Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-04 18:38:09    
Nani anaweza kuiokoa Kenya?

cri

Ingawa vyama viwili vya Kenya vilisaini Mpango wa Amani tarehe 1 Februari usiku, lakini hali ya nchi hiyo bado si tulivu. Jumuiya ya kimataifa inatiwa wasiwasi tena kuhusu hali inavyoendelea nchini humo.

Mapambano yaliyotokea tena tarehe 2 na tarehe 3 Februari nchini Kenya yamesababisha vifo vya watu 13, na wengine kumi kadhaa kujeruhiwa, na nyumba zaidi ya 200 kuteketezwa. Aidha kwenye sehemu ya mipaka kati ya mikoa ya Bonde la Ufa na Nyanza iliyoko kwenye sehemu ya magharibi nchini Kenya, pande mbili zilizopambana zilitumia upanga, upinde na mishale. Aidha kanisa lililoko huko Eldoret mkoani Bonde la Ufa lilichomwa moto na kuteketezwa.

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan anayefanya usuluhishi nchini Kenya anaona kuwa, mapambano yanayoendelea nchini Kenya yamekiuka eneo la migongano ambayo ilisababishwa kutokana na matokeo ya uchaguzi wa urais wa nchi hiyo, hali ambayo imesababisha migogoro mingine iliyopo kwa muda mrefu nchini humo kati ya makabila mbalimbali, kutokana na pengo kati ya umaskini na utajiri, na mgawanyo wa raslimali usio wa haki. Je, nani ataiokoa Kenya?

Wakati nchi za Afrika zilipopata uhuru, nchi zilizozitawala nchi hizo za Afrika zilieneza kwa nguvu "Demokrasia" ya nchi za magharibi, lakini demokrasia hiyo haikutia mizizi ya kawaida barani Afrika kutokana na demokrasia hiyo kutolingana na hali halisi ya nchi za Afrika. Aidha baada ya wakoloni wa Uingereza kuikalia Kenya, walizusha migogoro kwa makusudio, hatua ambayo ilisababisha migongano kati ya makabila katika nchi nyingi za Afrika ikiwemo Kenya ambayo migongano hiyo inaendelea mpaka sasa. Kutokana na historia ya ukoloni barani Afrika, na njama ya nchi fulani ya kujaribu kuanzisha makao makuu ya jeshi lake barani Afrika, tukajua kuwa nchi za magharibi kamwe hazitakuwa mwokoaji wa Kenya.

Viongozi wa nchi za Afrika wamesisitiza mara kwa mara kuwa, waafrika wanapaswa kuondoa matatizo kwa kujitegemea. Je, Umoja wa Afrika ukiwa jumuia kubwa zaidi na yenye uwezo mkubwa zaidi wa ushawishi barani Afrika, unaweza kufanya kazi kubwa ya namna gani? Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika uliomalizika hivi karibuni huko Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, unazitaka pande zinazohusika zijizuie, na kuviharakisha vyama vinavyohusika viondoe migogoro kwa njia ya amani. Lakini inakadiriwa kuwa hivi sasa Umoja wa Afrika bado hauna uwezo wa kuchukua hatua halisi. Mwenyekiti wa zamani wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni rais wa Ghana Bw. John Kufuor alieleza kuwa, hakuna shirika maalum kwenye Umoja wa Afrika linaloshughulikia kusaidia nchi wanachama wake kuondoa migongano inayotokana na uchaguzi mkuu. Aidha, Umoja wa Afrika unakabiliwa na ukosefu mkubwa wa mitaji.

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan na "kikundi cha watu maarufu wa Afrika" kinachoongozwa naye walifanya usuluhishi na kupata maendeleo makubwa, lakini kama alivyosema mjumbe wa Kamati ya marekebisho ya katiba ya Kenya ambaye pia ni mwanasheria wa mahakama kuu ya nchi hiyo Bw. Lumumba Mumma Kaluma, wasuluhishi wengi duniani waliingia na kuondoka kutoka Kenya, labda kazi zao ziliathiri vizuri hali ya mambo, lakini baada ya kuondoka kwao, matokeo ni tofauti, hali kadhalika kwa Bw. Annan.

Ukweli ndio hivyo. Ghasia kubwa zilizodumu kwa mwezi mmoja nchini Kenya zimesababisha vifo vya watu wengi na hasara kubwa kwa nchi hiyo. Kama viongozi wa Kenya wataendelea na mazungumzo kwa kufuata Mpango wa Amani, wananchi wa Kenya watashikilia kujizuia, na wakenya wote watajiita kuwa ni wakenya wala si kutoka kabila fulani, basi kuna uwezekano kuwa amani, utulivu, ustawi na maendeleo yatarejeshwa nchini Kenya.