Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-04 16:57:36    
Mradi wa kuhifadhi mabaki ya kale wa opera ya Huagu

cri

Opera ya Huagu inajulikana sana mkoani Hunan, China. Bw. Gao Wenbin ni msanii wa opera hiyo.

Mliyosikia ni opera ya Huagu, opera hiyo inapendwa kutokana na mahadhi na maneno yake yaliyo rahisi kueleweka. Nyimbo katika opera ya aina hiyo zinajulikana sana miongoni mwa wakazi mkoani. Bw. Gao Wenbin ni mmoja wa wasanii wa kundi la opera ya Huagu la wilaya ya You mkoani Hunan. Alijiunga na kundi hilo mwaka 1985, hadi sasa amekukwepo kwenye kundi hilo kwa miaka 22. Alipokumbusha jinsi alivyoanza kujihusisha na opera hiyo alisema,

"Nilianza kupenda opera ya Huagu nilipokuwa na umri wa miaka 12, na kutokana na kusikiliza opera hiyo mara kwa mara, wazazi wangu pia wanaipenda sana."

Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari ya chini, alipokuwa na umri wa miaka 16 Bw. Gao Wenbin alijiunga na kikundi kimoja cha opera hiyo katika sehemu ya makazi yake, miaka miwili baadaye alijiunga na kundi la Huagu la ngazi ya wilaya na kuwa mpigaji wa kinanda wa bendi, tokea hapo alianza maisha yake katika kundi hilo kwa zaidi ya miaka 20. Alisema,

"Nililianza kujifunza sanaa ya opera ya Huagu nilipokuwa na umri wa miaka 16, na mwaka 1985 nilipokuwa na umri wa miaka 19 nilijiunga na kundi la opera la wilaya ya You na kuwa mpigaji wa kinanda, baada ya juhudi za miaka zaidi ya 20 hatua kwa hatua nimepata maendeleo makubwa."

Mwishoni mwa karne iliyopita, Bw. Gao Wenbin mwenye juhudi nyingi amekuwa msanii muhimu wa kundi lake, alikuwa na hamu ya kupata nafasi nyingi za kufanya maonesho, lakini wakati huo wakulima wengi vijana walikuwa wanaondoka vijijini na kwenda kufanya kazi mijini, maonesho ya opera vijijini yalikuwa na hali mbaya. Hali hiyo ilikuwa pigo kubwa kwake, waigizaji wengi wa kundi lake waliondoka na kwenda kujitafutia kazi nyingine. Bw. Gao Wenbin alisema,

"Wakati huo opera za aina nyingi zilikuwa na hali mbaya sana hususan tokea mwaka 1997 hadi 2003, wasanii waishindwa kuona mustakbali mzuri, na kutokana na mishahara midogo wengi waliondoka na kwenda kufanya biashara."

Msanii Bi. Luo Xianlian aliyekuwa pamoja na Bw. Gao Wenbin katika kundi hilo alipokumbuka miaka hiyo alisema,  

"Wakati huo makundi mengi ya opera yalivunjika, isipokuwa kundi letu, hali ilikuwa mbaya sana hata mishahara yetu ilikuwa haina uhakika."

Aliyosema Bi. Luo Xianglian ni ya kweli, wasanii wengi waliondoka kutokana na wasiwasi wa maisha bila misharaha ya uhakika. Mke wa Bw. Gao Wenbin pia alimshawishi mume wake aondoke kwenye kundi lake, lakini kutokana na upendo wa opera ya Huagu alivumilia na akiwa na wakati alifanya kazi za kilimo ili kusaidia maisha ya familia yake. Bw. Gao Wenbin aliwahi kuyumbayumba alipoona wenzake walioondoka wakipata pesa nyingi kwa kufanya kazi nyingine, lakini mwishowe hakuondoka, aliamini kwamba baada ya dhiki itakuja faraja. Alisema,

"Siku zote sikuvunjika moyo, niliamini opera hiyo itafufuka."

Wilaya anakoishi Bw. Gao Wenbin ni wilaya inayozalisha mazao kwa wingi. Katika miaka ya karibuni kutokana na serikali kutilia mkazo kwenye shughuli za kilimo, uchumi wa wilaya hiyo umestawi, na maisha ya wakazi yamekuwa bora. Watu wasipokuwa na kazi hawaridhiki tena kucheza karata bali wanahitaji maisha ya kiutamaduni. Serikali ya mkoa wa Hunan ilitaka makundi ya opera yafanye maonesho vijijini. Opera ya Huagu ambayo inapendwa sana na wakazi imepata uhai mpya. Bw.Gao Wenbin alifurahi sana kuona hali hiyo. Alisema,

"Kila mahali tulipofanya maonesho wakazi wa huko walifurahi sana, na kila tulipoondoka walituuliza tutarudi lini tena?"

Bw. Gao Wenbin alisema ili kukidhi mahitaji ya wakazi, kundi lake limetunga hadithi nyingi kwa mujibu wa maisha ya wakazi. Mwaka jana kundi hilo lilifanya maonesho mara zaidi ya 300 na kila mara watazamaji walikuwa wengi. Kutokana na maonesho ya mara nyingi mishahara inaongezeka mwaka hadi mwaka. Bi. Luo Xiangqin wa kundi hilo alipozungumzia jambo hilo alisema,

"Tunaridhika sana na hali ya sasa, mishahara yetu imekuwa mara mbili kuliko mwaka jana, na sote tunaipenda kazi yetu."

Mshahara umekuwa mkubwa, Bw. Gao Wenbin anaungwa mkono zaidi na mke wake, kutokana maonesho ya kundi lake kupendwa na wakazi Bw. Gao Wenbina anaona kila siku inapita kwa furaha.

Idhaa ya kiswahili 2008-02-04