Kutokana na usuluhishi wa katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan, mazungumzo kati ya chama tawala kinachoongozwa na rais Mwai Kibaki wa Kenya PNU, na chama cha upinzani cha ODM kinachoongozwa na Bw. Raila Odinga yalianza rasmi tarehe 29 alasiri huko Nairobi. Pande hizo mbili zilieleza nia ya kuendelea na mazungumzo hayo, na kutoa wito kwa Wakenya watulie na kuepusha machafuko.
Katika mazungumzo hayo Bw. Odinga alitoa wito kwa Wakenya waache matumizi ya nguvu, akisema viongozi wa pande mbalimbali za kisiasa za Kenya wamekubaliana kushirikiana katika utatuzi wa mgogoro. Bw. Odinga alisema (sauti 1) "Kama nilivyosema mara nyingi kuwa, hata kama tuna sababu ya kukasirika, kamwe hatuwezi kutumia nguvu kuonesha hasira zetu. Matumizi ya nguvu yanaleta tu marudio ya matumizi ya nguvu, hali ambayo tulikuwa tumeshuhudia katika mwezi uliopita. Leo tunapaswa kuwaambia wananchi wetu, viongozi wenu wana nia ya kufanya ushirikiano kutatua masuala yote makubwa yanayoikabili nchi hii."
Rais Kibaki alilaani matumizi ya nguvu na kusisitiza kuwa anajitahidi kufikia maelewano ya taifa. Alisema (sauti 2) "ninalaani vikali vurugu zilizotokea katika baadhi ya sehemu za nchi yetu. Kama nilivyoahidi hapo awali, nitafanya kila niwezalo kufikia maelewano ya taifa. Sisi wakenya tunapaswa kufahamu kuwa, vurugu si mbadala wa mazungumzo, na sisi viongozi tuna wajibu wa kuenzi amani."
Baada ya vurugu mbaya zilizodumu kwa mwezi mmoja, ambapo watu 800 walipoteza maisha na wengine zaidi ya laki 2.5 kukimbia makazi yao, sasa mwangaza wa amani umeanza kujitokeza nchini Kenya. Katika mazungumzo hayo yaliyoanza tarehe 29, pande mbili zitajadiliana mapendekezo yaliyotolewa na Bw. Annan, yakiwemo jinsi ya kukomesha machafuko, namna ya kuondoa maoni tofauti kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu, na jinsi ya kuwafanya wakenya wote wanufaike na maliasili za nchi hiyo.
Baada ya mazungumzo ya tarehe 29, Bw Kibai na Bw Odinga walijitokeza wakiwa na tabasamu, kushikana mikono na kuongea kama walivyofanya siku 5 zilizopita, lakini tofauti kati yao bado hazijapatiwa ufumbuzi. Bw. Odinga alisema mazungumzo hayo si kati ya ODM na serikali bali ni kati ya vyama viwili vya ODM na PNU. Maana yake ni kuwa anakataa kumtambua rais Kibaki na serikali yake.
Hivi sasa vyama hivyo viwili vimewateua wawakilishi watatu kutoka kila upande wakishiriki kwenye mazungumzo, na Bw. Annan alitangaza muda wa kutatua mgogoro wa Kenya. Alisema (sauti 4) "Kwanza tunapaswa kutatua masuala yanayopaswa kutatuliwa kwa hivi sasa na kuchukua hatua za lazima, baadaye tutapata ufumbuzi wa kimsingi wa masuala. Tuna imani kuwa, masuala ya kimsingi yaliyosababisha mgogoro wa uchaguzi mkuu yataweza kutatuliwa ndani ya mwaka mmoja, na mgogoro wa kisiasa uliopo sasa utaondolewa ndani ya wiki nne, hata katika muda mfupi zaidi."
Siku hiyo hiyo wakati makundi mawili makubwa ya kisiasa nchini Kenya yakianza kufanya mazungumzo na kutoa wito wa kumaliza vurugu, matukio ya umwagaji damu yaliyosababishwa na mapambano ya kikabila yalikuwa yanaendelea huko mkoa wa Magharibi na mkoa wa Rift Valley nchini humo. Kwa mujibu wa polisi ya Kenya, kuanzia usiku wa tarehe 28 hadi tarehe 29, watu 11 waliuawa katika ghasia mkoani Magharibi, huku watu wasiopungua 80 walipoteza maisha katika mapambano ya kikabila yaliyotokea katika siku 3 za hivi karibuni huko Nakuru, mkoani Rift Valley. Dalili zote zinaonesha kuwa, itachukua muda kabla ya kuondolewa kwa mgogoro wa kisiasa nchini Kenya.
|