Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-24 19:30:24    
Dada Mahire na kampuni yake ya huduma za nyumbani

cri

Dada Mahire ambaye anatoka kabila la Wakhazak, moja kati ya makabila 55 madogomadogo nchini China, alianzisha kampuni ya kutoa huduma za nyumbani.

Saa 2 na nusu asubuhi Dada Mahire alifika kwenye kampuni yake kwa kutumia baiskeli, na kuanza kufanya maandalizi kwa ajili ya kazi za siku hiyo.

Dada huyo mwenye umri wa miaka 27 ni mkuu wa kampuni ya huduma za nyumbani mjini Yining, katika mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur. Tangu aanzishe kampuni hiyo miaka miwili iliyopita, maisha ya dada huyo Mkhazak yamekuwa yakitawaliwa na shughuli za kampuni hiyo. Kila asubuhi Dada Mahire anafika mapema kwenye kampuni kuandaa mpango wa kazi kwa ajili ya wafanyakazi wake, na jioni baada ya wafanyakazi wenzake kuondoka, anabaki kukagua utekelezaji wa mpango wa kazi wa siku hiyo.

Baadhi ya watu wanaona shughuli anazofanya Dada Mahire hivi sasa ni za kujitaabisha tu, kwani miaka miwili iliyopita dada huyo alikuwa anafanya kazi kwenye idara ya serikali, ambapo alifanya kazi rahisi zaidi na yenye pato la uhakika.

Dada Mahire alisema Ajira ya kwanza niliyopata ni kazi ya kuhifadhi nyaraka katika chama cha wanawake katika maskani yangu. Kazi hiyo inalingana na matarajio ya mama yangu, yeye anapenda nifanye kazi katika mazingira ya uhakika."

Dada Mahire alipata ajira hiyo mwaka 2003mara baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu. Lakini miaka mitatu baadaye aliamua kuacha kazi hiyo ambayo watu wengi walikuwa wanaitaka.

Mahire alielezea ni kwa nini alichukua uamuzi huo, akisema "Baada ya kufanya kazi hiyo kwa miaka mitatu, nilikuwa naona uchovu, bila kuwa na maendeleo makubwa wala uvumbuzi. Sikumwambia mama yangu, nilitoa ripoti kwa bosi wangu na kukabidhi shughuli nilizokuwa nazo, ilichukua muda wa wiki moja na zaidi, na nikaacha kazi hiyo."

Dada Mahire aliona kuwa ajira ya utumishi katika idara ya serikali haimfai, kwani yeye alikuwa anapenda kukabiliana na changamoto mpya. Je, lipi ni jambo linalofaa kwake, kupata ajira yenye pato la uhakika lakini haipendi, au kutumia vizuri ujana wake kufuatilia vitu anavyovutiwa na kukabiliana na changamoto mpya? Baada ya kutafakari kwa makini, dada huyo aliamua kuchagua maisha yenye changamoto. Lakini alifahamu kuwa, kwa vyovyote vile mama yake hatakubaliana na uamuzi wa namna hii, na ilimbidi atekeleze uamuzi wake kwanza bila kumwarifu mama yake.

Dada huyo kutoka kabila la Wakhazak alisema "Wako Wakhazak wachache tu wanaofanya biashara. Hali hii inatokana na utamaduni wa kabila letu. Zamani Wakhazak walikuwa wanaishi mbugani kwa raha mustarehe, na kutokuwa na mtizamo wa ushindani. Kwa hiyo kutokana na mtizamo wa jadi, wazazi hawafurahii kuona watoto wao wanafanya biashara."

Mpaka sasa mama yake bado anamshawishi dada Mahire aache shughuli za biashara. Mahire anamheshimu mama yake, hapingani na mama yake kwa maneno bali anakaa kimya akionesha maoni yake tofauti.

Alisema  "Mama yangu alihuzunika sana. Naelewa hisia zake, simkoseshi raha kwa maneno, ninachoweza ni kutenda shughuli zangu kwa makini."

Baada ya kuacha ajira serikalini, dada Mahire alianzisha biashara yake binafsi ya kunakili. Lakini haikuchukua muda mrefu alikuwa akivutiwa na hatua iliyochukuliwa na serikali ya huko ya kuwasaidia wahitimu wa vyuo vikuu kuanzisha shughuli zao.

Dada Mahire alisema "Katika hali nisiyotarajia, nilifahamishwa kuwa idara ya ajira ilitoa sera ya kuwasaidia wahitimu wa vyuo vikuu, ambapo wakianzisha shughuli zao wanapata unafuu wa kusamehewa nusu ya kodi. Kaka yangu aliniambia kuwa, sera ipo na wewe fikiria unachoweza kufanya. Wazo la kwanza lililonijia ni kuanzisha kampuni ya kutoa huduma za nyumbani. Nilipofanya kazi katika chama cha wanawake niliwahi kushughulikia shughuli hizo, kwa hiyo nilipenda kujiendeleza katika kazi hiyo."

Tukitaja kampuni ya kutoa huduma za nyumbani, watu wanapata taswira ya kusafisha nyumba tu. Na baada ya kuanzishwa kwa kampuni ya dada Mahire, wengine wengi walitoa maoni ya kupinga, wakisema kwa mhitimu wa chuo kikuu kujishughulisha na utoaji wa huduma za nyumbani badala ya kazi nzuri ya utumishi, ni kupoteza umuhimu wa elimu ya chuo kikuu?

Dada Mahire alieleza hali ngumu aliyokumbana nayo akisema"Mzee mmoja mwenye umri wa miaka zaidi ya 50 alinitafuta kwenye kampuni yangu, akiniangalia kwa muda mrefu na kuniuliza, je kwa nini unajishughulisha na kutoa huduma za nyumbani?"

Lakini Mahire anashikilia uamuzi wake. Anaona watu wa makabila ya Wakhazak na Wauygur wanaoishi mkoani Xinjiang wana tabia na mila tofauti, anapenda kutoa huduma za nyumbani kwa mujibu wa matakwa tofauti ya wateja. Alisema "Tunatoa huduma kwa mambo mengi toka kuzaliwa mpaka kufariki kwa mtu. Kwa mfano mtoto wa kabila la Wakhazak anapotimiza mwezi mmoja baada ya kuzaliwa, inafanyika sherehe maalumu, mtoto wa kike akitimiza umri wa miaka 7 kuna sherehe ya kumvalisha hereni, akianza kwenda shuleni tunaweza kutoa huduma za walimu wa nyumbani. Zaidi ya hayo tunatoa huduma za harusi na mazishi. Hayo yote ni sehemu ya huduma za nyumbani."

Je wanatekeleza vipi wazo lake la kutoa huduma za nyumbani za aina mpya na kuwapatia wateja huduma za kiwango cha juu? Tutaendelea na maelezo kuhusu kisa cha Dada Mahire wiki ijayo.

Idhaa ya kiswahili 2008-01-24