Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-04 15:36:30    
Hatma ya Chad itakuwaje?

cri

Tarehe 3 mapambano makali kati ya jeshi la serikali na vikosi vya upinzani yaliendelea huko N'Djamena, mji mkuu wa Chad, na huku vikosi vingine vikifanya mashambulizi dhidi ya jeshi la serikali kwenye sehemu ya mpaka wa mashariki wa nchi hiyo. Mpaka sasa haijulikani mapambano hayo yataendelea vipi.

Tokea mwaka 1960 Chad ilipopata uhuru, hali ya kisiasa nchini Chad haijawahi kuwa tulivu, Bw. Idriss Deby aliyekuwa mkuu wa jeshi alifanya uasi na kuipindua serikali ya Bw. Habre, mwezi Machi mwaka uliofuata alijitangaza kuwa rais wa Chad. Tokea hapo amekuwa rais wa nchi hiyo kwa vipidi vitatu mfululizo katika mwaka 1996, 2001 na mwaka 2006. Baada ya Idriss Deby kushika madaraka, kwa upande mmoja alikuwa anasaka vikosi vya upinzani, na kwa upande mwingine alifanya mazungumzo ya upatanishi na vikosi vya upinzani ili kuimarisha utawala wake. Hadi kufikia mwaka 2003 vikosi vya upinzani vilikuwa kimya. Lakini mwaka 2005 msukosuko ulianza kutokea. Mwezi Oktoba mwaka huo baadhi ya askari na maofisa wa kikosi cha ulinzi wa rais walifanya uasi wakijaribu kuipindua serikali ya Bw. Deby, lakini walishindwa na walikimbilia kwenye sehemu ya mpaka wa mashariki na kuunda vikosi vya upinzani na mara kwa mara walikuwa wanapambana na jeshi la serikali. Mwezi Aprili mwaka 2006 vikosi hivyo vilianza mashambulizi dhidi ya serikali na kudai kuwa vimekamata 80% ya ardhi ya nchi hiyo na vilikuwa karibu na mji N'Djamena, lakini mwishowe vilirudishwa na jeshi la serikali. Mwezi Oktoba mwaka 2007 serikali ya Chad ilisaini makubaliano ya amani na vikosi vya upinzani, lakini mwezi mmoja tu baadaye mapambano yalianza tena. Mwishoni mwa mwezi Desemba, vikundi kadhaa vya upinzani viliungana, na tarehe 31 Januari vikosi vya upinzani vilianza kupambana tena na jeshi la serikali na kufika mji mkuu N'Djamena.

Wachambuzi wanaona kuwa hali ya Chad licha ya kutegemea jinsi mapambano yatakavyoendelea, lakini pia inategemea misimamo ya jumuyia ya kimataifa, hasa msimamo wa Ufaransa. Kwa sababu Ufaransa ni nchi iliyokuwa inaitawala Chad, ina athari kubwa kwa Chad, sababu ya Bw. Idriss Deby kuweza kuwepo madarakani inahusiana moja kwa moja na uungaji mkono wa Ufaransa. Ufraransa kwa miaka mingi imekuwa inaiunga mkono serikali ya Chad katika mambo ya kufundisha askari, kutoa silaha, kutoa habari na huduma za kijeshi na matibabu, na Chad inaruhusu Ufaransa kuwa na askari 1200 nchini humo. Miaka miwili iliyopita vikosi vya upinzani vilipokuwa karibu na N'djamena jeshi la Ufaransa lilisaidia serikali ya Chad kusafirisha askari, kutoa huduma ya habari na pia kutoa msaada wa askari na kuvirudisha vikosi vya upinzani.

Lakini baada rais mpya wa Ufaransa kushika madaraka sera za kidiplomasia za Ufaransa zimerekebishwa, serikali ya Ufaransa inasisitiza kuwa jukumu la askari wa Ufaransa ni kulinda amani baada ya kupata idhini ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, na wala sio kushiriki kwenye migogoro ya nchi hiyo. Kuhusu mapambano ya sasa, msimamo wa Ufaransa kwa serikali ya Chad ni "kuunga mkono lakini kutoshiriki". Hivi sasa majukumu ya jeshi la Ufaransa ni kulinda madaraja, na licha ya kutoa habari za upelelezi haikutoa msaada wowote. Msimamo huo wa Ufaransa umeathiri nchi nyingi za Ulaya, tarehe 3 mabalozi wa nchi za Ulaya walifanya mkutano mjini Brussels lakini hawakutoa ratiba ya kutuma jeshi la kulinda amani nchini humo.

Hata hivyo, wachambuzi wanaona kuwa Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya hazitaruhusu Chad kuwa na serikali inayoiunga mkono Sudan. Sehemu ya mashariki ya Chad inapakana na Darfur ya Sudan, katika sehemu hiyo vikundi vyenye silaha vina shughuli nyingi. Hivi sasa kwenye sehemu za mipakani kati ya nchi hizo mbili kuna wakimbizi laki 2.4 wa Sudan na laki 1.8 wa Chad. Chad na Sudan zinashutumiana kuficha vikosi vya upinzani vya kila upande. Vyombo vya habari vya nchi za Ulaya vina wasiwasi kuwa, kama kundi la upinzani likishika madaraka ya serikali, Chad itashirikiana na serikali ya Sudan na kuifanya serikali hiyo kutumia mabavu kutatua suala la Darfur.

Hali ya Chad inaathiri hali ya usalama wa Afrika ya Kati, na pia itaathiri maslahi ya Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya. Hivi sasa bado inasubiriwa kama hatma ya mambo itakuwaje.

Idhaa ya kiswahili 2008-02-04