Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-22 15:46:47    
Barua 0120

cri

Msikilizaji wetu Zedekiah Mwita Matiko wa sanduku la posta 73, Isebania Kenya ametuletea barua akitoa ombi la kuwa mwanachama wa idhaa ya Kiswahili wa Radio China Kimataifa. Anasema amekuwa akisikiliza matangazo yetu ya kila siku kupitia Radio ya KBC kwa muda mrefu sasa, kwa hiyo ndiyo maana ameamua kutuandikia barua hii. Anaomba pia tumtumie kadi za salamu na ratiba ya matangazo yetu ya radio na kalenda kama zipo na picha za watangazaji wetu wote wa Radio China Kimataifa tafadhali sana kwa sababu wanasikia tu sauti zetu kwenye radio tu, mfano Fadhili Mpunji. Anasema yeye anaishi nchini Kenya mkoa wa Nyanza wilaya ya Kuria mji mdogo wa Mabera. Mwisho anatupa pongezi sana kwa kazi yetu nzuri sana tunayoifanya kwa kuwaeleza mambo ya dunia na ya China kwa ujumla.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Zedekiah Mwita Matiko kwa barua yake, tunamkaribisha kwa mikono miwili kuwa mwanachama wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu, na kutoa maoni na mapendekezo yake. ujumbe wake umefika, kwa hiyo asiwe na wasiwasi.

Msikilizaji wetu Ali Hamisi Kimani wa Rambira shule ya msingi sanduku la posta 169, Ndori Kenya ametuletea barua akianza kwa salamu za mwaka mpya wa 2008, na ni matumaini yake kuwa hatujambo kwani yeye ni mzima kabisa.

Anasema anaandika barua hii ili kutupongeza kwa kazi yetu nzuri, ingawa kizuri hakikosi dosari. Ama kwa kweli kutokana na majarida ya China pictorial tuliyomtumia mara kwa mara, maktaba yake ya vitabu imeanza kusheheni makala mbalimbali, anashukuru sana kwa hilo. Anashukuru pia kwa picha ya mnyama Panda anayepatikana nchini China katika mkoa wa Sichuan. Aidha angependa kutupongeza kwa kutangaza matokeo ya chemsha bongo kuhusu vivutio vya Mkoa wa Sichuan, maskani ya Panda.

Anasema anapenda kutimia fursa hii kuwapongeza wale wote walioshinda, anafahamu kuwa yeye hataweza kuja China lakini ataendelea kushiriki na kujaribu bahati yake kila mara shindano hili litakapoandaliwa, huku akiwa na matumaini kuwa siku moja atafaulu kupata tuzo bora zaidi kama vile nafasi ya kwanza au nafasi maalum. Anasema kabla hajamaliza barua yake, angependa kulalamika kuwa bado pendekezo lake la kutumiwa majibu sahihi ya chemsha bongo halijatiliwa maanani, anauliza ni kwa nini? Aidha, washindi wa nafasi ya kwanza ni wale wale waliokwishapata nafasi maalum wakati fulani. Kwa nini na wengine wanaoshiriki shindano hili wapo?

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Ali Hamisi Kimani kwa barua yake ya dhati, hapa tunapenda kuwashukuru wasikilizaji wetu wote mnaoshiriki kwa juhudi kwenye mashindano ya chemsha bongo yanayoandaliwa kila mwaka na Radio China Kimataifa. Lakini tunapenda kuwaambia kuwa, kila mara wasikilizaji wetu wengi wanajitahidi sana kujibu maswali vizuri. Wasikilizaji wanaopata nafasi maalum huwa wanachaguliwa na kamati ya uthibitishaji ya Radio China Kimataifa na siyo idhaa yetu, na ushindi hautokani na majibu ya chemsha bongo peke yake, pia yanatokana na sifa yaliyomo kwenye makala wanazotuandikia mara kwa mara. Na wasikilizaji wanaopata nafasi za kwanza, pili, na tatu huwa wanachaguliwa na Idhaa ya Kiswahili ya CRI. Tunasoma kwa makini majibu ya kila mshiriki, kweli wasikilizaji wetu waliowahi kupata nafasi za kwanza, pili na tatu mara kwa mara wanachaguliwa tena kuchukua nafasi ya kwanza, pili na tatu, kwa sababu wasikilizaji hao kweli wanajibu maswali yao vizuri, na kila mara wanaweza kutoa maelezo mazuri, ambayo yanaonesha kuwa wanasikiliza matangazo yetu kwa makini sana, hayo yanastahili kusifiwa. Mkumbuke kwamba, wasikilizaji wetu wote ni marafiki zetu, na wote tunawatendea kwa usawa. Ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu wote watasikiliza kwa makini matangazo yetu. Na kuhusu suala la kuwatumia wasikilizaji wetu majibu sahihi ya mashindano hayo, kwa sasa tunatafuta njia nzuri ya kuwafikishia majibu wasikilizaji wetu wote

Msikilizaji wetu wa Kenya Bw. Osborn Manyengo mwana wa Rosa S.L.P 4343 Kitale-Kenya , akiwa hapo Kenya mjini Kitale, anashukuru sana kwa vipindi vinavyopeperushwa hewani na Radio China Kimataifa, anasema yeye ni shabiki mkubwa sana hapo Kenya wa kipindi cha salamu zenu pamoja na mke wake Eunice Adema Lanya, na Ruth Vihenda, na wanaomba tumtumie Kadi za salamu na kitabu cha maelezo ya Radio China Kimataifa na nchi ya China kwa jumla.

Katika barua pepe tuliyoandikiwa na Bw Telly Wambwa, ameanza kwa salamu kutoka Bungoma, Kenya. Anasema yeye na familia yake ni wazima kabisa licha ya pilikapilika za kisiasa zinazoendelea kuhusu matokeo ya kura za urais mwezi Desemba mwaka 2007 hapo Kenya. Hivi sasa hali ya wasiwasi inapungua, na utulivu umeanza kupatikana polepole.

Bw Wambwa amejibu majibu ya Chemsha Bongo kuhusu "Tukutane Beijing mwaka 2008 kwenye Michezo ya Olimpiki". Ni matumaini yake kuwa mungu atazidi kumsaidia ili apate ushindi na kupata nafasi maalumu ya kutembelea China na Beijing kwenye Michezo ya Olimpiki 2008. Anatushukuru kwa zawadi nzuri iliyomtosha, aliyoipokea kwa furaha tarehe 08 / 01 / 2008. Mke na watoto wake walibubujika na machozi ya furaha na kushukuru sana kwa zawadi hiyo. Anasema ataendelea kutoa maoni katika vipindi vya Radio China Kimataifa atakapopata nafasi. Anasubiri kwa hamu majibu na kututakia wafanyakazi wote wa CRI maisha marefu hapa duniani. Atafurahi kushuhudia Mama Chen na wengine wakifika miaka zaidi ya 100 ili waendelee kuhudumia wasikilizaji wa CRI kutoka nchi tofauti tofauti.

Tunamshukuru sana Bw. Wambwa kwa barua yake ya kutueleza hali ya nchini Kenya. Kweli sisi sote wa hapa Beijing, China tunaona wasiwasi kila siku kuhusu mgogoro wa kisiasa nchini Kenya. Tuna matumaini kuwa, wananchi wa Kenya watapata amani na utulivu mapema iwezekanavyo, ili kutilia mkazo katika kuendeleza uchumi na jamii, kwani mgogoro wa kisiasa nchini Kenya si kama tu umesababisha vifo na majeruhi ya watu, bali pia umeathiri mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya Kenya na nchi majirani zake, ni matumaini ya watu wengi kuwa, hali ya utulivu na usalama itarudi mapema nchini Kenya.

Msikilizaji wetu Paul Mungai Mwangi wa sanduku la posta 69, Injinia North Kinangop, Kenya ametuletea barua akisema, ana matumaini kuwa hatujambo na tunaendelea kuchapa kazi, hana shaka kuwa kazi yetu inaendelea vizuri. Anapenda kutumia fursa hii pia kuwasalimia wasikilizaji wenzake. Anasema pia ana furaha isiyo na kifani kwa kuweza kujishindia nafasi ya tatu katika chemsha bongo iliyokwisha tarehe 15 Aprili, mwaka 2007, aliifurahia nafasi hiyo waliyoipata wakiwa wanane ijapokuwa alikuwa na uhakika wa kushinda katika nafasi maalum ambayo ingemwezesha kualikwa kutembelea mkoa wa Sichuan ulioko kusini magharibi mwa China.

Anasema hata hivyo hajavunjika moyo bali atajitahidi kushinda nafasi maalum kwenye chemsha bongo iliyoanza tarehe 11 Novemba mwaka 2007, ili aweze kualikwa kutembelea Beijing mwaka wa 2008 kujionea michezo ya Olimpiki. Anataka pia kuwapongeza washindi wengine saba wa nafasi ya tatu, huku akiwasalimu.

Na msikilizaji wetu Mchungaji Absalom Tadayo wa kanisa la Safehouse Springs of life sanduku la posta 32 Bungoma Kenya ametuletea barua akisema, angependa kutoa pongezi zake kwa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwa vipindi vyote ambavyo idhaa hii hupeperusha hewani kwa wasikilizaji wake walioko mbali na China. Pia anaipongeza idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwa kuwatumia wasikilizaji kadi za salamu ili wakumbukane kwa salamu.

Na vipindi vya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa vya kuelimisha, wasikilizaji wanavipata kama mwakilishi wa kiroho hapo Kenya, anaithamini Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwani ina uwezo wa kumwunganisha yeye msikilizaji na wachungaji wengine na China ambao hupewa fursa ya kutoa mafunzo katika idhaa hii. Hii itakuwa fursa kwake ya kujifunza mambo mengi kutoka China.

Idhaa ya kiswahili 2008-01-22