Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-14 17:09:15    
Uzalishaji mali katika sekta ya utamaduni mjini Beijing wastawi haraka

cri

Kama wewe ni mpenda sanaa, ukitembelea mji wa Beijing hakika usikose kufika kwenye mtaa wa sanaa No. 798, kwani hapo ni mahali ambapo wasanii zaidi ya mia moja wamekusanyika, na ziko sanaa za kila aina zikiwa ni pamoja na picha za kuchorwa, sanamu za kuchongwa na kufinyangwa, mapambo ya nyumba na picha zilizopigwa kwa kamera. Mtaa huo umekuwa kituo kikubwa cha sanaa mjini Beijing.

Mtaa wa sanaa No. 798 uko karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Beijing. Awali, kwenye sehemu hiyo kulikuwa na kiwanda kikubwa cha vifaa vya redio. Kiwanda hicho kilifungwa katika miaka ya 90 ya karne iliyopita na majengo yote yalikuwa matupu na yalikuwa hayatumiki. Mkurugenzi wa ofisi ya kusimamia mtaa huo Bw. Chen Yongli alisema, bila kutarajiwa majengo hayo yameshikamana na sanaa na kupata uhai mpya. Alisema,

"Sehemu hiyo ilianza kutumika kwa mambo ya sanaa mwaka 1996. Wakati huo ulikuwa ni maadhimisho ya mwaka wa 60 wa vita dhidi ya wavamizi wa Japan, Chuo Kikuu cha Sanaa cha Beijing kilitaka kufanya maonesho ya sanamu za mashujaa wa kupambana na wavamizi wa Japan lakini kilishindwa kupata sehemu kubwa inayoweza kuonesha sanamu hizo, mwishowe kilipata majumba ya kiwanda hicho na kilipanga jumba kubwa lenye eneo la mita za mraba 3,000. Tokea hapo chuo hicho kimekodi jumba hilo kwa ajili ya kufanya maonesho ya sanaa zilizotungwa na wanafunzi wa chuo hicho. Baada ya habari kuenea wasanii wengi walikusanyika hapa."

Katika miaka ya karibuni Beijing imekuwa inasisitiza kuendeleza uzalishaji mali wa sekta ya utamaduni na kuifanya michezo ya Olimpiki ya Beijing iwe ya michezo ya utamaduni kama ni moja ya malengo ya kuandaa michezo hiyo. Kutokana na lengo hilo mtaa wa sanaa No. 798 umestawi haraka kisanaa. Bw. Chen Yongli alisema,

"Mwishoni mwa mwaka 2005 serikali ya Beijing iliamua kuendeleza kwa juhudi uzalishaji mali wa sekta ya utamaduni. Kutokana na maendeleo ya miaka kadhaa, mtaa wa sanaa No. 798 umekuwa unajulikana kimataifa, baada ya kufanya uchunguzi na utafiti serikali ya Beijing inaona kuwa mtaa huo umefikia kipindi chake cha kuwekewa mkakati wa maendeleo, na mwaka 2006 iliamua kuufanya mtaa huo uwe kituo kikubwa cha sanaa mjini Beijing."

Hivi sasa wasanii wengi mashuhuri wamekusanyika hapo. Kwa mujibu wa hesabu iliyofanyika katika mwezi Julai mwaka 1997, kulikuwa na taasisi 354 zilizoshughulikia sanaa yakiwemo maduka ya picha za kuchorwa, ofisi binafsi za uchoraji, studio za kupiga picha za video, matengenezo ya muziki, upigaji wa picha za televisheni na ofisi za kutoa ushauri kuhusu usanifu. Kutokana na hali nzuri ya usafiri na mazingira bora, mtaa huo unajulikana duniani. Bibi Cheng Linghui aliyetoka kisiwa cha Taiwan anaendesha duka la picha za kuchorwa, anaona kuwa mtaa huo unaweza kulingana na sehemu maarufu ya sanaa ya Marekani mjini New York. Alisema,

"Nilikuja mjini Beijing mwaka 1994 na kuonana na mwalimu mmoja wa Chuo Kikuu cha Sanaa cha Beijing, wakati huo nilikuwa na lengo la kufungua duka la picha mjini Shanghai, lakini baada ya kuangalia mtaa huo nilisikitika kwa nini sikufungua duka langu hapa mapema. Kutokana na hadhi, kiwango cha juu cha usanii na sanaa za aina nyingi, mtaa huo unafanana sana na sehemu maarufu ya sanaa SOHO mjini New York."

Kuna sehemu nyingi nyingine kama mtaa No. 798 mjini Beijing. Baada ya kuona kuwa uzalishaji mali katika sekta ya utamaduni utakuwa na mustakbali mzuri, serikali ya Beijing ilianzisha jopo la uongozi la sekta ya utamaduni ili kutunga sera, kustawisha na kusimamia sekta hiyo. Kila mwaka serikali ya Beijing inatenga Yuan milioni 500 kwa ajili ya sehemu zenye mkusanyiko wa biashara nyingi za sanaa.

Naibu meya wa Beijing Bw. Jie Lin alisema uzalishaji mali ambao sekta ya sanaa ikiwa ni sehemu muhimu umekuwa nguvu kubwa ya kuhimiza uchumi wa Beijing. Alisema,

"Hali ya uchumi wa Beijing ni nzuri, na hii ni sababu ya kukua haraka kwa uzalishaji mali wa sekta ya utamaduni. Serikali, makampuni na wakazi wananufaika na mageuzi na maendeleo ya uchumi."

Imefahamika kuwa mwaka 2006 thamani iliyoongezeka katika uzalishji mali wa sekta ya utamaduni ilichukua zaidi ya 70% ya pato la Beijing, katika thamani hiyo mapato kutokana na biashara ya sanaa inachukua zaidi ya nusu. Kutokana na mpango, hadi kufikia mwaka 2010 sehemu zenye mkusanyiko wa biashara nyingi za sanaa zitaongezeka hadi kufikia 30, na kiasi cha mapato kitaongezeka zaidi katika pato la Beijing na kuzifanya sehemu hizo ziwe mhimili mhimu wa uchumi wa Beijing.

Idhaa ya kiswahili 2008-01-14