Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-22 15:19:48    
Mkoa wa Liaoning waendeleza shughuli mbalimbali ili kuwasaidia wakulima kuongeza mapato

cri

Katika miaka ya hivi karibuni, sehemu mbalimbali za mkoa wa Liaoning ulioko kaskazini mashariki mwa China zilisukuma mbele maendeleo ya uchumi kwa kuendeleza shughuli mbalimbali, na hatua hizo zimesaidia wakulima kuongeza mapato na kuwapatia wakulima fursa nyingi za kujipatia ajira. Hivi sasa serikali za miji mbalimbali ya mkoa huo, zinatafuta njia nyingi na nzuri zaidi ili kuendelea kuwasaidia wakulima kuongeza mapato.

Mwaka 2001 eneo la maendeleo ya uchumi na teknolojia lilianzishwa katika wilaya ya Faku iliyoko kaskazini mwa mkoa wa Liaoning. Katika eneo hilo watu wamepanda mimea ya aina mbalimbali ya biashara kwa mujibu ya hali ya hewa na ardhi ya huko, pia wamewavutia wawekezaji kutoka nje kuanzisha viwanda vya utengenezaji wa mazao ya kilimo na viwanda vya kauri huko. Maendeleo ya uchumi wa wilaya hiyo si kama tu yamewasaidia wakulima kuongeza mapato kwa kiasi kikubwa, bali pia yamebadilisha njia za uzalishaji wa kilimo, na kuongeza njia za kujipatia mapato kwa wakulima wa huko.

Bw. He Lixin ambaye ni mkulima mwenye umri wa miaka 38, alimwambia mwandishi wa habari kuwa, wazazi wake wanajishughulisha na kazi za kilimo, yeye na mkewe wanafanya kazi za vibarua kwenye kiwanda cha kauri, alisema,

"Hivi sasa wilaya yetu inachukua hatua kuvutia wafanyabiashara na uwekezaji, wawekezaji wamekuja hapa, ni rahisi kutafuta kazi ya vibarua, na mapato ni makubwa kuliko kwenye shughuli za kilimo. Nikijishughulisha na kilimo naweza kupata Yuan elfu 5 hadi elfu 6 kwa mwaka, sasa nafanya kazi kiwandani naweza kupata Yuan elfu 2 kwa mwezi."

Katika muda mrefu uliopita, viwanda vikubwa ni sehemu muhimu ya uchumi wa mkoa wa Liaoning. Katika miaka ya hivi karibuni, ili kutimiza maendeleo yenye uwiano ya viwanda na kilimo, serikali ya mkoa huo inahimiza maendeleo ya uchumi kwa njia mbalimbali. Kijiji cha Dalishu cha mji wa Fengcheng ndiyo kimewasaidia wanakijiji kujiendeleza kutokana na uchumi wa umma.

Mazingira ya kimaumbile ya kijiji cha Dalishu si mazuri kutokana na kuwa na milima mingi midogo midogo. Lakini wanakijiji wa kijiji hicho wakiongozwa na katibu wa tawi la kamati ya Chama cha Kikomunisti cha China Bw. Mao Fengmei, wamebadilisha milima midogo midogo kuwa bustani ya miti ya matunda yenye eneo la hekta 1800 kwa mujibu wa hali ya kijiografia ya huko. Kila mwaka watalii wengi wanakwenda huko kutazama maua katika majira ya kichipuko na majira ya joto, na kuvuna matunda katika majira ya kipukutiko. Ili kuongeza mapato kwa shughuli za utalii, kijiji hicho kimejenga hoteli, kituo cha kufanya mikutano, uwanja wa mpira wa kikapu na sinema. Aidha kituo cha kupanda mitishamba ya aina ya schisandra chinensis chenye eneo la hekta mia 7, kiwanda cha mbolea za kemikali, kiwanda cha vipuri vya magari na soko pia vimeanzishwa kwenye kijiji hicho, ambavyo vyote vinawapatia wanakijiji mapato makubwa.

   

Hivi sasa zaidi ya familia 400 za wakulima zinaishi katika nyumba zenye ghorofa, na familia zaidi ya 40 zimenunua magari. Bw. Li Qingzhong ni mmoja kati ya wakulima walionunua magari. Alipozungumzia mabadiliko ya maisha yaliyoletwa na maendeleo ya uchumi wa umma, alisema,

"Katika familia yangu kuna watu sita, mapato ya kila mtu kwa mwaka ni Yuan elfu 20 hadi elfu 30 hivi. Tunajishughulisha na upandaji wa mitishamba ya schisandra chinensis. Familia yangu ina hekta 4 za mashamba, mwanzoni tulipanda mboga na miti ya matunda, baadaye tulianza kupanda mitishamba ya schisandra chinensis. Hivi sasa tumekuwa na mapato makubwa zaidi, tuna magari na nyumba kadhaa zenye ghorofa."

Bibi Guanxin alisema, mkutano wa 17 wa Chama cha Kikomunisti cha China ulitoa sera nyingi za kuwanufaisha wakulima, chini ya uongozi wa makada wa kijiji chake, ana matumaini kubwa kuhusu maisha ya siku zijazo. Alisema

"Kwenye familia yangu kuna watu wanne, mapato ya kila mtu kwa mwaka ni Yuan elfu 20 hivi. Tumenunua malori kadhaa, tunaweza kufanya kazi katika vijiji vingine na kijiji chetu, kila mwaka tunaweza kupata mapato makubwa."

   

Mkuu wa kijiji cha Dalishu Bw. Mao Fengmei anaona kuwa, kuendeleza uchumi wa umma ni njia muhimu ya kuwatajirisha wakulima wa kijiji hicho, alisema,

"Nafikiri kuendeleza uchumi wa umma hasa uchumi wa ngazi ya kijiji ni kazi muhimu zaidi. Sasa tunapata mapato makubwa siku hadi siku. Nina uhakika kuwa siku zetu za mbele zitakuwa nzuri zaidi. Lengo letu ni kuwasaidia wanakijiji kuishi maisha mazuri zaidi kuliko wakazi wa mijini."

Ingawa sehemu mbalimbali za mkoa wa Liaoning zimepata mafanikio kadhaa katika kutafuta njia ya kuendeleza uchumi wa umma na kuwasaidia wakulima kuongeza mapato, lakini msingi wa kilimo na maendeleo ya vijiji mkoani humo bado yako nyuma. Naibu mkurugenzi wa kamati ya kilimo ya mkoa wa Liaoning Bw. Li Zhongguo alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema, katika sehemu ambayo uchumi wa umma umepata maendeleo zaidi, mapato ya watu ni makubwa zaidi, na maisha yao ni mazuri zaidi. Alisema maendeleo ya kilimo ya mkoa huo yameingia kwenye kipindi kipya, kuendelea kuwasaidia wakulima kuongeza mapato na kuendeleza uchumi wa umma vijijini ni suala wanalofikiria, alisema,

"Ni lazima tuongeze nguvu ya kutenga fedha nyingi zaidi kwa ajili ya maendeleo ya vijiji. Kusukuma mbele maendeleo ya vijiji kunahitaji nguvu mbili, kwanza ni nguvu ya nje, pili ni nguvu ya ndani. Nguvu ya nje ni nguvu ya serikali na jamii. Nguvu ya ndani ni nguvu ya wakulima. Tunafikiri njia ya kuendeleza uchumi wa umma vijijini kwa mujibu wa hali halisi ya mkoa wetu na moyo wa mkutano mkuu wa 17 wa Chama cha Kikomunisti cha China."

Mkuu wa kijiji cha Dalishu Bw. Mao Fengmei alisema, katika miaka ya hivi karibuni, serikali imekuwa inatekeleza sera za kuhimiza maendeleo ya kilimo, na imetenga fedha nyingi kwa ajili ya shughuli za kilimo. Mkutano mkuu wa 17 wa Chama cha Kikomunisti cha China ulitoa sera mbalimbali za kuendelea kuunga mkono maendeleo ya vijiji. Yeye na wanakijiji wengine wanafurahi sana, wana matumaini kuwa sera hizo zitatekelezwa kwa makini ili kutatua masuala yanayofuatiliwa zaidi na wakulima, alisema,

"Baada ya mkuu wa 17 wa Chama cha Kikomunisti cha China, sera husika zimetungwa, kazi muhimu zaidi ni kutekeleza sera hizo."