Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-21 18:12:24    
Kijiji cha mashairi ya Taohua cha nchini China

cri

Sijui kama mmewahi kufika sehemu ya vijijini ya China. Huko licha ya kuweko kwa mandhari nzuri ya mashamba, watalii pia wanaweza kuona utamaduni wa jadi wa sehemu ya vijiji wenye utaalamu wa huko. Kwenye mkoa wa Sichuan ulioko sehemu ya kusini magharibi mwa China, kuna kijiji kimoja kinachoitwa "kijiji cha mashairi ya Taohua" kinachojulikana kwa utungaji wa mashairi, na neno la Taohua ni maua ya mpichi.

Wapendwa wasikilizaji, wimbo mnaosikia sasa ni wimbo wa kienyeji wa huko unaoitwa "kutoka Longquan hadi mji wa Chengdu". Aliyeimba wimbo huo ni mzee Zeng Mingfang mwenye umri wa miaka 72 mwaka huu, mzee huyu anaishi kwenye kijiji cha Taoyuan cha tarafa ya Shanquan ya mji wa Chengdu. Kijiji cha mashairi ya Taohua nilichokitaja kiko kwenye eneo hilo, isipokuwa kijiji cha mashairi ya Taohua ni jina lingine la kijiji hicho kilichopewa na watalii. Inasemekana kuwa katika majira ya Spring ya miaka zaidi ya 70 iliyopita, mkulima aliyekuwa anajishughulisha na kilimo cha mipichi Bw. Jin Xitian aliwaita wakulima wa mipichi washiriki kwenye mkutano wa kutunga mashairi kuhusu maua ya mipichi, ambapo kila mkulima alitunga sentensi moja au ubeti mmoja ili kuonesha matarajio yake kuhusu mavuno mazuri na kusimulia maisha yao ya sehemu ya vijiji. Tokea hapo, kutunga mashairi kukawa jambo zuri zaidi la kujiburudisha kwa wakulima wa mipichi katika nyakati zisizo na kazi nyingi za mashambani.

Ukitaka kufika kwenye kijiji cha mashairi ya Taohua, huna budi kupanda mlima Longquan, kwani kijiji cha Taoyuan kiko kwenye kilele cha mlima huo. Katika majira ya Spring, maua ya mipichi yanachanua kote mlimani na yanapendeza sana. Kwa kuwa kijiji cha Taoyuan kiko kwenye mwinuko mkubwa, hivyo maua ya mipichi yanachelewa kuchanua kuliko sehemu nyingine za chini ya milima, kila mwaka maua ya mipichi yanapokauka na kuanguka chini, maua ya mipichi iliyoko kwenye sehemu ya juu ya mlima huo bado yanakuwa yamechanua vizuri sana, hivyo kijiji hicho cha mlimani kikaitwa kijiji cha Taohuayuan, maana yake ya kichina ni kijiji cha maua mengi ya mipichi.

Kama ukipita kwenye njia nyembamba ya mlimani, utaweza kufika kwenye nyumba nyingi ndogo lakini ni nzuri za wakulima zenye nyua. Ukisimama na kuziangalia kwa makini, utaona kuwa nyumba hizo ni tofauti na nyumba nyingine za kawaida ulizoona, maneno ya mashairi yamechongwa kwenye fremu ya juu ya mlango na kuta za ua wa nyumba, mbali na mashairi maarufu ya washairi wa China na wa nchi za nje, pia kuna mashairi mengi yaliyotungwa na wanakijiji wao wenyewe.

Wanakijiji wa kijiji hicho wanasema, wanapenda sana kutunga mashairi, wawe wazee au watoto. Katika nyakati zisizo na shughuli nyingi za kilimo, huwa wanakutana pamoja kuimba mashairi au kubadilishana uzoefu wa utungaji mashairi. Mashairi wanayotunga ni yenye maneno yanayoeleweka vizuri, yanayohusu uzoefu wa maisha na akili. Endapo utasikia mashairi hayo kwa mara ya kwanza, utaburudika zaidi kutokana na mashairi hayo yaliyotungwa kuhusu hisia za wakulima na maisha ya shambani.

Wanakijiji wanasema, mashairi yao yanapendwa sana na watalii. Hivyo biashara yao inayohusu shughuli za utalii imekuwa nzuri zaidi, hata katika majira ambayo maua ya mipichi yanakuwa yamepukutika, bado kuna watalii wanaokwenda kuwatembelea. Kutokana na mambo ya kiutamaduni ya mashairi, shughuli zao za utalii zinawavutia washairi wengi. Washairi maarufu wa sasa Shu Ting, Mang Ke na Lei Shuyan wote waliwahi kufika huko. Wasomi na washairi mara kwa mara wanajumuika majumbani kwa wakulima, na kijiji pia kinafanya shughuli za kiutamaduni mara kwa mara, wakazi wa sehemu ya Longquan wanasema huu ni "mtindo wa maisha ya maua ya mipichi". Lakini ni kwanini utamaduni wa mashairi unaweza kuota mizizi kwenye sehemu ya Longquan? Mkulima Wei Ping aliyesifiwa na wanakijiji kuwa ni kiongozi wa jumuiya ya wapenda mashairi cha kijiji cha Taohua, alitoa maoni yake akisema,

"Mashairi hayawezi kuota mizizi kwenye kijiji chochote kile, lakini yameweza kuota mizizi kwenye sehemu hiyo, kwani maua ya mipichi yana uhusiano mkubwa sana na utungaji wa mashairi, ambayo pia ni chanzo cha utamaduni nchini China; Pili, sehemu hiyo ni ardhi ya watu wa kabila la wakejia, ambao wana jadi ya kutunga mashairi; tatu, hapa ni karibu sana na mji, na panafaa kwa uendelezaji wa shughuli za utalii, kwa upande mwingine, shughuli za utalii pia zinaharakisha uunganishaji wa mashairi na mazingira ya kijiji."

Hivi sasa kijiji cha Taoyuan kimekuwa na maktaba yake kuhusu mashairi, na kimefungua tovuti ya "Baraza la kijiji cha mashairi ya Taohua cha China" kwenye Internet. Jumuiya ya mashairi ya China imethibitisha jina la sehemu hiyo la "Maskani ya mashairi ya sehemu ya vijiji ya China". Naibu kiongozi wa idara ya uenezi ya serikali ya wilaya ya Longquanyi, Bw. Kuang Li anajitahidi kufanya ushirikiano na idara za uchapishaji ili kuchapisha mashairi ya wakulima washairi. Hivi sasa kitabu cha "Mashairi 300 ya Taohua" kimechapishwa. Bw. Kuang Li alisema, hisia zake kuhusu mashairi haziwezi kutengana na mazingira ya shambani, wakazi wa huko ni sawasawa na yeye, ambao wanafuatilia moyo wa mashairi.

"Wilaya ya Longquanyi ilianza kupanda mipichi kabla ya miaka zaidi ya 2,000 iliyopita, historia hiyo inaafikiana na historia ya kitabu maarufu cha mashairi cha "Shijing", sehemu hiyo ina uhusiano mkubwa na utamaduni wa mipichi. Watu wa sehemu hiyo wanapenda sana kuimba nyimbo za kienyeji zinazoeleza maisha yao; kwa upande mwingine pia wana shauku kuhusu maisha mazuri ya kiroho, yaani moyo wa mashairi."

Dada Lei Jianying mwenye umri wa miaka 26 alikuwa ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha kilimo cha mkoa wa Sichuan, hivi sasa ni mtu aliyejitolea kwenda huko kufanya kazi baada ya kuhitimu masomo yake mwaka 2005. Kwenye kijiji cha mashairi ya Taohua, dada Lei Jianying alivutiwa sana na "mtindo wa maisha ya maua ya mipichi", na pia ameanza kutunga mashairi baada ya kazi, anataka kueleza upendo wake kuhusu ardhi ya sehemu hiyo. Katika shairi alilotunga hivi karibuni liitwalo "Ujana wa kijiji cha mipichi", dada Lei Jianying aliandika: "kama isingekuwa ardhi ya hapa, yeye hajui angeishi wapi; anga ya sehemu nyingine siyo ya kutakata sana kama ya hapo, na ardhi haiwezi kunukia vizuri kama ya hapa?.."

"Kuwa na shamba la mipichi la hekta 300 na kumiliki mashairi yote ya duniani" ni matarajio ya wanakijiji wa kijiji cha mashairi ya Taohua kuhusu mashairi na hisia zao. Maua ya mipichi licha ya kuongeza uzuri wa mazingira ya maumbile, pia yanawapa mwangaza mwingi zaidi katika akili yao. Wapendwa wasikilizaji, mkifika kwenye mazingira hayo, bila shaka mtaburudishwa sana na maua ya mipichi na mashairi yao!

Idhaa ya kiswahili 2008-01-21