Rais George Bush wa Marekani tarehe 16 mwezi Januari alimaliza ziara yake ya siku 8 kwenye sehemu ya mashariki ya kati, na alirudi nchini Marekani kutoka Misri. Katika ziara hiyo rais Bush alitumia muda mwingi kutembelea nchi nne za Kuwait, Bahrain, Umoja wa falme za kiarabu na Saudi Arabia, "Iran ni tishio kubwa dhidi ya usalama wa sehemu ya ghuba" yalikuwa ni maneno aliyoyasema mara kwa mara katika ziara hiyo. Sababu muhimu ya Bw Bush kutilia mkazo wa ziara yake katika sehemu ya ghuba ni kuwa,
Hivi sasa athari ya Iran katika sehemu hiyo inaongezeka siku hadi siku. Katika mwezi Machi na mwezi May ya mwaka uliopita, rais Mahmoud Ahmadinejad alitembelea Saudi Arabia na Umoja wa falme za kiarabu. Mwezi Desemba Bw Ahmadinejad alishiriki kwenye mkutano wa wakuu wa nchi wa kamati ya ushirikiano wa nchi za kiarabu za sehemu ya ghuba kutokana na mwaliko wa mfalme Hamad bin Khalifa, hapo baadaye alikwenda Mecca kushiriki shughuli za kuhiji za dini ya kiislamu kutokana mwaliko wa mfalme wa Saudi Arabia. Shughuli nyingi za kidiplomasia za rais Ahmedinejad kwenye sehemu ya ghuba zinamfanya rais Bush aone kuwa endapo hataboresha uhusiano na nchi za sehemu ya ghuba, pindi Marekani itakapokabiliana kijeshi na Iran, huenda nchi hizo zisiiunge mkono Marekani. Hivyo, hakuwa na budi kufanya ziara katika nchi za ghuba mara tu baada ya kuingia mwaka 2008 ili kugombea kuwa na ushawishi wake kwenye sehemu hiyo.
Rais George Bush alikuwa na sababu za kuzitembelea nchi hizo. Katika nchi 6 za sehemu ya ghuba, Bush alichagua Saudi Arabia, Umoja wa nchi za falme za kiarabu, Bahrain na Kuwait, lakini Qatar, ambayo pia ni nchi muhimu kwenye sehemu ya ghuba, haimo kwenye nchi alizotembelea. Wachambuzi wanaona kuwa, sababu yake ni Qatar kumwalika Bw Ahmedinejad kushiriki mkutano wa wakuu wa nchi wa ushirikiano wa nchi za ghuba mwezi Desemba mwaka uliopita. Bw Bush kutoitembelea Qatar ni kutokana na uhasama. Sababu za kutembelea Umoja wa falme za kiarabu na Bahrain ni kuwa Umoja wa nchi za falme za kiarabu imekuwa ikigombana na Iran kuhusu suala la mamlaka ya visiwa vitatu, wakati Bahrain ina uhusiano mbaya na Iran katika suala la umiliki wa mamlaka ya nchi. Vyombo vya habari vya Iran vilitangaza kuwa, Bahrain ni ardhi ya Iran, jambo ambalo linapingwa vikali na watu wa Bahrain. Rais Bush alifanya ziara katika nchi zenye migogoro na Iran kwa lengo la kupunguza athari ya Iran kwenye sehemu ya ghuba.
Mbali na hayo, lengo lingine la ziara ya Bw Bush kwenye nchi za ghuba ni kutaka kupimana na Iran katika suala la uchumi. Nchi za ghuba zina raslimali nyingi ya mafuta, na raslimali ya mafuta na gesi za Iran pia ni nyingi. Hivi sasa bei ya mafuta duniani inapanda sana, ambapo nchi za ghuba na Iran zimenufaika kutokana na hali hiyo. Katika suala la kudumisha bei kubwa ya mafuta, nchi za ghuba na Iran zina maslahi ya pamoja, tena zinaungana mkono kwa kiwango fulani. Lakini kwa Marekani nchi inayotumia nishati nyingi, haifurahii kuona nchi za ghuba kuwa na msimamo wa namna moja pamoja na Iran kuhusu suala la bei ya mafuta. Bw Bush alisema tarehe 15 nchini Saudi Arabia kuwa, bei kubwa ya mafuta inaleta athari mbaya sana kwa maendeleo ya uchumi wa Marekani, anatarajia kuwa OPEC na Saudi Arabia zitaongeza utoaji mafuta. Endapo lengo la Bush linatimizwa, hii itakuwa kama ni kuleta mvutano kati ya Iran na nchi za ghuba.
Mwishoni kuvutana na Iran kuhusu suala la usalama wa kikanda pia ni jambo muhimu katika ziara ya Bw Bush kwenye sehemu ya ghuba. Hivi sasa Marekani imekwama katika suala la usalama wa Iraq. Kutokana na wasiwasi wa kuathiriwa na hali isiyo ya utulivu ya nchi jirani ya Iraq, nchi za sehemu ya ghuba zinatarajia Marekani iisaidie Iraq kurejesha hali ya utulivu na kulinda usalama wa sehemu hiyo. Ingawa nchi za ghuba hazipendi kuona Iran inakuwa na nguvu kubwa kwenye sehemu hiyo, lakini kutokana na kuishiwa mbinu nzuri kwa Marekani, baadhi ya nchi za ghuba hazina la kufanya ila tu kuimarisha mawasiliano na Iran ili kuleta hali ya utulivu kwenye sehemu hiyo. Bw Bush alisisitiza mara kwa mara kuwa, Iran ni tishio kubwa kwa sehemu hiyo, hali halisi ni kuwa anasisitiza kuwa Marekani ni nguvu muhimu ya kulinda usalama wa sehemu hiyo.
|