Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-15 16:32:49    
Barua0115

cri
Msikilizaji wetu Paul Mungai Mwangi wa sanduku la posta Injinia North Kinangop, Kenya ametuletea barua akisema kuwa, kwanza shukrani zake za dhati zitufikie wafanyakazi wa idhaa hii ya Kiswahili kwa jinsi tunavyoshughulikia vipindi vyote, maelezo ya watangazaji pia ni kemkem na hueleweka bila tatizo lolote. Wanaomba tuendelee vivyo hivyo.

Hata hivyo angependa idhaa hii itangazie kwa kina swala la ukabila ambao ni janga linaloangamiza bara zima la Afrika. Ukabila umekita mizizi katika mataifa mengi ya Afrika tangu nchi hizo zilipopata uhuru wao kutoka kwa wakoloni. Vita vya kikabila vilizuka punde tu baada ya kuondoka wazungu na katika nchi kama Somalia na sehemu ya Darfur iliyoko kusini mwa Sudan damu nyingi ya binadamu yanaendelea kumwagika. Hata leo, Kenya ni mojawapo ya nchi chache sana ambayo licha ya kuwa na makabila 42, imetunukiwa zawadi ya amani tangu uhuru. Hata hivyo ukabila umeleta athari kwa baadhi ya watu. Matamshi yao huwasha cheche za mto na kuzusha uhasama kati ya makabila yanayoishi pamoja.

Kupitia kipindi cha makabila madogomadogo nchini China, Radio China Kimataifa inaweza kusaidia kumaliza janga hili kwa kuelezea jinsi makabila mengi ya China huishi kwa masikilizano, na kuepusha dhana kuwa ukabila hauwezi kuangamizwa kwa sababu ya makabila mengi yaliyoko katika nchi za Afrika. Wingi wa makabila yafaa uchukuliwe kama utajiri wa tamaduni za nchi husika.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu huyo Paul Mungai Mwangi kwa barua yake ya kutuelezea maoni yake kuhusu ukabila. Kweli nchini China kwa jumla kuna makabila 56, kabila ya wahan ni kabila kubwa kabisa, na makabila mengine 55 ni madogomadogo, lakini serikali ya China inafuata kwa makini sera kuhusu kuishi pamoja kwa masikilizano kati ya watu wa makabila mbalimbali, hasa kutilia maanani kuwasaidia makabila madogomadogo kujiendeleza. Kwa mfano, mkoani Yunnan, kusini magharibi mwa China, wanaishi watu wa makabila mengi madogomadogo, lakini watu wa makabila hayo wanaishi pamoja kwa amani na masikilizano, ambapo wanafanya juhudi za kuendeleza uchumi na jamii. Hali kadhalika kwa mkoa unaojiendesha wa Tibet. Kwa watu wote wanavyojua, kila kabila lina desturi na mila zao na utamaduni wao, hizo ni kama ni mali za taifa, tukifanya juhudi kubwa kuenzi mila na utamaduni wa makabila mbalimbali, tutapata manufaa zaidi, na kuweza kuwafanya watu wa makabila mbalimbali waishi pamoja katika hali nzuri zaidi ya masikilizano na kujitahidi kujenga taifa lao.

Msikilizaji wetu Magembe Jackson wa sanduku la Posta 356 Milambo Sekondari Tabora, nchini Tanzania, kwenye barua yake ameanza kwa salamu kwa wasikilizaji na watangazaji, na anasema kuwa yeye ni mzima. Anasema yeye ni miongoni mwa watu wanaohamasika na matangazo ya Radio China Kimataifa. Hivyo basi kutokana na hilo anaomba tumtumie ratiba ya vipindi ambavyo tunatangaza, hasa vinavyohusu Historia ya China, Uchumi na Teknolojia nchini China.

Msikilizaji wetu mwingine Bw Joseph Mukaburu Wasike wa sanduku la Posta 89 Bungoma, Kenya, ameanza kwa kusema yeye na mashabiki wenzake kutoka Khachonge Muungano salamu klabu wanatusalimu sana. Wanatushukuru sana kwa barua na salamu wanazopata kupitia Radio China Kimataifa, na wanapenda tuendelee kuwaandikia na kuwapa habari zaidi kuhusu China. Mbali na salamu, wanasema wanashukuru pia kwa habari kuhusu michezo ya olimpiki, itakayofanyika mwaka huu hapa Beijing.

Anasema wao wanapenda sana tuzidi kuwapa habari kuhusu michezo hiyo, na kama ikiwezekana tuwatumie picha nyingi zaidi kuhusu michezo hiyo ya olimpiki, na kama ingewezekana wanasema, wangependa sana kuja china kuona michezo hiyo wao wenyewe, lakini hawana njia. Hivyo basi wanasema wanategemea sana habari zetu kwa wingi. Mwisho wanasema wanatuombea tu kila la heri kwenye kwa kazi yetu, na tuendelee kuwasiliana mara kwa mara.

Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu Magembe Jackson na Joseph Mukaburu Wasike kwa barua zao za kutoa maoni kuhusu vipindi vyetu, maoni yao ni mazuri, tunapoandaa vipindi vyetu hakika tutazingatia kwa makini maoni na mapendekezo yao. Na mwaka huu habari kuhusu Michezo ya Olimpiki ya Beijing hakika zitakuwa kemkem.

Msikilizaji wetu mwingine Nazael Piniel wa sanduku la Posta 30 Arusha, Tanzania. Ameanza barua yake kwa kutoa pongezi kwa waandaaji wa vipindi, watangazaji na wasikilizaji wote wa Radio China Kimataifa. Anasema yeye anafurahia matangazo yetu, na anapenda kufahamu lugha mbalimbali, ikiwemo lugha ya kichina, kwani anavutiwa sana na lugha ya kichina, ingawa hajasikiliza kipindi kipya cha mafunzo ya lugha ya Kichina tangu tulipoanza kurusha kipindi hicho.

Anaendelea kusema kuwa alianzia kusikiliza kipindi cha Jifunze kichina katikati, hivyo yale aliyojifunza ameyaelewa kidogo na anapenda kuelewa zaidi ili aweze kuijua lugha ya kichina kwani anaipenda sana. Na kama inawezekana anaomba tumtumie jarida lililoanza tangu mwanzo au kitabu chochote ambacho anaweza kusoma na kuelewa zaidi, pamoja na kanda ya wimbo wa kichina. Mwisho anatutakia kazi njema na moyo wa kuendelea kufundisha kichina.

Tunamshukuru Nazael Piniel kwa barua yake, kuhusu kipindi cha jifunze kichina, hakika tutafanya juhudi kubwa zaidi kuandaa vizuri kipindi hiki. Kutokana na sababu mbalimbali, katika siku zilizopita kipindi hiki kilikuwa cha marudio, lakini kuanzia mwezi ujao, tutatangaza vipindi mfululizo kwa mujibu wa kitabu rasmi tulichopata.

Msikilizaji wetu Pius Bitamale wa sanduku la Posta 3030 Mwanza Tanzania, ameanza barua yake kwa kuwasalimia wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa na kutupa pole kwa kazi za kila siku, lakini akiwa na matumaini kuwa hatujambo na tunaendelea kuchapa kazi. Anasema ni mzima, na lengo la barua yake ni kutaka kutushukuru kwa kumjibu barua yake na kumtumia kadi za salamu pamoja na maua mawili, vitu hivyo vyote vilifika salama bila matatizo yoyote. Anasema kuwa kwa muda kidogo hakufuatilia sana matangazo ya Radio China Kimataifa, kwa kuwa alibanwa na masomo hakuweza kutuandikia barua lakini sana ana muda wa kutosha.

Anaendelea kusema, anafikiri kuwa Radio China kimataifa inachukua nafasi ya kwanza kwa kuwajali wasikilizaji wake. Anaomba tuendelee na utaratibu huo na pia anaomba tutayarishe fomu za wasikilizaji kwa ajili ya kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusu vipindi wanavyosikiliza. Na kwa kuwa bado anaendelea kupokea bahasha zilizokwishalipiwa gharama za stempu, ataendelea kuwasiliana nasi mara kwa mara.

Msikilizaji wetu Francis Oduko Magio wa sanduku la Posta 4 Mubwayo Hakati, Kenya. Yeye kwenye barua yake aliyotuandikia, kwanza ameanza kwa kututaka wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa tupokee salamu na shukurani nyingi. Anashukuru sana kwa kadi za salamu pamoja na picha za viwanja mbalimbali vya michezo ya olimpiki ya Beijing. Anasema hakika hata kama hajafika China kujionea kwa macho yake maandalizi ya michezo hiyo, lakini hizo picha zinamuonesha jinsi mambo yalivyopendeza. Anamaliza barua yake kwa kusema, kwa kuwa anapenda kusoma sana, anasema kama inawezekana anaomba tumtumie magazeti ama kitabu kinachoeleza mengi kuhusu Radio China Kimataifa na China.

Tunawashukuru kwa dhati wasikilizaji wetu Pius Bitamale na Francis Oduko Magio na wasikilizaji wengine waliotutumia barua za kueleza maoni na mapendekezo. Ni matumaini yetu kuwa, mtaendelea kutufuatilia, kusikiliza matangazo yetu na kutuletea maoni na mapendekezo ili tujitahidi kwa pamoja kuandaa vizuri vipindi vyetu mbalimbali.

Idhaa ya kiswahili 2008-01-15