Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-05 17:55:04    
Barua 0203

cri

Msikilizaji wetu Emmanuel Bernard wa sanduku la posta 71 Tarime Mara Tanzania, ametuletea barua pepe akisema anafurahia sana kupata matangazo yetu kila siku kwa njia nzuri sana. Anasema anapenda kutumia fursa hii kutoa maoni yake kuhusu matangazo yetu kwa mwaka mzima wa 2007, hasa kuhusu kipindi cha Sanduku la barua na Salamu zenu. Angeomba vipindi hivyo viongezwe muda wa kutosha. Vilevile Ukimwi limekuwa ni jambo linalowatesa sana watu, ingekuwa vizuri kama kungekuwa na kinachohusu ugonjwa wa Ukimwi. Na Mwisho anasema, anapenda kutukumbusha kuwa, zawadi yake ya ushindi wake wa tatu kwenye shindano la chemsha bongo bado hajapata. Vile vile anasema kwenye shindano la sasa pengine tunaweza kuwaona wana Kemogemba wakija kushuhudia michezo ya Olimpiki. Anatutakia kila la heri, na heri ya mwaka mpya wa jadi wa China.

Tunamshukuru Emmanuel Bernard kwa barua yake ya kueleza maoni yake kuhusu vipindi vyetu na kueleza matumaini yao ya kupata ushindi kwenye shindano la chemsha bongo, ni matarajio yetu kuwa tutawaona wana Kemogemba kushuhudia Michezo ya Olimpiki hapa Beijing, China.

Msikilizaji wetu mwingine Bw Hilal Nasor Al-Kindy Sanduku la barua 22 Al-Amrat Oman ametuandikia barua akisema, ni muda umepita hajapata barua wala picha au gazeti toka kwetu, basi anaomba kama tukipata barua hii, basi tusimsahau kwa vitu hivyo vyenye picha za kuvutia zenye sura ya nchi, miti, wanyama, milima na vinginevyo.

Wasikilizaji wetu Augustine Athanas na Susan Masaba kutoka kijiji cha Ng'wang'wali sanduku la barua 116 Bariadi, Shinyanga Tanzania wametuandikia barua wakisema, wao ni wazazi wa Yakobo Mvanga anayesoma Seminari ya Makoko, wamefurahi sana kwa zawadi nzuri ya kitambaa cha mezani, tulichomtumia mwanao, baada ya ushindi wa chemsha bongo. Wanasema wao ni watanzania lakini wamebahatika kupata zawadi ya kitambaa kutoka kwa wachina, hii imewafurahisha sana. Wanasema kama familia yao ingekuwa na uwezo wangekuja China kutoa shukurani, kwa hiyo wamechagua njia ya kutoa shukurani kwa njia ya barua. Wanamaliza barua yao kwa kuomba tuwasalimu wachina wote.

Tunawashukuru Augustine Athanas na Susan Masaba kwa barua yao, kweli tunafurahia mafanikio waliyopata katika chemsha bongo, ni matumaini yetu kuwa wataendelea kusikiliza matangazo yetu na kushiriki kwenye chemsha bongo ya kila mwaka, ni matarajio yetu kuwa tutaweza kukutana hapa Beijing, China.

Msikilizaji wetu Daniel Ngoya S.L.P.172 Bungoma Kenya ametuletea barua akisema, anapenda kuchukua fursa hii kutoa salamu zake kutoka huko Lwanda, akitumai wasikilizaji na watangazaji wa Radio China Kimataifa wote ni buheri wa afya. Angependa kutujulisha kuwa, huko Lwanda kuna wasikilizaji wengi ambao wanapenda kushiriki kwenye matangazo ya idhaa yetu, lakini tatizo ni kwamba hawana kadi za salaam. Wao wanafuatilia matangazo yetu, kwani yanawaelimisha na kuwaburudisha, na wangependa kushukuru kwa hayo yote ambayo tunafanya.

Anasema wao kama watoto wa Lwanda kweli wangependa tuwe tunawatumia maswali, ili kama bahati ikiwaangukia washinde shindano la chemsha bongo basi waweze kuja kutembelea China, na kama nyota njema ikiwaangukia watakuwa na furaha kubwa isiyo kifani. Anasema hayo ni maombi yao, na pia anapenda kukumbusha kuhusu kutumiwa kadi za salamu, ili nao waweze kuwasalimia wasikilizaji wengine wanaowakumbuka kwa salamu.

Pia ana ombi binafsi, anasema angependa kupata radio moja ndogo kutoka China ili aweze kusikiliza vizuri matangazo yetu; na anapenda kukamilisha barua yake kwa kuwasalimu wafuatao: Amos Wafula, Shariff Samuel, Wasilwa Vitalis, Wekesa Rob, Mkuu wa bweni wa Lwanda Madam Ruth na wengine wengi ambao hajawataja.

Tunamshukuru Bw. Daniel Ngoya kwa barua yake, leo tumesoma barua tatu ambazo zimeeleza matarajio ya kupata ushindi kwenye chemsha bongo ya mwaka huu ili kupata fursa ya kuja China kushuhudia Michezo ya Olimpiki, tunafurahi sana, na kuwatakia wasikilizaji wetu kila la heri.

Msikilizaji wetu Amos Nyongesa wa SLP 165 Shule ya Sekondari Bungoma, Kenya ametuandikia barua akianza kwa salamu kwa watangazaji na wasikilizaji wa Radio China kimataifa. Anasema ni matumaini yake kuwa mwaka huu tumepanga mengi ya kuboresha matangazo yetu. Yeye ni mzima na anaendelea kusikiliza vipindi vyetu katika wakati wa likizo. Yeye ni mwanafunzi katika shule ya upili ya Bungoma juu. Anatupongeza kwa kazi tunayoifanya, kwani tuna watangazaji shupavu wanaokizungumza Kiswahili kwa ufasaha huku wakizingatia sarufi. Anasema jambo hili limempa hamasa ya kuipenda zaidi Radio China Kimataifa.

Pili, anasema angependa kutumia fursa hii kuishukuru Kampuni inayosambaza bidhaa na dawa za Kichina, ya Tianshi. Kampuni hiyo imewasambazia dawa zenye manufaa makubwa kwao. Hata yeye kwa sasa ni mwanachama wa Tianshi, na huwa anatumia baadhi ya bidhaa za Tianshi, amenufaika sana na anajivunia kushirikiana na kampuni hiyo. Kwa kweli, ada ya mja hunena, muungwana ni kitendo. Matendo yetu yamemfanya yeye mkenya aone uungwana wetu, na kuona juhudi zetu katika kuwaelimisha na kuwaburudisha. Anatushukuru sana na anatutakia kila la heri.

Tunamshukuru Amos Nyongesa kwa barua yake ya kueleza maoni yake kuhusu usikivu wa matangazo yetu na kutokana na maelezo yake tumeona amekuwa na mawasiliano mazuri na wachina kadha wa kadha, ni matumaini yetu kuwa urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika utaimarishwa siku hadi siku.

Bw. Noel Mashauri wa Seminari ya Ntungamo SLP 227, Bukoba, Tanzania ametuandikia barua akisema, kwanza angependa kuwajulia hali wasikilizaji na watangazaji wa Radio China kimataifa, anasema yeye anaendelea na masomo yake akiwa buheri wa afya.

Kwanza, anatupongeza kwa kazi nzuri ya kuwapatia habari kemkem hasa kutoka nchini China, na matangazo kuhusu fahari na urithi uliopo nchini China, kwa hilo anatupongeza sana, na zaidi ni juhudi kubwa zilizopo tangu uongozi mpaka mhusika wa mwisho anayefanikisha matangazo yawafikie wasikilizaji, ya kuunganisha China na bara la Afrika hasa Afrika ya Mashariki, pia nia kubwa ya kila mwaka kutaka angalau mtu mmoja, baina ya wasikilizaji kupata wasaa wa kutembelea China.

Pili, Bw Mashauri anapenda kutufahamisha kuwa anuani yake mpya, na kutuambia kuwa, seminari ya Ntungamo ni seminari kubwa kwa maandalizi ya mapadri. Kwa hiyo ataendelea kutumia anwani hiyo mpaka hapo atakapotujulisha vinginevyo. Anaomba samahani kutokana na kushindwa kuwa na mawasiliano nasi, na anatuomba tusichoke.

Tatu, anapenda kuwajulisha wapenzi wote wa salamu, na wasikilizaji wa Radio China kimataifa kuwa, anapatikana kwenye anwani hiyo na wadumishe mawasiliano kwa njia ya salamu na barua. Pia, anaomba Wang Xiaobin, atumiwe anwani hii ili amwandikie, kwani kwa sasa hafahamu anuani yake mpya, ila anafahamu kuwa yuko idhaa ya kihindi ya hapa Radio China Kimataifa.

Tunamshukuru sana Noel Mashaur kwa barua yake ya kueleza maoni na mapendekezo yake kwa matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, tumeona yeye anasikiliza kwa makini matangazo yetu, na mapendekezo yake yanaweza kutusaidia kutoa ripoti kwa ofisi husika ya CRI ili siku zijazo tuwahudumie vizuri zaidi wasikilizaji wetu.

Idhaa ya kiswahili 2008-02-05