Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-18 19:46:34    
Kwa nini nchi za Ghuba zajitahidi kuisogelea karibu Iran?

cri

Hivi karibuni Rais George Bush alipokuwa ziarani kwenye nchi za Ghuba alijitahidi kutangaza fikra yake kuhusu "tishio la Iran" ili kuitenga zaidi Iran. Lakini alipoondoka tu nchi za Ghuba zikatangaza kuwa zitaendelea kuimarisha uhusiano na Iran.

Tarehe 17 waziri wa mambo ya nje wa Falme za Kiarabu Bw. Abdullah alipokutana na balozi wa Iran alisisitiza kwamba nchi ya Falme za Kiarabu itaweka kipaumbele uhusiano kati yake na Iran, alisema hakuna chochote kinachoweza kuathiri uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili, na serikali ya Falme za Kiarabu itaendeleza uhusiano wa kirafiki kwa pande zote kati ya nchi hizo mbili. Siku hiyo hiyo naibu waziri mkuu wa Kuwait ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje Bw. Mohammed Sabah kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema, Kuwait inathamini sana uhusiano kati yake na Iran na itastawisha uhusiano huo wenye maana ya mkakati. Na Bw. Saud al Faisal wa Saudi Arabia, nchi ambayo ni kubwa kati ya nchi za Ghuba, tarehe 15 alisema "Iran ni nchi jirani yetu, na ni nchi kubwa katika ukanda wetu, hatuna sababu ya kupingana nayo." Yote hayo yameonesha kwamba fikra za George Bush kuhusu "tishio la Iran" hazipokelewi sana. Wachambuzi wanaona kuwa hivi karibuni vitendo vya nchi za Ghuba vimeonesha kuwa nchi hizo zimekomaa katika mambo ya kidiplomasia. Sababu yao ya kufanya hivyo inatokana na maslahi yao binafsi.

Kwanza nchi za Ghuba zikiwa ni pamoja na Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Oman, Qatar, Kuwait na Bahrain, hazipakani na Iran lakini ni nchi zilizo karibu zikitazamana na Iran kupitia bahari. Ingawa nchi hizo sio maskini sana kwa kutegemea mafuta, lakini nchi hizo karibu zote ni ndogo, hazina nguvu kubwa za kijeshi. Mashariki ya Kati siku zote ni nchi zenye hatihati, msukosuko wa kisiasa unaoendelea katika ukanda huo unazipasa nchi hizo ziweke usalama wao kwa nchi kubwa. Kwa hiyo toka muda mrefu uliopita nchi hizo zilikuwa zikijitahidi kuweka uhusiano mzuri na Marekani, ni nchi zinazoitii sana Marekani.

Lakini tokea mwaka 2003 baada ya Marekani kuanzisha vita dhidi ya Iraq, hali ya kisiasa kwenye sehemu ya Mashariki ya Kati imebadilika kuwa mbaya. Hali hiyo imezifahamisha nchi za Ghuba kuwa usalama wao hauwezi kuhakikishwa kwa nchi moja tu, "jirani anaweza kusaidia zaidi kuliko jamaa aliye mbali", kwa hiyo kuweka uhusiano mzuri na Iran ni busara iwapo hawataiudhi Marekani.

Pili, mpaka sasa uwezekano wa Marekani kutumia mabavu dhidi ya Iran bado upo, kutokana na hali hiyo nchi za Ghuba hazitaki kubururwa vitani na Marekani. Baadhi ya vyombo vya habari vinasema, maneno ya Rais George Bush kuhusu "tishio la Iran" ni ishara tu ya tishio, nchi za Ghuba zilizoathirika vibaya kutokana na vita vya Iraq hazitaki kutokea tena kwa vita karibu nao. Imefahamika kuwa vita dhidi ya Iraq vimezitia hasara sana nchi za Ghuba, shughuli za uchukuzi, utalii, na mambo ya fedha zimezorota vibaya, bei ya bidhaa ilipanda kwa kiwango kikubwa. Licha ya hayo, ili kujilinda usalama wao ilizipasa nchi hizo kununua silaha nyingi za kisasa.

Aidha, kama Marekani ikianzisha vita dhidi ya Iran mlango wa bahari wa kusafirisha mafuta hakika utafungwa, mapato ya nchi za Ghuba kutokana na mafuta yatapungua kabisa. Tarehe 16 gazeti la Saudi Arabia lilichapisha makala ikisema kama Bw. George Bush akitaka Mashariki ya Kati iwe na amani, ni lazima aheshimu haki ya watu wa kanda hiyo kuishi kwa utulivu, aache msimamo wake dhidi ya Iran aache wazo la kuanzisha vita. Ni wazi kwamba watu wa nchi za Ghuba wanapinga kabisa kuwepo kwa vita vya Marekani dhidi ya Iran. Na kujisogeza karibu na Iran, kwa kiasi fulani kunapunguza uwezekano wa kuanzisha vita.

Kuna haja ya kusema kwamba kusogea karibu na Iran hakuna maana ya kuwa mbali na Marekani. Wakati nchi hizo zinapogusia uhusiano na Iran hazijasahau kusisitiza kudumisha urafiki wa jadi na Marekani.