Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-19 15:43:20    
Maisha mapya ya wachezaji wa mchezo wa Mukamu kwenye sehemu ya Tulufan mkoani Xinjiang

cri

Sanaa ya Mukamu ni maonesho ya mchanganiko wa nyimbo, ngoma na muziki wa kabila la Wauyghur kwenye mkoa unaojiendesha wa Xinjiang. Kuna maonesho ya Mukamu ya aina kadhaa kwenye sehemu mbalimbali mkoani humo, kati ya hayo Mukamu ya sehemu ya Tulufan ni sehemu muhimu ya sanaa hiyo ya kabila la Wauyghur. Mukamu ya Tulufan ina umaalumu wa kuwa na nyimbo zenye historia ndefu, muziki mpya, kuonesha vitu mbalimbali na kuweza kuchezwa pamoja na ala maalumu za muziki za kichina zikiwemo Suona, na mchezo huo wa sanaa hasa umestawi zaidi kwenye tarafa ya Lukeqin ya wilaya ya Shansha na wilaya nyingine jirani.

Bw. Yili Muhemati ni msanii wa Mukamu. Zamani alikuwa mwailmu wa chuo cha ualimu, lakini anapenda sana mchezo wa sanaa ya Mukamu, na mwaka 1997 aliacha kazi ya ualimu na kuanza kujifunza sanaa ya Mukamu. Bw. Muhemati alipata kanda ya rekodi ya maonesho ya msanii hodari wa zamani wa Mukamu, na alijifunza mchezo wa sanaa ya Mukamu kwa kusikiliza kanda hiyo kwa miaka mitano. Sasa Bw. Muhemati amekuwa msanii maarufu wa Mukamu, anafanya kazi katika idara ya utamaduni ya serikali ya mtaa. Alisema,

"Mazingira ya idara ya utamaduni ni mazuri sana, ninaandika nyimbo za Mukamu na kufanya mazoezi kila siku. Nimemaliza kujifunza mambo yote ya mchezo wa sanaa ya Mukamu."

Bw. Hujiamuniyazi Kewuer ni mfanyakazi mwenzake. Yeye alianza kujifunza kucheza ngoma ya Mukamu alipokuwa na umri wa miaka 12. kutokana na kupenda sana sanaa ya Mukamu, mzee Kewuer mwenye umri wa miaka 85 amejishughulisha na sanaa ya Mukamu kwa miaka 73. Sasa yenye ni msanii wenye umri mkubwa zaidi wa maonesho ya sanaa ya Mukamu katika idara hiyo. Alisema,

"Mimi nina afya njema, kucheza ngoma ya Mukamu ni kama kufanya mazoezi ya kujenga mwili, na kunasaidia afya yangu."

Mzee Kewuer alikumbusha kuwa, zamani wasanii wa Mukamu walikuwa wachache sana, kwa kuwa mazingira ya kujifunza sanaa hiyo hayakuwa mazuri. Wasanii hao walikusanyika na kufanya mazoezi kwa hiari katika sehemu mbalimbali, hasa kwenye harusi za watu wa kabila la Wauyghur. Lakini katika miaka kadhaa iliyopita, serikali ilitoa msaada mkubwa kwa kuhifadhi na kuendeleza mchezo wa sanaa ya Mukamu. Wilaya ya Shanshan ya sehemu ya Tulufan ilianzisha shughuli za kuhifadhi mabaki ya utamaduni, na kuanzisha idara maalumu ya utamaduni, mbali na hayo serikali ya wilaya hiyo pia ilitenga fedhaa maalumu kwa ajili ya kupa ruzuku ya kila mwezi kwa wasanii 11 hodari wa mchezo wa sanaa ya Mukamu. Sasa mzee Kewuer anapata ruzuku ya yuan mia nne kwa mwezi.

Mwaka 1999, serikali ya wilaya ya Shanshan ilinunua ala za muziki na nguo za maonesho kwa ajili ya wasanii wa Mukamu zenye thamani ya yuan elfu kumi kadhaa, aidha mwaka huo serikali hiyo pia ilichapisha vitabu na CD kuhusu mchezo wa Mukamu kwa lugha mbili za makabila ya Wahan na Wauyghur kwa gharama ya yuan elfu 50. Sasa mapato ya wasanii wa Mukamu pia yanaongezeka kwa kiasi kikubwa. Bw. Muhemati alisema,

"Sisi wasanii wa Mukamu tunafurahi sana, na tunapenda kufanya maonesho ya mchezo wa sanaa ya Mukamu. Zamani tulifanya maonesho hayo bila kupata mapato, hata tuliwahi kutaka kuacha kazi hiyo. Lakini sasa serikali inatupa ruzuku, tunafurahi sana. Aidha vijana wanaopenda kujifunza mchezo huu wa sanaa, pia wanaongezeka siku hadi siku."

Mwezi Septemba mwaka jana, kituo cha kwanza cha kufundisha na kufanya maonesho ya mchezo wa Mukamu kilianzishwa kwenye tarafa ya Lukeqin ya wilaya ya Shanshan. Kutokana na takwimu zinazohusika, mwaka 2007 idadi ya waandishi wa habari kutoka nchini na nchi za nje waliofanya mahojiano kwenye kituo hicho ilikuwa zaidi ya elfu tatu. Kwa kupitia magazeti, radio, televisheni na mtandao wa Internet, watu wengi siku hadi siku wanaanza kufahamu mchezo huo maalumu wa kabila dogo. Sasa maonesho ya Mukamu yametoka mkoani Xinjiang, na kuanzia mwaka 1992, wasanii wa Mukamu walifanya maonesho mara nyingi kwenye miji mikubwa nchini China ikiwemo Beijing na Shanghai. Mwaka 2000, wasanii wazee wa Mukamu walikwenda nchini Uingereza kufanya maonesho, hata malkia wa nchi hiyo alikutana nao.

Kutokana na mchezo wa Mukamu kuendelea siku hadi siku, Bw. Muhemati ambaye ni katibu wa idara ya utamaduni ya tarafa ya Lukeqin anaona kuwa kuwafundisha wachezaji vijana wa mchezo huo ni muhimu sana, hata alishauri kueneza mchezo wa Mukamu kwenye shule. Alisema itakuwa vizuri endapo shule za sehemu za Tulufan zitawaajiri walimu wa mchezo huo na kuanzisha vipindi viwili vya Mukamu kwa wiki. Bw. Muhemati aliyekuwa mwalimu haridhiki sana na jinsi vijana wanavyojifunza mchezo wa Mukamu. Alisema,

"Ninawataka wajifunze kwa makini, kusikiliza vizuri na kufanya mazoezi vizuri."

Bw. Muhemati aliwaambia waandishi wetu wa habari kuwa, akiwa msanii wa Mukamu, anapenda mchezo huo uvutie watu wengi zaidi ili upate maendeleo makubwa zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2008-02-19