Tarehe 28 Rais Pervez Musharraf wa Pakistan alimaliza ziara yake ya siku nane barani Ulaya. Vyombo vya habari vinaona kuwa lengo kuu la ziara ya rais huyo barani humo ni kuboresha sura ya Pakistan duniani, na kuondoa kutoelewana na kutafuta imani na uungaji mkono kutoka kwa nchi za Ulaya. Lakini kwa kuzingatia matokeo ya ziara yake, rais Pervez Musharraf amefanikiwa kwa kiasi fulani.
Rais Perbvez Musharraf kwa nyakati tofauti alifanya ziara nchini Ubelgiji, Ufaransa, Uswisi na Uingereza, na alihudhuria mkutano wa kiuchumi wa kila mwaka uliofanyika mji wa Davos. Kabla ya ziara yake, nchi za Ulaya zilikuwa na wasiwasi kuhusu uchaguzi mkuu wa Palestina, mapambano dhidi ya ugaidi na suala la usalama wa nyuklia, na ziliishutumu mara kwa mara na kusababisha shinikizo kubwa kwa serikali ya Pakistan.
Pamoja na shughuli za kuboresha sura ya Pakistan barani Ulaya, nchini Pakistan pia vilifanywa vitendo vingi kusaidia shughuli hizo. Kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya Pakistan, hivi karibuni jeshi la usalama limeimarisha operasheni kwenye sehemu ya Waziristan Kusini, kaskazini maghaaribi mwa Pakistan, na kwa makusudi iliwaeleza wanadiplomasia na waandishi wa habari wa nchi za nje kuhusu hatua za serikali ya Pakistan kudhibiti rasilmali zake za nyuklia. Kuhusu uchaguzi mkuu viongozi wakuu wa Pakistan kwa mara nyingi na mahali tofauti walieleza kwamba Pakistan itahakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa haki na usawa.
Mawasiliano kati ya Rais Pervez Musharraf pamoja na viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wa NATO, kwa kiasi fulani yamesaidia kuondoa kutoelewana kati ya ya nchi za Ulaya na Pakistan. Rais wa Ufaransa alisema nchi yake itaendelea kuiunga mkono Pakistan kwa nguvu zote katika mapambano dhidi ya ugaidi, na kusema utulivu na umoja wa kikabila nchini Pakistan unalingana na maslahi ya kimataifa. Waziri mkuu wa Uingereza alipozungumza na Rais Pervez Musharraf aliahidi kwamba atashirikisha viongozi wa nchi nyingine kuiunga mkono zaidi Pakistan katika mambo ya siasa na uchumi na kuisaidia nchi hiyo kupambana zaidi na ugaidi na siasa kali.
Lakini vyombo vya habari pia vinasema, kutokana na kuwa nchi za Ulaya haziiamini Pakistan vya kutosha, lengo la ziara ya Rais Pervez Musharraf halijafanikiwa kikamilifu. Maneno aliyosema mwakilishi mwandamizi anayeshughulikia mambo ya nje na sera za usalama katika Umoja wa Ulaya Bw. Javier Solana yalimkatisha tamaa Bw. Musharraf, akisema ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Pakistan utaamuliwa na hali ya uchaguzi mkuu wa Pakistan. Na Bw. Musharraf hakuweza kuhutubia kamati ya mambo ya nje ya Umoja wa Ulaya na bodi ya wakurugenzi ya NATO.
Vyombo vya habari vya Pakistan vilifuatilia sana ziara ya Bw. Musharraf barani Ulaya. Vinaona kuwa nchi za Ulaya zinatambua nafasi muhimu ya Pakistan katika mapambano dhidi ya ugaidi duniani na hasa nafasi yake katika kutuliza hali ya Afghanistan, kwa hiyo Bw. Musharraf amekaribishwa bila kupuuzwa. Lakini nchi hizo za Ulaya zinaiunga mkono Pakistan kwa masharti, na sharti la kwanza ni kuwa ni lazima Pakistan ihakikishe uchaguzi mkuu unafanyika kwa uhuru, uwazi na haki. Na zaidi ya hayo tofauti na Marekani, nchi za Umoja wa Ulaya zinapendelea kuondoa nguvu za siasa kali kupitia kustawisha uchumi badala ya nguvu za kijeshi.
Idhaa ya kiswahili 2008-01-29
|