika ziara yake ya siku mbili George Bush alifanya mambo ya maana.

Kwenye mazungumzo Bw. George Bush kwa mara ya kwanza alizungumzia mgogoro wa ardhi. Alisisitiza kuwa utatuzi wa mgogoro wa ardhi unahitaji pande mbili zishauriane na makubaliano ya amani yanahitaji pande zote mbili "zilegeze misimamo kwa uchungu". Rais George Bush alitaka Israel imalize ukaliaji wa ardhi ya Kiarabu ulioanza mwaka 1967, na kuona kwamba makubaliano ya amani lazima yahakikishe Palestina iwe nchi inayomilikiwa na watu wa Palestina na Israel iwe nchi inayomilikiwa na Wayahudi wa Israel, au kwa maneno mengine inamaanisha kuwa "mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel ni lazima yahakikishe kuwa Israel ina mpaka unaokubalika, wenye usalama na unaoweza kulindwa", na huku pia "ni lazima ihakikishe Palestina ina mamlaka ya nchi, uhuru, ukamilifu wa ardhi na uhai wake". Anaona kuwa makubaliano ya amani kuhusu mgogoro wa mpaka "ni lazima yarekebishe mpaka uliowekwa katika vita vya mwaka 1949 kwa mujibu wa hali ilivyo sasa". Rais George Bush alirudia ahadi aliyotoa kwa waziri mkuu wa zamani wa Israel Bw. Sharon akisema "Israel haina haja kuondoa kabisa jeshi lake kutoka ardhi iliyopatikana kwenye vita vya tatu vya Mashariki ya Kati mwaka 1967". Bw. George Bush alipendekeza kutatua matatizo ya wakimbizi wa Palestina kwa kusukuma Palestina iwe nchi na kuanzisha utaratibu wa kuwapa fidia. Kuhusu hadhi ya Jerusalem Rais George Bush hakutoa mapendekezo yoyote, lakini alizitaka pande mbili ziendelee kutafuta ufumbuzi.

Wachambuzi wanaona kuwa yote hayo yameonesha kuwa Rais George Bush alitumia busara sana katika ziara yake akijaribu kupata mafanikio fulani kabla ya yeye kuondoka madarakani mwezi Januari mwaka kesho, lakini pia wanaona kuwa matumaini hayo ya George Bush ni vigumu kutimizwa.

Kwanza, Rais George Bush alikwepa kugusia sababu zilizokwamisha mazungumzo, yaani mradi wa kujenga makazi kwenye sehemu ya mashariki ya Jerusalem na sehemu ya magharibi ya mto Jordan. Kwenye mazungmzo Mahamoud Abbas alisema Palestina haikupata jibu bayana kuhusu lengo la kuweka mji mkuu mjini Jerusalem kwa mujibu wa azimio la Umoja wa Mataifa. Kwa upande mwingine, waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert alikataa matakwa ya Marekani kuhusu kusimamisha miradi ya kujenga makazi ya Wayahudi kwenye sehemu ya mashariki ya Jerusalem, na kuweka sawa hadhi ya Jerusalem na sehemu nyingine za makazi ya Wayahudi, akitarajia kuacha masuala yote husika kwenye mazungumzo kati ya pande mbili. Hii inaashiria kuwa mazungumzo yatakayofanyika yatakuwa magumu.

Pili, ili kuzingatia hisia za pande mbili, Rais George Bush alikuwa na msimamo wa upole katika masuala mengi. Kwa mfano, kwa upande mmoja aliona kujenga makazi ya Wayahudi ni haja ya usalama wa sehemu ya magharibi ya mto wa Jordan, lakini kwa upande mwingine kujenga makazi hayo kumeiletea Palestina matatizo. Msimamo kama huo hauna maana yoyote kwa utatuzi wa matatizo.

Tatu, kuhusu suala la kuweka bayana mpaka ambalo ni muhimu sana katika mgogoro kati ya pande mbili, Rais George Bush ingawa anataka makubaliano ya amani lazima yahakikishe Palestina inakuwa nchi inayomilikiwa na watu wa Palestina, na Israel inakuwa nchi inayomilikiwa na Wayahudi, lakini vyombo vya habari vinaona kuwa George Bush anaipendelea Israel kutokana na maneno aliyosema "kurekebisha mpaka uliowekwa katika vita vya mwaka 1949 kwa mujibu wa hali ilivyo sasa" na "Israel haina haja kuondoa kabisa jeshi lake kutoka kwenye ardhi iliyopatikana katika vita vya mwaka 1967".