Serikali ya Marekani na bunge la nchi hiyo tarehe 24 zilifikia makubaliano kuhusu mpango wa kuhimiza mambo ya uchumi. Kutokana na mpango huo serikali ya Marekani itarudisha kodi yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 100 kwa zaidi ya familia milioni 100 za Marekani, ili kuhamasisha watu kufanya matumizi, na kuzuia uchumi wa Marekani usididimie, kwani uchumi wa nchi hiyo sasa uko katika hali ya kudidimia.
Hivi karibuni watu wengi wamesema uchumi wa Marekani unakabiliwa na hali ya kudidimia, ambapo biashara kwenye soko la hisa la Wall street imeshuka kwa kiasi kikubwa kwa siku kadhaa mfululizo, hali yake imeathiri masoko yote ya hisa kote duniani. Katika hali hiyo, Kamati ya hazina ya Marekani tarehe 22 iliamua kuchukua hatua za kupunguza faida na riba kwa kiasi kikubwa, ili kutuliza soko la fedha, na kuwafanya wawekezaji wawe na imani tena na uchumi wa Marekani. Wakati huo huo, Ikulu na bunge la Marekani pia zilijadili kwa dharura mpango wa kuhimiza uchumi. Baada ya kufanya majadiliano kwa wiki moja, tarehe 24 pande hizo mbili zilifikia makubaliano kuhusu mpango wa kuhimiza uchumi.
Kutokana na mpango huo, serikali ya Marekani itarudisha kodi yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 100 kwa familia milioni 116, ambapo kila mlipa kodi atarudishiwa dola za kimarekani 600, katika familia moja, kama mume na mke wote wana ajira, watarudishwa dola za kimarekani 1200. Aidha, kila familia yenye mtoto mmoja, mtoto huyo atarudishwa dola za kimarekani 300.
Na mtu mwenye mapato ya zaidi ya dola za kimarekani 3000 kwa mwaka ambaye hajafikia kigezo cha kutoa kodi pia atarudishwa dola za Kimarekani 300; na mtu mwenye mapato ya zaidi ya dola za kimarekani 75,000 kwa mwaka, ama mapato ya mume na mke yamefikia zaidi ya dola za kimarekani laki 1.5, kodi watakayorudishwa itapungua kwa kiasi fulani; na mwingine mwenye mapato zaidi ya dola za kimarekani elfu 87 kwa mwaka, ama mapato ya mume na mke yamefikia zaidi ya dola za kimarekani laki 1.74, kodi watakayorudishwa ni baadhi ya sehemu tu.
Mpango huo pia utaruhusu kupunguza asilimia 50 ya ununuzi wa vifaa na zana kwa viwanda na makampuni ya Marekani, na kufuta kodi ya nyongeza za ununuzi wa viwanda vidogo na makampuni madogo. Aidha umeweka hatua mbalimbali za kuvifanya viwanda na makampuni yaliyopatwa na hasara yawe na muda wa kutosha ili kupunguza hasara zao.
Rais Geroge Bush wa Marekani siku hiyo alitoa taarifa akisema, sera na hatua zilizowekwa kwenye mpango huo wa kuhimiza uchumi ni sahihi, na fedha zinazohusika na mpango huo ni mwafaka. Spika wa Baraza la chini la bunge la Marekani Bw. Nancy Pelosi pia alisema, huu ni mpango kabambe unaostahili kusifiwa, ambao utaziwezesha familia zenye mapato ya kati ziwe na pesa nyingi za matumizi, pia utaleta nafasi nyingi za ajira. Waziri wa fedha Bw. Henry Paulson alisema, ataendelea kudumisha ushirikiano na Baraza la juu na la chini kwenye bunge, ili kuuwezesha mpango huo upitishwe mapema iwezekanavyo. Baraza la juu la bunge la Marekani litajadili mpango huo. Kiongozi wa chama chenye wabunge wengi kwenye Baraza la juu Bw. Harry Reid alisema, lengo la Baraza la juu ni kuukabidhi mpango huo kwa Ikulu katikati ya mwezi ujao, ili kumwachia rais Bush asaini na uanze kutekelezwa.
Siku mpango huo wa kuhimiza uchumi ulipofahamika, biashara kwenye soko la hisa la Wall street ilipanda kwa kiasi kikubwa. Wachambuzi wamedhihirisha kuwa, baada ya kamati ya hazina ya Marekani kutangaza kupunguza faida na riba, na mpango huo kutangazwa, yote hayo yatawezekana kuisaidia Marekani kuepusha hali ya kudidimia kwa uchumi wake, na kwa uchache ama kwa muda, yatapunguza wasiwasi wa watu kuhusu kudidimia kwa uchumi wa Marekani.
Lakini vyombo fulani vya habari vya Marekani pia vimesema, mpango huo hautaweza kuleta msaada halisi, kwani sera ya kurudisha kodi haitaweza kuvumbua nguvu halisi ya matumizi. Wataalamu kadhaa wa elimu ya uchumi pia wamedhihirisha kuwa, ingawa viongozi wa bunge la Marekani wameahidi kuchukua hatua haraka iwezekanavyo, lakini watu hawataweza kurudishwa kodi mapema. Hivyo mpango huo utahimiza namna gani uchumi wa Marekani mwaka huu, bado unatakiwa kufuatiliwa.
|