Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-28 18:52:48    
Ushirikiano wa nchi mbalimbali waleta mustakabali mzuri duniani

cri

Mkutano wa mwaka 2008 wa Baraza la uchumi la dunia ulifungwa tarehe 27 huko Davos, nchini Uswisi. Masuala yaliyozungumzwa sana kwenye mkutano huo wa siku 5 yalikuwa ni pamoja na uchumi wa dunia, maendeleo endelevu na mazungumzo ya raundi ya Doha. Na wanasiasa na watu mashuhuri wa mambo ya kiuchumi na kiutamaduni kutoka nchi mbalimbali walikuwa wakifikia maoni ya pamoja kuwa, ushirikiano ni msingi wa kuleta mustakabali mzuri wa dunia hii.

Watu waliohudhuria mkutano huo walikubaliana kuwa, mwaka huu kasi ya ongezeko la uchumi wa dunia itapungua kwa kiasi, lakini hali haitakuwa mbaya sana, huku China, India pamoja na nchi na sehemu nyingine zenye ustawi wa kiuchumi katika miaka ya hivi karibuni zitadumisha mwelekeo wa maendeleo ya kasi ya uchumi. Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Bw. Tony Blair akihutubia ufungaji wa mkutano huo alisema, kutokana na kuenea kwa utandawazi wa uchumi duniani nchi mbalimbali zina uhusiano wa karibu zaidi, kwa hiyo hazina chaguo lingine bali kufanya ushirikiano.

Mwaka huu kupungua kwa thamani ya soko la hisa la Marekani kulisababisha kuyumbayumba kwa masoko ya hisa duniani. Ndiyo maana uchumi wa Marekani ulikuwa moja ya masuala yaliyozungumzwa sana kwenye mkutano huo wa baraza la uchumi la dunia. Watu waliohudhuria mkutano huo walikuwa na maoni ya pamoja kuwa, kasi ya ongezeko la uchumi wa Marekani itapungua, ingawa bado wana maoni tofauti kuhusu uchumi wa Marekani utadidimia au la.

Kutokana na utandawazi wa uchumi duniani, haiwezekani kwa nchi yoyote kuwepo kuathiriwa na hali ya dunia nzima, kwa hiyo kufanya ushirikiano ni njia pekee ya kulinda maslahi ya nchi moja moja. Naibu waziri mkuu wa China Bw. Zeng Peiyan akihutubia mkutano huo alisema, hivi karibuni maendeleo ya uchumi wa dunia yanakabiliwa na kuongezeka kwa hali isiyo na uhakika, kwa mfano athari ya msukosuko wa mkopo wa makazi wa Marekani inavyozidi, kupanda kwa bei ya mali ghafi na kufufuka kwa sera ya kujilinda kibiashara. Ili kukabiliana na changamoto hizo, China inapenda kushirikiana bega kwa bega na jumuiya ya kimataifa, kujitahidi kutafuta ufumbuzi wa masuala na kutoa mchango ili kudumisha utulivu wa uchumi na maendeleo endelevu ya dunia.

Mbali na kufanya makadirio ya uchumi wa dunia, maendeleo endelevu ni suala lingine muhimu lililojadiliwa kwenye mkutano huo. Kwa mfano vikao karibu 30 vilifanyika kuhusu suala la mazingira, idadi ambayo ni ongezeko la asilimia 70 kuliko mwaka jana. Katika vikao zaidi ya 200 vilivyofanyika katika siku 5 zilizopita, kikao cha kujadili hatua za kufikisha malengo ya milenia kilichofanyika tarehe 25 kiliwavutia watu zaidi. Kikao hicho kiliwashirikisha wawakilishi wa pande mbalimbali, wakiwemo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-Moon, mwakilishi wa nchi zinazoendelea ambaye ni rais Umaru Yar'adua wa Nigeria, mwakilishi wa nchi zilizoendelea ambaye ni waziri mkuu wa Uingereza Bw. Gordon Brown, pamoja na wawakilishi wa wafanyabiashara na mashirika yasiyo ya kiserikali. Taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya kumalizika kwa kikao hicho inatoa wito wa kusaidia nchi maskini kabisa na watu wao kwa vitendo halisi, ili mwaka 2008 juhudi za kuondokana na umaskini zipate maendeleo makubwa. Hivi sasa nchi maskini na nchi tajiri zote zinakabiliwa na shinikizo kubwa katika suala la kuondokana na umaskini, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ni njia pekee ya kuleta ustawi wa pamoja, la sivyo walimwengu wote watakumbwa na hasara. Ndiyo maana, Bw. Ban Ki-Moon alisema, Umoja wa Mataifa unapaswa kujitokeza ili kufanya uratibu na kushirikisha nchi mbalimbali na nguvu katika maeneo mbalimbali.