Makamu wa rais wa Iran ambaye pia ni mwenyekiti wa shirika la nishati ya atomiki ya nchi hiyo Bw. Gholam Reza Aghazadeh alisema, Iran inapenda kutatua masuala yote yaliyobaki kuhusu mpango wake wa nyuklia mwezi Februari mwaka huu.
Bw. Aghazadeh alitoa kauli hiyo tarehe 13, baada ya ziara ya mkurugenzi mkuu wa Shirika la nishati ya atomiki la kimataifa Bw. Mohamed El Baradei nchini Iran tarehe 11 na 12 Januari. Hii ilikuwa ziara ya kwanza ya Bw. Baradei nchini Iran, tokea mwezi Aprili mwaka 2006. Tarehe 13 Januari msemaji wa Bw. Baradei alisema, Iran na Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki zimekubaliana kuwa, katika wiki 4 zijazo zitaanza kutekeleza mpango wa utendaji uliofikiwa na pande hizo mbili mwaka jana. Zaidi ya hayo Iran ilitoa ripoti kwa Bw. Baradei kuhusu mitambo ya kusafisha uranium nzito aina ya P2. Na habari kuhusu mitambo hiyo ya aina mpya iliyosanifiwa na kutengenezwa na Iran inatakiwa sana na Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, kwani itasaidia kufanya uthibitisho wa utekelezaji wa mpango wa nyuklia wa Iran.
Lakini wanadiplomasia wa nchi za magharibi wana maoni tofauti kuhusu taarifa iliyotolewa na Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki, na wana wasiwasi kuhusu uwezo wa Bw. Baradei kuishawishi Iran iache shughuli za kusafisha uranium nzito. Baadhi ya wachambuzi wanasema haiwezekani kutatua masuala yote yaliyobaki kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran katika muda wa hivi karibuni.
Wachambuzi hao wanaona kuwa, baada ya kufanya uchunguzi kwa miaka kadhaa, Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki bado halijafahamu mambo muhimu kabisa kuhusu shughuli za nyuklia za Iran. Shirika hilo na Iran zilikuwa zimefikia makubaliano kuhusu mpango wa utekelezaji mwezi Agosti mwaka jana na Iran ingewasilisha habari nyeti kuhusu suala la nyuklia na kujibu maswali yote yaliyobaki. Lakini mpaka sasa Iran bado haijatekeleza ahadi iliyotoa.
Mbali na hayo lengo kuu la ziara hiyo ya Baradei ni kuishawishi Iran ifanye ushirikiano zaidi na shirika lake, lakini kwenye ziara hiyo hakueleza wazi msimamo wa kuitaka Iran isimamishe shughuli za kusafisha uranium nzito. Na matokeo hayo hayaifurahishi Marekani na nchi washiriki wake wa magharibi. Na ni vigumu kusema kuwa suala la nyuklia la Iran linaweza kutatuliwa bila utatuzi wa suala la kusafisha uranium nzito.
Maendeleo aliyopata Bw. Baradei kwenye ziara yake hiyo nchini Iran yatajulikana kwenye ripoti yake itakayotolewa mwezi Machi mwaka huu, na ripoti hiyo itakuwa msingi muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua uamuzi wa kuiwekea Iran vikwazo vingine au la. Iran imeamua hivi sasa kumpatia Bw. Baradei habari muhimu kuhusu teknolojia za nyuklia ilizo nazo, jambo ambalo linawatia shaka watu, huenda hatua hiyo ya Iran ina lengo la kuwekea ushawishi kwa Bw. Baradei kabla hajaandaa ripoti yake.
Kwenye ripoti kuhusu suala la nyuklia la Iran alizotoa Bw. Baradei siku za nyuma, hakujibu bayana swali la kama Iran inaendeleza silaha za nyuklia au la. Bw. Baradei anatarajiwa kutoa ripoti mpya baada ya miezi mwili. Katika muda huu mfupi, hakuna uwezekano mkubwa kwa Shirika la nishati ya atomiki la kimataifa kuthibitisha kuwa mpango wa nyuklia wa Iran hautekelezwi kwa amani. Ziara hiyo ya Bw. Baradei huenda inasaidia kuifanya Iran iharakishe kufanya ushirikiano na shirika hilo, lakini bado ni mapema mno kufikia uamuzi kuwa, Iran inaweza kutatua masuala yote yaliyobaki kuhusu mpango wake wa nyuklia ndani ya wiki nne zijazo.
|