Pakistan ni nchi jirani mwema wa China, licha ya kuwa nchi hizo mbili zina uhusiano mzuri wa kisiasa na kiuchumi, pia zina ushirikiano mkubwa katika mambo ya michezo. Kadiri michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 inavyokaribia, ndivyo Pakistan inavyozidi kufuatilia hali ya maandalizi ya michezo hiyo. Tarehe 12 mwandishi wetu alizungumza na mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Olimpiki ya Pakistan Bw. Arif Hassan. Kwenye mazungumzo Bw. Arif alisema,
"Neno ninalotaka kueleza kwa ufupi kuhusu hali ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing, ni 'nzuri sana'. Wachina wamefanya kazi nzuri sana na sisi pia tunajivunia kazi yao. Urafiki kati ya Pakistan na China ni mzuri, tunapoona jinsi wanavyoandaa vizuri michezo ya Olimpiki pia tunaona fahari, tunawatakia kila la heri."
Kamati ya Michezo ya Olimpiki ya Pakistan ilianzishwa mwaka 1948, kamati hiyo ina ushirikiano wa miaka mingi na Kamati ya Michezo ya Olimpiki ya China. Kufanyika kwa michezo ya 29 ya Olimpiki mjini Beijing kumeleta ushirikiano mkubwa zaidi kati ya kamati hizo mbili. Bw. Arif Hassan anaridhika sana na ushirikiano huo. Alisema,
"Kamati ya Michezo ya Olimpiki ya Pakistan na Kamati ya Michezo ya Olimpiki ya China zina ushirikiano wa karibu sana, na ushirikiano huo ulianza hata kabla ya Beijing kupata nafasi ya kuwa mwenyeji wa michezo hiyo. Ndugu wa China wametoa misaada mingi kwa michezo ya Pakistan ikiwa ni pamoja na kuwandaa wachezaji wa kuogelea na wa mpira wa meza, na ushirikiano huo unaendelea hadi sasa, na pia sasa tunawasiliana zaidi kutokana na michezo ya Olimpiki ya Beijing."
Kama alivyosema Bw. Arif Hassan, katika miaka ya karibuni kamati hizo mbili za michezo ya Olimpiki zimekuwa na ushirikiano mkubwa zaidi. Mwandishi wetu alipokuwa anazungumza na Bw. Arif Hassan ofisini mwake, aliwaona wafanyakazi wa Kamati ya Michezo ya Pakistan wakishughulika na maandalizi ya kumkaribisha Bw. Jiang Xiaoyu, naibu mwenyekiti mtendaji wa Kamati ya Maandalizi ya Michezo ya Beijing atakayefanya ziara nchini Pakistan.
Imefahamika kwamba ziara ya Bw. Jiang Xiaoyu nchini Pakistan, ni kwa ajili ya shughuli za kukimbiza mwenge wa Olimpiki nchini humo, mji mkuu wa nchi hiyo Islamabad ni moja ya miji ambayo mwenge wa Olimpiki utapita. Serikali ya Pakistan imefanya juhudi nyingi ili kuufanya mwenge huo uweze kukimbizwa nchini humo bila matatizo. Bw. Arif Hassan alisema,
"Tuko mbioni kufanya maandalizi ili watu wote waone shamshamra kubwa kama ya sikukuu, kabla ya mwenge kuwasili nchini na kabla ya kuanza kwa michezo ya Olimpiki ya Beijing tutafanya shughuli nyingi mfululizo kupitia televisheni, redio, filamu na magazeti ili kuwafahamisha watu wetu umuhimu wa michezo ya Olimpiki na hasa michezo hiyo ya Beijing."
Kwenye mazungumzo Bw. Arif Hassan alieleza hali ya maandalizi ya wachezaji wa Pakistan watakaoshiriki kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing. Alisema timu ya mpira wa magongo imepata nafasi ya kushiriki kwenye michezo hiyo, na hivi sasa wachezaji wa ndondi wanachujwa mjini Kazakhstan, ana matumaini kuwa wachezaji hao wataweza kupata nafasi ya kushiriki kwenye michezo hiyo ya Beijing. Alisema,
"Tuna matumaini kuwa michezo ya Olimpiki ya Beijing itafanyika kwa kufana kabisa kuliko michezo mingine iliyopita!"
|