Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-14 20:29:47    
Misitu ya Shennongjia ya mkoani Hubei, China

cri

Kwenye mkoa wa Hubei ulioko kwenye sehemu ya kati ya China, kuna misitu maarufu ya asili ya Shennongjia, mazingira ya asili ya ikolojia ya sehemu hiyo yamehifadhiwa vizuri kutokana na watu kufika kwenye sehemu hiyo mara chache, sehemu hiyo imekuwa bohari muhimu la raslimali za mimea na wanyama pori la nchini China.

Wapendwa wasikilizaji, milio mnayoisikia ni milio ya kima wenye manyoya ya rangi ya dhahabu, wanyama hao wanahifadhiwa kitaifa nchini China. Tukisema sehemu ya Shennongjia ni bohari la wanyama na mimea pori la China, kabisa hatutii chumvi, sehemu hiyo yenye eneo la zaidi ya kilomita za mraba 3,000, ina wanyama na mimea wa zaidi ya aina 4,700, na aina zaidi ya 60 za wanyama na mimea zinawekewa mkazo na serikali kuhifadhiwa nchini China.

 

Toka miaka ya 70 ya karne iliyopita, miti ya misitu ya asili ya huko ilikatwa ovyo, maisha ya wanyama pori yalikabiliwa tishio kubwa. Hali mbaya ya ikolojia ya huko ilizingatiwa na serikali pamoja na wataalamu husika wa China, mwezi Machi mwaka 2000 mradi wa kuhifadhi misitu ya asili ya Shennongjia ulizinduliwa, na kupiga marufuku kukata miti ya sehemu hiyo. Baada ya jitihada za zaidi ya miaka 7, eneo la misitu limefikia 88% ya sehemu ya Shennongjia, wakati misitu imefikia zaidi ya 96% kwenye sehemu muhimu ya Shennongjia. Mabadiliko ya ikolojia ya sehemu ya Shennongjia yameleta mazingira bora kwa maisha ya wanyama pori. Mlinzi wa misitu Bi Jiang Lingling anashughulikia hifadhi ya misitu ya Shennongjia tangu miaka michache iliyopita, alisema,

"Tangu mradi wa kuhifadhi misitu ya asili uanzishwe mwaka 2000, kima wenye manyoya ya rangi ya dhahabu, Caragana wenye matumbo ya rangi nyekundu pamoja na mbuzi pori wanaonekana kwenye kila mlima wa sehemu hiyo, hivi sasa milima imebadilika kuwa ya rangi ya kijani na maji yamebadilika kuwa safi."

Hivi sasa sehemu ya Shennongjia imekuwa na mazingira mazuri, na wakazi wa huko wanafanya shughuli za uzalishaji mali zisizoleta athari mbaya kwa mazingira ya kimaumbile. Ofisa wa sehemu ya misitu ya Shennongjia, Bw. Qian Yuankun alisema,

"Wakazi wa sehemu ya Shennongjia baada ya kufanya vizuri kazi za kuhifadhi mazingira ya ikolojia, wanaendeleza shughuli za dawa za miti-shamba na ufugaji wa nyuki kwa kutumia raslimali za milimani, hivi sasa pato la familia za wafanyakazi wa misitu limeongezeka kwa udhahiri."

 

Uzalishaji mali wa namna hiyo isiyoleta athari mbaya kwa mazingira ya maumbile ni kilimo cha ikolojia inayoendelezwa kwa nguvu kwenye sehemu ya misitu ya Shennongjia, vijiji 35 kati ya vijiji 81 vya huko vimekuwa vijiji vinavyoshughulikia kilimo cha ikolojia. Licha ya shughuli za upandaji miti na ufugaji, shughuli za utalii wa ikolojia pia zimeanzishwa kwenye sehemu hiyo.

Sehemu zote zenye mandhari nzuri na vivutio ziko ndani ya milima ya kijani, hata watalii wakienda huko katika majira ya joto, wanafurahi na kuburudishwa kwa upepo mwororo. Vitu wanavyoona watalii ni miti mingi mikubwa na sauti wanayosikia ni milio ya wanyama pori wa aina mbalimbali pamoja na sauti ya mtiririko wa maji kwenye mabonde. Katika miaka ya hivi karibuni, sehemu 4 zenye mandhari nzuri zimejengwa kwenye sehemu ya misitu, na idadi ya watalii wanaokwenda kuitembelea sehemu hiyo inazidi laki 6 kwa mwaka. Tarafa ya Muyu ni mahali panapotembelewa na watalii wengi, karibu wakazi wote wa eneo hilo wanashughulikia kazi za utalii au kazi zinazohusiana na utalii. Bw. Li Shikai anayemiliki mkahawa kwenye tarafa ya Muyu, alisema,

"Tangu kuanzishwa kwa shughuli za utalii kwenye sehemu ya Shennongjia, pato la wakazi wa sehemu hiyo limeongezeka kwa udhahiri, lakini ongezeko la watalii pia limeleta shinikizo kwa mazingira ya ikolojia ya sehemu ya misitu. Ili kuhifadhi mazingira ya ikolojia, maslahi ya shughuli za kiuchumi yamewekwa katika nafasi ya pili, kuhifadhi mazingira ya maumbile pamoja na mimea na wanyama pori adimu yanayotegemewa sana na wakazi wa huko, kumekuwa mambo yanayozingatiwa kila dakika na serikali ya sehemu hiyo, ofisa wa serikali ya sehemu ya Shennongjia, Bw. Qian Yuankun alisema,

"Wakati tunapohimiza maendeleo ya uchumi na jamii ya sehemu ya Shennongjia, daima tunatilia mkazo hifadhi ya mazingira ya ikolojia, na tunaiweka kazi hiyo katika nafasi ya mbele kabisa, na kutatua vizuri mgongano kati ya maendeleo ya uchumi na hifadhi ya mazingira ya maumbile."

 

Ili kufanya marekebisho kuhusu makazi ya wanyama pori wa zaidi ya aina 1,000 walioko kwenye sehemu za mandhari na kuboresha mazingira ya ikolojia ya sehemu hiyo inayosifiwa kama ni "bohari la gene za viumbe vya aina mbalimbali", sehemu ya misitu ya Shennongjia ilisitisha shughuli za utalii kwa zaidi ya miezi miwili kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Machi mwaka 2006. Ingawa kitendo hicho kilileta usumbufu kwa watalii, lakini kitendo hicho kilikuwa ni cha lazima. Kutokana na hifadhi na marekebisho yaliyofanywa kwa mfululizo katika miaka michache iliyopita, mazingira ya ikolojia ya sehemu ya Shennongjia yanaboreshwa siku hadi siku, na idadi ya wanyama pori pia inaongezeka kwa mfululizo. Katika mwaka uliopita wataalamu husika wa Uingereza, Marekani na Mexico walikwenda kufanya uchunguzi Shennongjia, na walisifu sana aina nyingi za viumbe na hali nzuri ya ikolojia na misitu ya asili ya huko.

Wapendwa wasikilizaji, idadi ya kima wenye manyoya ya rangi ya dhahabu kwenye sehemu ya Shennongjia imeongezeka hadi kufikia zaidi ya 1,200 kutoka zaidi ya 600 hapo awali. Sasa kima wenye manyoya ya rangi ya dhahabu wamekuwa kivutio maalumu kwenye sehemu ya Shennongjia. Bw. Qian Yuankun anafurahi sana kila anaposikia milio ya kima hao, alisema,

"Tumehifadhi vizuri sehemu ya Shennongjia, hivi sasa idadi ya kima wenye manyoya ya rangi ya dhahabu inaongezeka kwa mfululizo, eneo la maisha ya kima hao pia linaendelea kupanuka, na kuwa na kivutio kikubwa zaidi, sehemu ya Shennongjia itakuwa na mazingira mazuri na kuwa maskani ya kupatana kati ya binadamu na maumbile."