Tarehe 30 Januari mkutano wa kujadili usalama wa nishati na mabadiliko ya hali ya hewa uliohudhuriwa na nchi na makundi makubwa ya kiuchumi ulifanyika huko Hawaii. Hii ni mara ya pili kwa Marekani kuitisha mkutano wa namna hii, ambapo wajumbe kutoka nchi 16, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa walihudhuria mkutano huo.
Mwenyekiti wa kamati ya sifa ya mazingira ya ikulu ya Marekani Bw. James Connaughton alisema, lengo la mkutano huo ni kuhimiza mchakato wa mazungumzo ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, kutekeleza na kujadili zaidi masuala kadhaa nyeti yaliyomo kwenye mpango uliopitishwa mwezi Desemba mwaka jana kwenye mkutano wa Bali ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa, ili mazungumzo kuhusu hatua mpya za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa yaweze kumalizika kabla ya mwishoni mwa mwaka 2009. Mada kuu ya mkutano huo wa Hawaii ni pamoja na jinsi ya kuweka malengo ya muda mrefu ya dunia na malengo ya muda wa kati ya nchi moja moja kuhusu kupunguza utoaji wa hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto, na malengo hayo yawe yanalingana na malengo ya maendeleo ya uchumi; jinsi ya kuzishawishi nchi kubwa zikubali kuchukua hatua za kupunguza utoaji wa hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto, na kupima ufanisi wa hatua hizo, kutoa ripoti husika na kufanyia ukaguzi hatua hizo; na jinsi ya kutunga mkakati wa ushirikiano na uenezi wa teknolojia husika. Mbali na hayo kusaidia nchi zinazoendelea katika matumizi ya nishati safi vilevile ni suala muhimu linalozungumzwa kwenye mkutano huo.
Katika maandalizi ya mkutano huo, serikali ya Marekani hivi karibuni ilitangaza kuwa, itatoa dola za kimarekani bilioni 2 katika miaka mitatu ijayo ili kuzisaidia nchi zinazoendelea kununua teknolojia za nishati safi. Ingawa Marekani imekuwa ikipiga hatua katika kukabiliana na suala la kuongezeka kwa joto duniani, wachambuzi bado wana shauku ya kujua kama maendeleo yanaweza kupatikana kwenye mkutano huo au la. Kwani katika suala la kupunguza utoaji wa hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto duniani, tangu mwanzo serikali ya Bush imekuwa ikikaidi kusaini makubaliano ya Kyoto, sababu yake ni kuwa makubaliano hayo hayakuhusisha wajibu wa nchi zinazoendelea katika kupunguza utoaji wa hewa za joto, hatua ambayo Marekani inaona si ya haki, na itasababisha kuongezeka kwa idadi ya watu wasio na ajira nchini Marekani. Zaidi ya hayo Marekani inataka nchi zinazotoa uchafuzi kwa wingi kubeba wajibu huo kwa pamoja, ikisema nchi mbalimbali zinapaswa kuchukua hatua na kutunga malengo ya kupunguza utoaji wa hewa joto kwa hiari.
Wanaharakati wa kuhifadhi mazingira wa Marekani wanasema, ni vizuri kwa serikali ya Bush kuitisha mkutano wa kujadili usalama wa nishati na mabadiliko ya hali ya hewa, lakini bado haijabadili msimamo wake uliokuwepo tangu mwanzo. Lengo la kuitisha mkutano huo ni kuzishawishi nchi nyingine zikubali msimamo huo wa Marekani, na wanataka Marekani itoe sera na hatua halisi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani badala ya kurudia malengo yake ya muda mrefu.
Wachambuzi wanaona kwa vyovyote vile mkutano huo una manufaa katika kutatua suala la kuongezeka kwa joto duniani, kwani unashirikisha nchi zinazotoa kwa wingi hewa inayosababisha kuongezeka kwa joto duniani. Zaidi ya hayo shinikizo kutoka nchini na nje ya Marekani zitaifanya serikali ya Bush ishughulikie kwa makini suala la kuongezeka kwa joto duniani. Muda wa utekelezaji wa makubaliano ya Kyoto utamaliza mwaka 2012. Katika mkutano huo wa Hawaii nchi mbalimbali zinaweza kujadiliana makubaliano mapya na huenda kufikia maoni ya pamoja katika masuala kadhaa, likiwemo kuzipa nchi zinazoendelea msaada wa kukabiliana na kuongezeka kwa joto duniani.
|