Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-11 18:14:42    
Sherehe za mwaka mpya wa China huendelea kwa siku 15

cri

Siku ya tano ya mwaka mpya ni siku ya kumkaribisha mungu wa utajiri kwa kumfanyia tambiko. Masimulizi ya kale yanasema, siku hiyo mungu wa utajiri anakuja duniani na kuwaletea wanadamu bahati ya kutajirika. Kwa hiyo watu hufanya sherehe ya kumkaribisha. Lakini hivi leo watu wengi hawafanyi sherehe hiyo, na badala yake wanakula jiaozi, chakula ambacho ni kama sambusa ndogo iliyochemshwa.

Kwa sababu umbo la jiaozi linafanana na pesa za China ya kale, katika siku hiyo watu wanakula chakula hicho kwa maana ya kuingiza fedha nyumbani, na ndani ya jiaozi kuna vijazo vya aina tofauti, kwa mfano ndani ya chakula hicho kukiwa na peremende, itamaanisha kuwa mtu anayekula peremende hiyo atakuwa na maisha matamu.

Siku ya 15 ya mwaka mpya ni sikukuu ya taa. Katika usiku wa siku hiyo mwezi unakuwa wa mviringo kabisa kwa mara ya kwanza katika mwaka. Jioni watu wanatoka majumbani na kwenda kuangalia aina mbalimbali za taa na kutegua vitandawili vilivyotundikwa pembeni mwa taa.

Katika siku hiyo watu hula vidonge vya unga unaonatanata, kwa Kichina vinaitwa "Yuan Xiao". Ndani ya vidonge kuna kijazo na vinapikwa kwa kukaangwa au kuchemshwa. Katika lugha ya Kichina matamshi ya "Yuan Xiao" yanafanana na matamshi ya "kuungana" ikimaanisha wanafamilia wanaungana na kuishi kwa upendo. Kwa sababu mwezi wa siku hiyo ni mviringo kamili, wanafamilia wanapokula chakula hicho huwakumbuka jamaa zao walioshindwa kurudi nyumbani na kuwatakia kila la heri.

Baada ya sikukuu ya taa yaani tarehe 15 Januari katika kalenda ya Kichina, shamrashamra za mwaka mpya zinaisha. Kwaherini!

Idhaa ya kiswahili 2008-02-05