Mkutano wa 10 wa viongozi wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika ulifunguliwa tarehe 31 Januari mjini Addis Ababa, mada ya mkutano huo ni "Maendeleo ya viwanda barani Afrika", viongozi au wajumbe kutoka nchi 53 za Umoja wa Afrika watajadiliana kuhusu maendeleo ya viwanda barani humo, uchaguzi wa mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika, msukosuko wa kisiasa nchini Kenya na kuunda serikali ya muungano wa nchi za Afrika.
Tarehe 27 Desemba mwaka jana Kenya ilifanya uchaguzi mkuu, baada ya siku tatu tume ya uchaguzi ilimtangaza Rais Kibaki kuwa mshindi wa uchaguzi huo, lakini chama cha upinzani ODM kililaani kuwa udanganyifu ulifanyika katika hesabu ya kura na kukataa matokeo ya uchaguzi huo. Baadaye matokeo ya uchaguzi huo yaliyopingwa na chama hicho yalizusha vurugu kubwa kote nchini Kenya, hadi sasa vurugu bado zinaendelea, hali hiyo nchini Kenya imekuwa ajenda muhimu katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika Bw. Alpha Oumar Konare kwenye ufunguzi wa mkutano huo alitaka pande zote nchini Kenya zichukue hatua za kutuliza ghasia na kutafuta ufumbuzi. Alisema Rais Mwai Kibaki na kiongozi wa chama cha ODM, Bw. Raila Odinga wana "majukumu maalum" ya kutatua msukosuko wa kisiasa nchini Kenya. Alisisitiza kuwa jumuyia ya kimataifa inapaswa kuisaidia Kenya ili kuwapunguzia msiba kwa watu wa Kenya. Kisha katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon alitangaza kuwa siku hiyo atakutana na Bw. Mwai Kibaki mjini Addis Ababa, na siku ya pili yaani tarehe mosi Februari atafanya ziara nchini Kenya.
Wakati Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa vinapotaka pande mbili zimalize mgogoro wa mauaji, mbunge mmoja wa chama cha upinzani aliuawa katika mji wa Eldoret, magharibi mwa Kenya. Kutokana na tukio hilo mazungumzo yaliyopangwa kufanyika siku hiyo kati ya serikali na chama cha upinzani yaliahirishwa.
Msukosuko wa kisiasa nchini Kenya umesababisha athari mbaya kwa uchumi wa Kenya na Afrika ya Mashariki. Kenya ni kituo cha uchumi na mawasiliano kwa Afrika ya Mashariki, na ni nchi kubwa ya kibiashara kwa nchi jirani zake, msukosuko wa kisiasa wa Kenya sio tu umeathiri vibaya uchumi wa nchini pia umesababisha athari mbaya mfululizo kwa uchumi wa nchi zote za Afrika ya Mashariki, thamani ya biashara kati ya nchi za Afrika ya Mashariki na Kenya imepungua kwa kiasi kikubwa na mapato ya ushuru wa forodha pia yamepungua.
Bw. Kofi Annan aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa na "kikundi cha watu mashuhuri wa Afrika" alijitahidi kufanya usuluhishi, tarehe 24 Januari kwa mara ya kwanza Bw. Mwai Kibaki na Bw. Raila Odinga walifanya mazungumzo ya ana kwa ana. Siku tano baadaye pia kutokana na usuluhishi wa Bw. Kofi Annan, pande mbili zilifanya mazungumzo rasmi. Hivi sasa mazungumzo ya pande hizo yameingia kwenye kipindi cha masuala ya kimsingi, na kwa mujibu wa matakwa ya Bw. Kofi Annan pande hizo zitatoa ratiba na kujadiliana hatua za dharura na kutafuta ufumbuzi wa kimsingi wa msukosuko huo. Bw. Alpha Oumar Konare kwenye ufunguzi alisisitiza kuwa, Umoja wa Afrika unaunga mkono juhudi za Bw. Kofi Anna katika usuluhishi na anatumai usuluhishi huo utapata mafanikio.
Kwenye mkutano huo wa siku tatu, juhudi za kutatua suala la Kenya zinazofanywa na Umoja wa Afrika zitafuatiliwa sana kuona kama mafanikio kiasi gani yatapatikana.
Idhaa ya kiswahili 2008-02-01
|