Baada ya mapambano ya siku mbili, tarehe 4 hali ya N'djamena mji mkuu wa Chad ilirudi kuwa ya utulivu. Vikosi vya upinzani havikufanya mashambulizi tena baada ya kuondoka mjini humo alasiri tarehe 3. Jioni ya tarehe hiyo serikali ya Chad ilitangaza kwamba imekomesha jaribio la uasi. Lakini vikosi vya upinzani vilisema "vinaondoka kwa mbinu za kivita", na hivi sasa viko nje tu ya mji huo na vitafanya mashambulizi tena.
Tarehe 4 mjini N'djamena askari wa Chad walikuwa wakifanya doria mitaani, magari ya kijeshi yalikuwa yakipita barabarani, miili ya watu ilikuwa inaonekana hapa na pale na majengo ya redio ya taifa na masoko yaliharibiwa vibaya, helikopta zilikuwa zinavinjari angani na milio ya mlipuko ilikuwa inasikika mara moja moja. Kutokana na kuhofia vikosi vya upinzani kuanza tena mashambulizi, wakazi laki saba wa mji wa N'djamena na wakazi walio karibu na mji huo wamekimbilia kwenye sehemu ya mpaka wa Cameroon. Kwa mujibu wa takwimu za serikali ya Cameroon, kwenye mji mdogo wa Kousseri tu wakimbizi elfu 15 wamekusanyika huko.
Baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukutana, tarehe 4 lilitoa taarifa ya mwenyekiti ikionya vikali vikosi vya upinzani kwa kuharibu utulivu wa taifa, taarifa hiyo pia imezitaka nchi zote wanachama wa baraza hilo zitoe msaada kwa mujibu wa matakwa ya serikali ya Chad na kwa kufuata katiba ya Umoja wa Mataifa. Mwakilishi wa Chad katika baraza hilo Bw. Mahamat Adoum tarehe 3 aliwasilisha "Ombi la Msaada" akitaka misaada ya aina yote inayowezekana ili kumaliza msukosuko huo.
Wachambuzi wanaona kuwa taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imezisaidia Ufaransa na nchi nyingine zinazohusika na Chad kwa manufaa kuingilia kati msukosuko huo. Serikali ya Ufaransa siku zote inasisitiza kuwa kuweko kwa jeshi la Ufaransa kunatokana na idhini ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, na wala sio kuingilia kati mgogoro wa ndani wa nchi ya Chad. Lakini kutokana na kutotaka kuacha maslahi na athari yake, serikali ya Ufaransa ilikuwa ikijitahidi na kutafuta usuluhishi kutoka nchi nyingine. Rais wa Ufaransa aliwahi kusema Ufaransa ikipata tu idhini ya Umoja wa Mataifa, jeshi la Ufaransa "litaingilia kati kwenye mgogoro huo moja kwa moja". Hivi sasa ndege za kivita za Ufaransa zimekuwa zikiruka pambezoni mwa Chad na Sudan, ili kuzuia nchi nyingine kuivamia Chad. Sambamba na hayo, jeshi la kulinda amani la Umoja wa Ulaya lenye askari elfu 3,700 ambao wengi wao ni askari wa Ufaransa wako tayari kwenda kutekeleza majukumu nchini Chad.
Marekani inaunga mkono msimamo wa Ufaransa. Mwakilishi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa alisema, Ufaransa ina uwezo wa kukabiliana na suala la Chad kwa busara na kwa uongozi, "kama Ufaransa ikifanya mambo mengi zaidi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaiunga mkono."
Hivi sasa kwa mujibu wa azimio la Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo na Libya zimeamua kutuma wajumbe kusuluhisha mgogoro wa Chad, na pamoja na hayo majeshi ya nchi za nje pengine yakaingia nchini kuisaidia serikali kudhibiti hali ya msukosuko.
Idhaa ya kiswahili 2008-02-05
|