Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-04 16:53:42    
Mradi wa kuhifadhi mabaki ya kale ya Beijing uliofanyika kwa miaka minane umekamilika

cri

Mradi wa kuhifadhi mabaki ya kale ya Beijing uliofanyika kwa miaka minane umekamilika. Katika muda wa miaka minane iliyopita serikali ya Beijing ilitenga Yuan milioni 930 kwa ajili ya kukarabati na kuhifadhi mabaki ya kale, mafanikio yake ni makubwa.

Beijing imekuwa na miaka zaidi ya 3,000 tokea ilipoanza kujengwa na imekuwa mji mkuu wa China kwa miaka zaidi ya 800, una mabaki ya kale mengi na ni mji maarufu duniani kutokana na utamaduni wake. Mjini Beijing licha ya kuwepo kasri la kifalme, hekalu la Tian Tan na ukuta mkuu, pia kuna mabaki zaidi ya 3,500 ikiwa ni pamoja na bustani nyingi za kifalme, majengo ya kidini na makazi ya watu. Mtaalamu mashuhuri wa mabaki ya kale wa China Bw. Xu Pingfang alipozungumzia mradi huo alisema,

"Miji nchini China ina historia ndefu na ilitokea sambamba na ustaarabu wa China. Miji ya kale ilikuwa inaendelea bila kusita na pia ina vipindi vya maendeleo ya haraka, hali hiyo ni tofauti na miji ya Ulaya. Sehemu ya katikati ya mji wa Beijing ambayo ndio mji wa kale ilijengwa katika enzi za Yuan, Ming na Qing, ni matokeo ya ujenzi wa miaka mingi, zaidi ya nusu ya ustaarabu wa China umebaki katika mji huo, kwa hiyo miji ya kale ya China ni mabaki muhimu ya utamaduni wa China."

Kuanzia mwaka 2000 serikali ya Beijing ilianza kukarabati mabaki ya kale yasiyoweza kuhamishika. Mwaka 2002 serikali ya mji ilianza kutekeleza "Mpango wa Miaka 25 wa Kuhifadhi Sehemu ya Kale ya Beijing" na "Mpango wa Kuhifadhi Mji Maarufu wa Kale wa Beijing", baadaye mabaki zaidi ya mia moja yalikarabatiwa. Mkuu wa Idara ya Mabaki ya Kihistoria ya Beijing Bw. Kong Fanchi alisema,

"Katika mradi huo kazi muhimu ni kukarabati mabaki sita ya urithi wa utamaduni duniani. Kwanza ni ukarabati wa kasri la kifalme na mazingira ya pembezoni mwa kasri hilo. Pili ni ukrabati wa bustani ya Tian Tan, kazi ya kulikarabati hekalu hilo sio kubwa, kazi kubwa ni kurudisha mazingira ya awali yaliyo pembezoni mwa bustani hiyo ikiwa ni pamoja na kuhamisha wakazi na taasisi. Kwenye Pango la "Peking Man" lililopo kwenye eneo la Zhou Kou Dian kwenye kiunga cha Beijing, tumehamisha viwanda kadhaa vya saruji na viwanda vya kusaga mawe. Kwenye kasri la majira ya joto ukarabati ulifanyika zaidi kwa majengo yaliyoko kwenye mstari wa katikati, na kimsingi majengo hayo yamerejea kuwa na sura ya awali. Kazi ya kukarabati Ukuta Mkuu iligharimu fedha nyingi zaidi kutokana na urefu wake mkubwa. Kazi ya kukarabati makaburi 13 ya wafalme ilifanyika zaidi kwa makaburi mawili yaliyokuwa yameharibika."

Baada ya kupata mafanikio ya kipindi, mwaka 2003 serikali ya Beijing ilianza kutekeleza mpango wa miaka mitano wa kuhifadhi mabaki ya kale kwa ajili ya michezo ya Olimpiki, fedha zilizotumika zilikuwa Yuan milioni 600, kazi ya ukarabati ikiwa ni pamoja na Hekalu la Confucius na Chuo cha Kifalme, malango ya kuta za mji, mahekalu na majumba ya jamaa wa wafalme. Ofisa wa Idara ya Mabaki ya Kale ya Beijing Bw. Wang Yuwei alieleza,

"Kazi kubwa za ukarabati wa hekalu la Confucius na Chuo cha Kifalme ni mbili, moja ni kuondoa Maktaba ya Mji Mkuu iliyokuwepo ndani ya chuo hicho na hekalu hilo, serikali ya Beijing iliijengea maktaba hiyo kwenye sehemu nyingine, pili ni ukarabati wenyewe ambao ulikuwa mkubwa sana. Kwa mujibu wa 'Sheria ya Uhifadhi wa Mabaki ya Kale' tumebakiza alama zote za kihistoria wakati tulipofanya ukarabati."

Bw. Wang Yuwei alisema, Hekalu la Confucius na Chuo cha Kifalme baada ya kukarabatiwa vimefunguliwa kwa umma ili kuwafahamisha jinsi elimu ya kale ilivyokuwa nchini China na kutoa huduma kwa ajili ya utafiti wa historia.

Katika mradi wa kukarabati mabaki ya kale, wataalamu wa mabaki ya kale walifanya ushirikiano na wataalamu wa nchi za nje, kwa mfano katika ukarabati wa Kasri la Kifalme walishirikiana na wataalamu wa Italia, katika ukarabati wa makaburi 13 ya wafalme walishirikiana na wataalamu wa Israel, na katika ukarabati wa madhabahu ya Xian Nong Tan walishirikiana na wataalamu wa Marekani.

Hadi hivi sasa mradi wa kuhifadhi mabaki ya kale ya Beijing uliofanyika kwa miaka minane sasa umekamilika. Lakini mkuu wa Idara ya Mabaki ya Kihistoria ya Beijing Bw. Kong Fanchi alisema, mradi huo ni kazi ya kipindi hiki, Beijing ikiwa ni mji wa kale kazi ya kuhifadhi mabaki ya kale itaendelea bila kusimama. Alisema,

"Kazi muhimu katika uhifadhi wa mabaki ya kale zitakuwa ni aina mbili, moja ni kuendelea kukarabati, nyingine ni kurudisha mazingira ya awali kwa kuondoa majengo yasiyofaa kwenye mazingira hayo, na nyingine ni kuimarisha uhifadhi wa vichochoro na nyumba zenye ua wa mraba."

Bw. Kong Fanchi aliongeza kuwa michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008 umeiletea Beijing fursa nzuri ya kihistoria, michezo hiyo imehimiza kazi ya uhifadhi wa mabaki ya kale mjini Beijing, ili kufanikisha kazi ya uhifadhi wa mabaki ya kale baada ya michezo ya Olimpiki kumalizika, serikali ya Beijing imeamua kuwa kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2015 itatekeleza "Mpango wa uhifadhi wa kipindi kirefu wa ukarabati wa mabaki ya kale", na kila mwaka itatenga Yuan milioni 150.

Idhaa ya kiswahili 2008-02-04