Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-29 15:31:22    
Timu ya riadha ya China yajiandaa kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing

cri
Ili kujiandaa kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008, timu ya riadha ya China imeanza kufanya mazoezi katika majira ya baridi, na hiki ni kipindi muhimu kwa timu ya China kuongeza uwezo wake. Mwaka 2007 timu ya riadha ya China ilipata mafanikio mbalimbali. Kwenye Mashindano ya riadha duniani yaliyofanyika huko Osaka, timu ya China ilipata medali moja ya dhahabu, moja ya fedha na moja ya shaba, na kushika nafasi ya 11 kwenye orodha ya medali, na hayo ni mafanikio makubwa zaidi iliyopata timu ya China tokea Mashindano ya riadha duniani yaliyofanyika huko Monte Carlo mwaka 1993; Kwenye mashindano ya riadha ya Asia, timu ya China ilipata medali saba za dhahabu, tano za fedha na nne za shaba, na kushika nafasi ya kwanza tena barani Asia.

Aidha wachezaji hodari wa China pia walipata mafanikio makubwa: mwaka 2007 Zhou Chunxiu alipata ubingwa kwenye mashindano ya mbio za Marathon kwa wanawake yaliyofanyika huko London ambayo ni mashindano maarufu zaidi duniani. Akizungumzia sababu ya kupata mafanikio hayo makubwa, kocha mkuu wa timu ya riadha ya China Bw. Feng Shuyong alisema:

"Naona kuwa mafanikio hayo yalitegemea juhudi tulizofanya katika miaka kadhaa iliyopita. Katika miaka ya hivi karibuni tumekuwa tukifanya uchunguzi kuhusu umaalum wa michezo mbalimbali, ili kuwasaidia makocha kupata ufahamu mzuri zaidi kuhusu michezo ambayo wanatoa mafunzo, na kufanya mazoezi vizuri zaidi."

Mafanikio yaliyopatikana katika mwaka 2007 yalitia moyo sana timu ya riadha ya China, na kuweka msingi mzuri zaidi kwa timu hiyo kupata mafanikio makubwa zaidi, pia yameihimiza timu ya riadha ya China kufanya maandalizi kwa juhudi kubwa zaidi kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008. Hivi sasa wachezaji wa michezo mbalimbali ya timu ya riadha ya China wanafanya mazoezi ya majira ya kipindi cha kwanza ya baridi katika sehemu mbalimbali nchini China.

Hayo vilevile ni mazoezi ya mwisho katika majira ya baridi kabla ya Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, na hali ya mazoezi hayo inahusiana sana na matokeo ya wanariadha wa China kwenye Michezo ya Olimpiki, hivyo mazoezi hayo yanaitwa na kocha mkuu Bw. Feng Shuyong alisema ni ya kujiandaa katika "kipindi cha mwisho kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki". Alisema mazoezi ya kipindi cha kwanza katika majira ya baridi yamepata maendeleo mazuri. Bw. Feng Shuyong alijumuisha hali ya mazoezi hayo akisema:

"Hadi sasa mazoezi hayo yamefanyika kwa miezi miwili na kupata mafanikio yanayotufurahisha. Wachezaji wengi wamemaliza mazoezi kwa kufuata mpango uliowekwa."

Kati ya wanariadha mbalimbali, mchezaji maarufu Liu Xiang pia anafanya mazoezi kwenye uwanja wa michezo. Hivi sasa watu wakitaja mchezo wa riadha wa China, humtaja mwanariadha huyo aliyepata ubingwa wa mbio za mita 110 za kuruka viunzi kwa wanaume kwenye Michezo ya Olimpiki ya Athens. Akiwa mchezaji bora wa timu ya riadha ya China, Liu Xiang ameonesha mara kwa mara uwezo wake kutokana na mafanikio aliyoyapata, hususan baada ya kupata ubingwa kwenye mbio za mita 100 kwa wanaume kwenye mashindano ya riadha duniani yaliyofanyika huko Osaka mwaka 2007.

Hivi sasa michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 inakaribia, Liu Xiang anafanya mazoezi katika majira ya baridi mjini Beijing. Mazoezi ya kipindi hiki ni muhimu sana kwa hali ya afya na uwezo wa ushindani kwa Liu Xiang, hivyo yanawekewa mkazo mkubwa. Bw. Sun Haipin ambaye ni kocha wa Liu Xiang alieleza hali halisi kuhusu mazoezi hayo akisema:

"Kwa ujumla hali ya mazoezi ya Liu Xiang inanifurahisha. Kwani Liu Xiang hakuvaa viatu vyenye njumu kwenye mazoezi yaliyofanyika mjini Shanghai, na hali yake ya kufanya mazoezi mjini Beijing baada ya kuvaa viatu vyenye njumu inanifurahisha."

Hadi sasa maandalizi ya Michezo ya Olimpiki yameingia kwenye kipindi cha mwisho. Je, wachezaji wa riadha wa China wana mipango gani ya kufanya mazoezi na kushiriki kwenye mashindano mbalimbali? Kocha mkuu Feng Shuyong alieleza kuwa, mashindano ya riadha ya China yatafanyika kuanzia tarehe 26 hadi 27 Januari mwaka 2008 na kuanzia tarehe 30 hadi 31 Januari mwaka 2008, na China itatuma wachezaji 18 kushiriki kwenye Mashindano ya kirafiki ya riadha ya ubingwa wa dunia yatakayofanyika mwezi Machi mwaka huu, na wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kushiriki kwenye mashindano yaliyofanyika nchini Hispania watashiriki kwenye mashindano ya riadha yatakayofanyika mwezi Februari nchini Australia. Aidha wanariadha wa China watashiriki kwenye mashindano mbalimbali yatakayofanyika kuanzia mwezi Mei hadi Julai katika nchi za Japan, Marekani na barani Ulaya.

Akizungumzia kazi ya kuwachagua wachezaji watakaoshiriki kwenye Michezo ya Olimpiki, kocha mkuu Feng Shuyong alisema, kutokana na mpango, orodha za wachezaji wa mchezo wa kutembea (foot race) na mbio za Marathon zitaamuliwa mwezi Januari na mwezi Aprili mwaka 2008, na wengine wataamuliwa baada ya Mashindano ya riadha ya kimataifa yatakayofanyika kuanzia tarehe 21 hadi 24 mwezi Mei.

Ingawa timu ya riadha ya China ilipata mafanikio makubwa katika mwaka 2007, na mazoezi ya majira ya baridi yanaendelea vizuri, lakini kiwango cha mchezo wa riadha bado kiko nyuma kikilinganishwa na cha nchi zenye uwezo mkubwa duniani. Bw. Feng Shuyong ana ufahamu mzuri kuhusu kiwango cha mchezo wa riadha bado kiko nyuma kikilinganishwa na kile cha nchi zenye uwezo mkubwa duniani. Bw. Feng Shuyong ana ufahamu mzuri kuhusu kiwango cha mchezo wa riadha wa China duniani. Akizungumzia kuhusu Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 Bw. Feng Shuyong alisema:

"Hadi sasa ni miezi minane tu imebaki kabla ya kufunguliwa kwa Michezo ya Olimpiki ya Beijing. Tunapaswa kuona kuwa uwezo wetu bado si mkubwa, na tunakabiliwa na wapinzani wenye uwezo mkubwa, hivyo tunapaswa kufanya juhudi kubwa wakati tunapojiandaa kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki."

Idhaa ya kiswahili 2008-01-29