Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-04 19:34:01    
Mkahawa wa "Jasmini" na mwendeshaji wake mgeni

cri

Kwenye mji wa Jinan, mji mkuu wa mkoa wa Shangdong ulioko kwenye sehemu ya mashariki ya China, kuna eneo moja wanaloishi kwa wingi waislamu, katika eneo hilo kuna mkahawa wa kipekee wa kihindi, ambao kila siku unakuwa na wateja wengi. 

Mara tu baada ya kuingia kwenye mkahawa wa "Jasmini", mtu anaweza kusikia harufu ya udi wa India na harufu ya bizari kwenye vitoweo, kuta za mkahawa huo zimebandikwa picha za mandhari ya kimaumbile na posta kadi za India na Pakistan, na televisheni inaoneshwa video ya ngoma ya India, watumishi wa mkahawa huo wote ni wahindi wanaovaa mavazi ya kihindi, nyimbo na ngoma za asili ya India pamoja na wateja wanaoongea kwa lugha za aina mbalimbali, vinawafanya watu waone kama wamefika katika nchi ya India.

Kwenye mkahawa huo, mwandishi wetu wa habari alimwona Bw. Shadi, ambaye ni kijana na mrefu, aliyekuwa mwendeshaji wa zamani wa mkahawa wa "Jasmini", na ni rafiki mkubwa wa Bw. Naveed, ambaye ni mwendeshaji wa sasa wa mkahawa huo. Alipomweleza mwandishi wetu wa habari wazo lake la kufungua mkahawa huo, Bw. Sadi alisema,

"Marafiki zangu wengi ni wapakistan na wahindi, marafiki zangu hao bado hawajazoea chakula cha kichina, hivyo nilifungua mkahawa wa "Jasmini" na kuuza vitoweo vya kihindi."

Hivi sasa Bw. Shadi anasoma katika chuo kikuu cha Shandong, wakati alipofika mjini Jinan zaidi ya miaka minne iliyopita, pia hakuzoea vitoweo vya kichina, hivyo alifungua mkahawa huo. Hivi sasa licha ya wahindi na wapakistan, hata baadhi ya wageni wanaotoka nchi nyingine, wanakula chakula katika mkahawa huo. Lakini Bw. Shadi ameishi mjini Jinan kwa miaka mingi, na ameanza kupenda vitoweo vya kichina, hasa anavutiwa sana na utamaduni wa China wenye historia ya miaka mingi. Alisema,

"Ninapenda sana utamaduni wa China, nimefika China kwa ajili ya kujifunza utamaduni na uchumi wa China. Mwanzoni mambo mengi sikuyafahamu, marafiki zangu walinisaidia sana. Sasa ninaipenda China sana, kwani China ni nchi nzuri sana."

Bw. Shadi alisema, anafanya shughuli za biashara nchini China anapata nafuu nyingi za kisera, hivyo biashara yake ya mkahawa ni nzuri sana. Anasema hali ya hewa ya Jinan ni nzuri, mji ni safi sana, watu ni wachangamfu na wana urafiki, kwa hiyo anataka kuishi siku zote kwenye mji huo, alisema,

"Mtu hatapata shida katika mahitaji yake ya maishani, ninaweza kupata vitu vizuri katika sehemu mbalimbali. Hivi sasa kila kitu kinapatikana nchini China, katika nchi za nje kiasi cha 90 ya bidhaa ni kuagizwa kutoka China, makochi, televisheni na kompyuta zote zinatengenezwa hapa China. Niliishi nchini Ufaransa kwa miaka miwili, nchini Uingereza kwa miaka sita, na Russia kwa nusu mwaka, ninaona China ni nchi nzuri zaidi, kwa sababu wachina ni watu wema, wana tabia nzuri, na wanapenda kusaidia watu."

Bw. Shadi anaishi kwa furaha mjini Jinan, amepata marafiki wengi. Nusu mwaka iliyopita, rafiki yake mpakistan Naveed alichukua mkahawa wa "Jasmini" na kuwa mwendeshaji wa pili wa mkahawa huo. Pakistan ni nchi jirani ya India, nchi hizo mbili zina mazoea ya namna moja katika chakula, tena zina desturi zinazofanana. Kwa hiyo ni sawa kabisa kwa Bw. Naveed kuendesha shughuli za mkahawa huo, alisema,

"Katika miji ya Beijing, Shanghai, Guangzhou na Yiwu, watu wanaweza kupata vitoweo vya kihindi na kipakistan, lakini katika mji wa Jinan, hawawezi. Niliona mji wa Jinan una wageni wengi wa nchi za nje, wamarekani na waingereza pia wanapenda kula vitoweo vya kihindi. Katika mkahawa wangu kuna wateja wageni wengi."

Bw. Naveed alisema baadhi ya chakula na viungo vinavyotumika kwa kupika vitoweo katika mkahawa huo, vinaletwa kutoka India na Pakistan, hata wapishi wanatoka India au Pakistan, kitu kinachozingatiwa zaidi ni sifa ya mkahawa huo. Katika mkahawa huo wageni wanaweza kupata aina nyingi za vyakula vya kihindi, hususan wali uliopikwa kwa bizali, wali huo unapikwa kwa viungo vingi vya kiwango cha juu, hivyo unanukia vizuri na kupendwa sana na wateja.

Wali na vitoweo vizuri vinawavutia sana wateja, hivyo shughuli za biashara ya mkahawa inakuwa nzuri siku hadi siku. Bw. Naveed alisema licha ya kuhakikisha ubora wa chakula, mkahawa huo unazingatia kutoa huduma bora. Kwa mfano, baadhi ya wateja wanaopenda chakula chenye ladha nzito ya viungo, wanapochagua chakula hupenda kuchagua chakula chenye pilipili nyingi, wakati huo huo watumishi wa mkahawa wanawashawishi wabadilishe na kuchagua chakula chenye pilipili kidogo, kwani chakula chenye pilipili nyingi kinaathiri matumbo na utumbo wa chakula. Mambo hayo madogo hufanya wateja waone kama wako nyumbani mwao. Hivi sasa wateja wa mkahawa huo siyo wageni peke yao, wateja wachina pia wanaongezeka kwa wingi.

Ili kukidhi mazoea ya wateja wachina, mkahawa umetoa vitoweo vya aina mbili kwa wateja: vyenye pilipili na visivyo na pilipili. Mwanafunzi wa Pakistan anayesoma katika chuo kikuu cha udakatari cha Shandong Bw. Mohamad Yousaf ni mteja anayefika kwenye mkahawa huo mara kwa mara, na sasa amekuwa rafiki mkubwa wa Bw. Naveed. Bw. Yosaf alisema kila anapokumbuka chakula cha nyumbani, huwa anakwenda kwenye mkahawa huo.

"Mwanzoni baada ya kufika katika mji wa Jinan, ilikuwa ni vigumu kupata chakula cha waislamu, baada ya kufunguliwa kwa mkahawa wa "Jasmini", wanafunzi kama mimi tunajisikia vizuri sana."

Kwa watu wanaoishi ugenini, itakuwa ni jambo la kufurahisha sana kuweza kupata chakula cha nyumbani. Bw. Yosaf alisema, anaishi kwa furaha katika mji wa Jinan kama anaishi kwao kabisa. Sasa anafurahia zaidi maisha yake kwa kuwa amepata marafiki wengi wa China, anaweza kupata chakula cha kichina, tena anafika kwenye mkahawa wa "Jasmini" wakati anapokumbuka nyumbani kwao. Alisema,

"Ninaishi Jinan kwa furaha, sina shida yoyote, watu wa Jinan ni wema sana, ninaishi hapa bila tatizo lolote. Kama nitapata nafasi ya kuishi siku zote nchini China, hakika nitachagua kuishi hapa."

Mwenyedeshaji wa mkahawa wa "Jasmini", Bw. Naveed pia hataki kuondoka huko, anasema sasa biashara yake inaendelezwa vizuri sana, mkahawa wake unaonekana hauwezi kupokea idadi kubwa ya wateja, sasa amenuia kufungua mkahawa mwingine mkubwa zaidi.