Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-23 19:55:16    
Suala la nyukilia la Iran lawa na utatanishi zaidi

cri

Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 6 kuhusu suala la nyukilia la Iran, ulimalizika tarehe 22 mwezi Januari huko Berlin. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Bw. Frank Walter Steinmeier, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika baada ya mkutano huo alisema, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi mbalimbali waliohudhuria mkutano wa suala la nyukilia la Iran, siku hiyo waliafikiana kuhusu mambo muhimu yaliyomo kwenye mswada wa azimio jipya la baraza la usalama la umoja wa mataifa. Mkutano huo umezidisha matatizo ya suala la nyukilia wakati mvutano katika suala la nyukilia la Iran ulianza kupungua.

Kutokana na mwaliko wa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 5 za wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani, Russia, China, Uingereza na Ufaransa, pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia mambo ya kidiplomasia na sera za usalama Bw. Javier Solana, walikuwa na mkutano mjini Berlin siku hiyo kuhusu suala la nyukilia la Iran. Baada ya mkutano huo, Bw. Steinmeier akiwa pamoja na mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani, Russia, China na Bw. Solana walishiriki kwa pamoja mkutano na waandishi wa habari, Bw. Steinmeier alisema nchi 3 za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zikiuwakilisha Umoja wa Ulaya, zitawasilisha rasmi mswada wa azimio jipya kuhusu suala la nyukilia la Iran kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, lakini hakudokeza mambo yaliyomo katika mswada huo wa azimio. Lakini mjumbe mmoja wa ujumbe wa Marekani alidokeza kuwa mambo yaliyomo katika mswada huo ni pamoja na kuimarisha nguvu ya kupiga marufuku kusafiri kwa viongozi wa Iran na kuzuia mali za nchi hiyo zilizoko katika nchi za nje, lakini hakuna hatua za kuongeza vikwazo vya kiuchumi. Habari zinasema baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litaujadili mswada huo katika wiki chache zijazo.

Kuhusu suala hilo, waziri wa mambo ya nje wa China, Bw. Yang Jiechi alisema, kuimarisha mfumo wa kutoeneza silaha za nyukilia duniani, kutatua suala la nyukilia la Iran kwa njia ya mazungumzo ya kidiplomasia, na kwa njia ya amani, kunalingana na maslahi ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa. Alisisitiza kuwa pande zinazohusika zinatakiwa kuongeza juhudi ya kidiplomasia na kutumia wazo jipya kutafuta njia ya kutatua suala la nyukilia la Iran kwa muda mrefu, kwa pande zote na hatua mwafaka. Alisema vitendo vya baraza la usalama vinatakiwa kuchangia kutimizwa kwa lengo hilo. Alisema serikali ya China siku zote inafanya juhudi kuhimiza usuluhishi na mazungumzo, na inataka kuendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa. Katika wakati ambao mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Russia bado hawajaeleza misimamo yao, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Bw. Steinmeier alisema mkutano wa siku hiyo ni wa kujenga na wa kupiga hatua. Alisema pande zote zilizoshiriki kwenye mkutano zimeeleza wasiwasi wao kuhusu suala la nyukilia la Iran, zinataka Iran ifanye ushirikiano na jumuiya ya kimataifa, kutekeleza ahadi iliyotoa ya kulieleza wazi Shirika la kimataifa la Nishati ya Atomiki kuhusu "masuala ambayo bado hayajatatuliwa" ili kurudisha hali ya kuaminiana. Alisisitiza kuwa, wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa kuhusu Iran kutaka kuendeleza silaha za nyukilia, bado haujaondelewa, na jumuiya ya kimataifa haina budi kuendelea kufanya juhudi kuepusha matokeo ya msiba.

Mwezi Septemba mwaka jana, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 6 walikuwa na mkutano wa kujadili mambo ya kuweka vikwazo wa azimio la tatu dhidi ya Iran, lakini hazikufikia makubaliano. Hivi sasa hali mpya imetokea kuhusu suala la nyukilia la Iran. Kwanza taarifa iliyotolewa na idara ya upelelezi ya Marekani mwezi Septemba mwaka jana inasema, Iran ilisitisha mpango wa silaha za nyukilia mwaka 2003, taarifa hiyo imepunguza nguvu za uwekaji vikwazo dhidi ya Iran. Pili, Russia imeamua kuipatia Iran nishati ya nyukilia na nchi za kiarabu zinaimarisha uhusiano na Iran, mambo hayo yamepunguza shinikizo la nje dhidi ya Iran.

Mchambuzi anasema katika hali ya namna hiyo, jumuiya ya kimataifa inaona kuna haja ya kuwa na wazo na vitendo vya namna moja kuhusu suala la nyukilia la Iran, huenda hili ni lengo halisi la mkutano huo.