Katika siku nne zilizopita, sehemu ya Palestina na Israel imekumbwa tena na hali ya wasiwasi, kwani Israel imeanza kuweka vikwazo kwa pande zote dhidi ya ukanda wa Gaza ili kuwalazimisha watu wenye silaha wa Palestina kuacha kurusha maroketi dhidi ya sehemu ya kusini ya Israel, na wakazi wa huko wamekabiliwa na maisha magumu zaidi.
Kutokana na ukosefu wa nishati uliosababishwa na vikwazo vilivyowekwa kwa pande zote, vituo vya kuzalisha umeme huko Gaza tarehe 20 vilifunga mitambo yote ya kuzalisha umeme, na mji wa Gaza uko katika hali ya giza, vituo vya gesi na maduka ya mikate yalifungwa, na hospitali pia zilikabiliwa na ukosefu wa nishati za kuzalisha umeme, aidha majokofu pia yaliacha kufanya kazi, na kusababisha kupanda kwa haraka kwa bei ya vyakula vya nyama na maziwa.
Hivi sasa watu wengi kati ya wakazi milioni 1.5 kwenye ukanda wa Gaza wanahitaji misaada ya vyakula, lakini kazi ya mashirika ya utoaji wa misaada la Umoja wa Mataifa kwenye sehemu hiyo pia imekwama kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Israel. Msemaji wa Idara ya utoaji wa misaada kwa wakimbizi na mirdi ya Umoja wa Mataifa Bw. Chris Gunness, tarehe 21 Januari alisema kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Israel dhidi ya ukanda wa Gaza, nishati inayotumiwa katika kazi ya uchukuzi na mifuko ya plastiki iliyotumiwa kwa kutoa vyakula ya shirika hilo imekaribia kwisha, endapo hali hiyo itadumishwa, kazi ya utoaji wa misaada ya shirika hilo kwenye sehemu hiyo italazimika kuachwa ifikapo tarehe 24 au 25 Januari.
Matatizo hayo yanayoukabili ukanda wa Gaza yanafuatiliwa na jumuiya ya kimataifa. Kuanzia tarehe 18 Januari, siku ambayo Israel ilianza kuweka vikwazo kwa pande zote dhidi ya ukanda wa Gaza, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon alitoa taarifa akitoa mwito wa dharura wa kulitaka jeshi la Palestina liache mara moja vitendo vya ufyatuaji wa risasi na kuishambulia Israel kwa maroketi, pia alilitaka jeshi la ulinzi wa Israel lijizuie. Tarehe 21 Umoja wa nchi za kiarabu ulitoa taarifa ukilihimiza baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liitishe mkutano ili kuzuia vitendo vya Israel kwenye ukanda za Gaza, na kuihimiza ifungue vituo vilivyoko mipakani, ili kulinda haki za binadamu za wakazi wa huko. Siku hiyo Umoja wa Ulaya pia ulitoa taarifa ukilaani makundi ya Palestina kufanya mashambulizi ya maroketi dhidi ya Israel, na kuzitaka pande hizo mbili zisimamishe vita, pia inaona kuwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Israel vitachochea msukosuko wa kibinadamu kwenye ukanda wa Gaza.
Waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert siku hiyo alisema, hali ya msukosuko wa kibinadamu haitaruhusiwa kutokea Gaza. Lakini pia amesisitiza kuwa wakazi wa Gaza hawataishi vizuri endapo usalama wa wakazi wanaoishi kusini mwa Israel hauwezi kuhakikishwa.
Wachambuzi wamesema, tangu ukanda wa Gaza unaodhibitiwa na kundi la Hamas utangazwe na Israel kuwa "sehemu ya uadui" na kuwekewa vikwazo vya kiuchumi mwezi Septemba mwaka jana, mashambulizi yanayofanywa na watu wenye silaha wa Palestina dhidi ya sehemu ya kusini ya Israel hayajasita. Lakini safari hii kutokana na mashambulizi makali ya kundi la Hamas na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na jeshi la Israel kwenye ukanda wa Gaza, uhusiano dhaifu wa kuaminiana kati ya Palestina na Israel ulioanzishwa kwenye mkutano wa Annapolis umekumbwa na pigo kubwa, makundi yenye siasa kali yameungwa mkono zaidi na wananchi, mustakabali wa amani kati ya Palestina na Israel unakabiliwa na tishio kubwa zaidi. Makubaliano ya amani anayotarajia kufikiwa mwaka huu rais Bush wa Marekani, huenda bado yako mbali na lengo.
|