Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-29 16:37:01    
Mahojiano na meneja mkuu wa tawi la kampuni ya zana za umeme nyumbani ya Bosch na Siemens nchini China

cri

Kampuni ya zana za umeme za nyumbani ya Bosch na Siemens ni kampuni maarufu inayotengeneza zana hizo duniani. Thamani ya uuzaji wa bidhaa ya kampuni hiyo inachukua nafasi ya kwanza barani Ulaya na inachukua nafasi ya tatu duniani. Mwaka 1994 kampuni hiyo ilifungua tawi lake nchini China, na baadaye ikaanza kupata maendeleo yenye utulivu. Kwenye makao makuu ya tawi lake nchini China yaliyoko mjini Nanjing, meneja mkuu wa tawi hilo Bw. Gerke Roland alimwelezea mwandishi wetu wa habari maendeleo ya kampuni hiyo nchini China. Kampuni hiyo ilimkaribisha mwandishi wetu wa habari, Bw. Gerke alimsalimia kwa kichina, akisema,

"Ninafurahi kukuelezea habari zinazohusu kampuni yetu, bidhaa zetu na chapa zetu."

Mwaka 2002, Bw. Gerke aliteuliwa kuwa meneja mkuu wa tawi la kampuni ya zana za umeme nyumbani ya Bosch na Siemens nchini China. Lakini alivutiwa na China hata kabla ya kampuni hiyo hazijafungua tawi lake nchini China. Alipokuwa meneja mkuu wa kwanza wa mauzo wa kampuni hiyo hapa China, alikuwa anashughulikia mauzo ya bidhaa kwenye soko la China kwa miaka mitano, na alifanikiwa kuanzisha utaratibu kamili wa mauzo hapa nchini. Bw. Gerke alisema alipokuja China kwa mara ya kwanza, aligundua kuwa aina za majokofu na mashine za kufulia nguo zilizokuwa zinatumiwa na Wachina zilikuwa chache na za zamani, na akaona kuwa soko la China itakuwa ni kubwa. Baadaye kampuni hiyo ilianza kuuza bidhaa zake kwenye soko la China. Bw. Gerke alisema maendeleo ya uchumi wa China yameongeza mapato ya wananchi, kuongezeka kwa uwezo wa kununua zana za umeme zinazotumiwa nyumbani ni sababu kubwa iliyochangia maendeleo ya shughuli za kampuni hiyo nchini China, alisema,

"Maendeleo ya shughuli zetu nchini China ni muhimu kwa kampuni yetu. Tunafurahi kuona kuwa shughuli zetu zinapata maendeleo mwaka hadi mwaka. Tunaamini kuwa kutokana na maendeleo ya uchumi wa China, shughuli zetu zitapata maendeleo zaidi."

Mpaka sasa, Kampuni ya zana za umeme zinazotumiwa nyumbani ya Bosch na Siemens imeanzisha viwanda vitatu na kampuni moja inayoshughulikia uuzaji wa bidhaa. Kampuni hiyo imekuwa na wafanyakazi zaidi ya elfu 7, utaratibu wa mauzo wa kampuni hiyo umeenea kwenye zaidi ya miji 600 nchini China. Ni wazi kuwa kampuni hiyo imechukua nafasi kubwa kwenye soko la China.

Kampuni hiyo ina mikakati tofauti ya maendeleo na makampuni mengine ya nje. Kama umewahi kuja China, unaweza kupata picha kuwa mijini Beijing na Shanghai kuna majengo mengi ya makao makuu ya makampuni ya kimataifa, lakini kampuni ya zana za umeme nyumbani ya Bosch na Siemens ilianzisha makao makuu ya tawi lake nchini China mjini Nanjing. Bw. Gerke anaeleza sababu ya Kampuni yake kuuchagua mji wa Nanjing, akisema,

"Tulichagua kuanzisha makao makuu ya tawi la kampuni yetu mjini Nanjing, kwa sababu huu ni mji muhimu katika sehemu ya kati ya China. Tena mji huu una historia ndefu. Jambo muhimu zaidi ni kuwa mji huu ni kituo cha elimu, ambao una vyuo vikuu vingi na nguvu kazi nyingi. Pia tunazishukuru serikali za mkoa wa Jiangsu na mji wa Nanjing, ambazo zilitusadia kupata mafaniko wakati tulipoingia mjini Wuxi mwaka 1994 na tulipokuja hapa Nanjing mwaka 1997."

Kampuni ya Bosch na Siemens ilinufaika na kuwepo kwa nguvu kazi nyingi mjini Nanjing. Bw. Gerke alisema kampuni hiyo imetunga mpango kamili wa kuwaandaa wafanyakazi, na kuchagua wanafunzi hodari kutoka vyuo vikuu na shule za mafunzo ya kazi za huko, alisema,

"Tunashirikiana na vyuo vikuu vingi, kwa mfano tunawapatia wanafunzi wa chuo kikuu cha Dongnan fursa ya kufanya mazoezi katika kampuni yetu, na tunawapatia wanafunzi wa shahada ya kwanza na shahada ya pili nafasi za ajira. Aidha tunashirikiana na shule ya mafunzo ya ufundi wa kazi ya Nanjing ili kuandaa mafundi. Baada ya kupata mafunzo watakuja kufanya kazi katika kampuni yetu, na kama wana uwezo wa kufanya kazi katika nchi za nje, huenda watatumwa kufanya kazi katika matawi mengine ya kampuni yetu duniani."

Bw. Gerke anaona kuwa kuwaandaa wafanyakazi ni jambo muhimu sana kwa maendeleo ya kampuni. Katika makao makuu ya tawi la kampuni hiyo, kila mfanyakazi ana fursa ya kupata mafunzo nchini Ujerumani. Na kampuni hiyo inatilia maanani kuwasaidia wafanyakazi wawe na moyo wa kushirikiana. Bi. Zhang Ling ambaye alijiunga na kampuni hiyo mwaka 2007 alisema, akiwa mfanyakazi mpya, anapenda sana mazingira kwenye kampuni hiyo, kila mfanyakazi anaweza kupata maendeleo hatua kwa hatua, jambo ambalo ni muhimu sana kwake, alisema,

"Nafikiri kampuni yetu ni nzuri, kila mfanyakazi ana cheo chake, na anajua vizuri njia ya maendeleo. Mkuu na wenzangu wanapenda kunisaidia, ninaweza kujifunza mambo mengi, nafikiri mambo hayo yatanisaidia kujiendeleza."

Hivi sasa chapa za Siemens na Bosch za kampuni hiyo zinatambuliwa na wateja wa China. Ili kuwapatia wateja huduma kamili baada ya mauzo, kampuni hiyo inatunza njia ya mawasiliano ya kila mteja. Mwandishi wetu alimtembelea Bw. Shen Kuang ambaye ni mteja mmoja wa kampuni hiyo. Nyumbani kwake kuna mashine ya kufulia nguo ya chapa ya Siemens. Bw. Shen alisema,

"Nimetumia mashine hii kwa miaka 10, na bado inafanya kazi vizuri. Ninafua nguo nyingi na vitu vingine vikubwa vikiwemo mashati kwa mashine hii. Inaweza kukidhi mahitaji yangu. Pia ninafua viatu vya michezo kwa mashine hii, na inaweza kufua viatu na vikawa safi."

Kutokana na kampuni hiyo kuwa na teknolojia za kiwango cha juu, imani ya wateja, na uwezo mkubwa wa kupata maendeleo kwenye soko la China, Bw. Gerke ana matumaini kuhusu mustakabali wa kampuni hiyo, alisema,

"Kwanza tutaendelea kukidhi mahitaji ya wateja kwa teknolojia za kisasa na huduma kamili. Pili tutashikilia kuendeleza shughuli zetu nchini China kwa muda mrefu. Hivi sasa tumeanzisha viwanda vitatu nchini China, ambavyo pia ni njia muhimu ya kushirikiana na serikali ya China. Tatu tuna wenzi na wafanyabiashara wazuri wa kushirikiana, kuhakikisha ushirikiano wa kunufaishana nao ni jambo muhimu sana."