Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-13 20:11:50    
Maisha ya wafugaji wa kabila la Watibet

cri

Sehemu ya kusini magharibi ya mkoa wa Qinghai, inajulikana kama Chanzo cha Mito Mitatu kutokana na kuwa na vyanzo vya mito mitatu mikubwa ya China ya Changjiang, Huanghe na Lancangjiang. Sehemu hiyo iliyoko katikati ya Uwanda wa Juu wa Qinghai-Tibet ina mito na maziwa mengi, ni chanzo muhimu cha maji nchini China. Lakini katika miaka kadhaa iliyopita, mazingira ya kimaumbile ya sehemu ya vyanzo vya Mito Mitatu yameanza kuathiriwa nashughuli za binadamu. Ili kuhifadhi mazingira, wafugaji wanaohamahama zaidi ya elfu 30 wa kabila la Watibet kwenye sehemu hiyo wamehamishwa na kupewa makazi ya kudumu mijini.

Bw. Nyima mwenye umri wa miaka 38 alikuwa mfugaji wa kuhamahama. Miaka mitatu iliyopita aliuza ng'ombe wake zaidi ya 40, na alihamia kwenye kijiji kipya kilichoko kwenye kitongoji cha mji wa Golmud mkoani Qinghai kutoka kwenye sehemu ya Chanzo cha Mito Mitatu yenye mwinuko wa zaidi ya mita 4500 kutoka usawa wa bahari. Bw. Nyima alisema ikilinganishwa na maisha ya kuhamahama ya zamani, maisha ya sasa ni mazuri sana, alisema,

"Baada ya kuhamia hapa, tunapoumwa na magonjwa tunaweza kupata matibabu hapa hapa kijijini, na tunatumia maji na umeme kwa urahisi. Maisha yetu yameboreshwa sana ikilinganishwa na yale ya zamani."

Bw. Nyima pamoja na baba yake, mke na watoto wake watatu sasa wakaa kwenye nyumba nzuri yenye eneo la mita zaidi ya 70 za mraba, na hivi karibuni wamenunua televisheni. Bw. Nyima aliwaambia waandishi wetu wa habari kuwa, kutokana na kuitikia mwito wa serikali, mwaka 2004 familia yake pamoja na familia nyingine zaidi ya 100 za wafugaji wa kabila la Watibet walihamia kwa hiari kwenye kijiji hicho kipya kutoka sehemu ya Chanzo cha Mito Mitatu waliyoishi kizazi baada ya kizazi, na walipewa nyumba bure na serikali.

Kwa wafugaji kutoka uwanda wa juu, kuhamia mijini kunamaanisha mabadiliko makubwa ya maisha katika pande mbalimbali. Zamani watu hao walijua kufuga wanyama tu, maisha mapya yameletea changamoto kubwa, hata mwanzoni baadhi yao hawakujua kutumia jiko la makaa ya mawe. Serikali ya China ilichukua hatua mbalimbali, ili kuwasadia wafugaji hao kukabiliana na changamoto hiyo. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kuwajengea nyumba. Kijiji kipya kwa wahamiaji kutoka sehemu ya Chanzo cha Mito Mitatu Bw. Nyima anachoishi kina eneo la hekta 35, kwenye kijiji hicho serikali ilijenga nyumba 128, na kila familia ilipewa nyumba yenye eneo la mita zaidi ya 60, aidha shule na hospitali pia zimejengwa kwenye kijiji hicho. Mbali na hayo wahamiaji hao pia walipewa ruzuku na serikali ya China. Ili kuwasaidia watu hao waliokuwa wafugaji kuzoea maisha mapya na kupata uwezo wa kuendesha maisha, serikali ya sehemu hiyo pia iliwapatia mafunzo ya kazi. Kwa mfano Bw. Nyima alijiunga na mafunzo ya kuendesha gari na akawa dereva, alisema,

"Mimi nilijifunza kuendesha gari mwaka jana. Nilinunua gari la mizigo, na sasa ninafanya kazi ya usafirishaji kati ya mji wa Gormud na sehemu ya mto wa Toto. Mbali na hayo nina jumba la Langma, na kila mwaka familia yangu inapata mapato ya Yuan zaidi ya elfu 30."

Jumba la Langma lililotajwa na Bw. Nyima ni jumba la kulipia la kuimba nyimbo na kucheza ngoma. Watu wa kabila la Watibet ni hodari wa kuimba nyimbo na kucheza ngoma. Kutokana na utamaduni huo, wahamiaji hao wengi walianzisha jumba la kutoa huduma za burudani kwa watalii kutoka sehemu za nje, ili kujiongezea mapato. Baba wa Nyima Bw. Sumzhub alihamia kwenye kijiji hicho pamoja na mtoto wake miaka mitatu iliyopita. Mzee huyo aliyeishi kwenye mashamba ya nyasi kwenye uwanda wa juu kwa miaka mingi alipozungumzia maisha ya hivi sasa, aliridhika sana, akisema,

"zamani tulipokuwa uwanda wa juu, tulikuwa tunaendesha maisha kwa kutegemea ufugaji. Baada ya kuhamia hapa, maisha yameboreshwa sana. Zamani tulipopatwa na magonjwa, tulilazimika kusafiri kilomita 70 hadi 80 ili kutibiwa, lakini sasa kuna kituo cha matibabu kwenye kijiji chetu. Mimi wala mtoto wangu Nyima hatujapata fursa ya kusoma shuleni, lakini sasa wajukuu wangu wamepata fursa hiyo, hata wanapanga kusoma hadi vyuo vikuu."

Manufaa mengine kutokana na uhamiaji ni kupata fursa ya kwenda shuleni. Shule ya Chanzo cha Mito Mitatu iko kwenye katikati ya kijiji cha wahamiaji, ujenzi wake ulikamilika mwezi Julai mwaka jana. Watoto wote wa wahamiaji hao mwenye umri wa miaka kati ya 6 na 12 wanasoma shule hiyo. Mtoto wa Bw. Nyima Soinam Gonpo mwenye umri wa miaka nane alisoma kwenye shule hiyo, alisema,

"Zamani sikupata fursa ya kwenda shuleni, sasa ninafurahi sana kupata fursa hiyo. Ninasoma masomo ya lugha ya kichina, lugha ya kitibet na hisabati. Darasa letu ni kubwa sana."

Si watoto wa wahamiaji hao tu, bali wafugaji wengi ambao hawajahama, pia wamewapeleka watoto wao kwenye nyumba za jamaa zao waliohama, ili kuwapatia fursa ya kwenda shule. Kwa wafugaji wengi wa kabila la Watibet, elimu ni sababu muhimu ya kuhama, pia inawaletea matumaini katika siku zijazo. Mkuu wa kijiji cha wahamiaji kutoka sehemu ya Chanzo cha Mito Mitatu Bibi Zhang Xiaowen alisema, kwa shule ya makabila madogo madogo, serikali ya China inatekeleza sera ya kusamehe ada ya masomo na vitabu, na kutoa ruzuku kwa wanafunzi wanaotoka kwenye familia zenye matatizo ya kiuchumi.

Kutokana na hatua za kuhamisha wafugaji na kupunguza ufugaji wa wanyama, kazi za kuhifadhi mazingira kwenye sehemu ya Chanzo cha Mito Mitatu zimepata mafanikio ya awali. Katika miaka kadhaa ijayo, serikali ya China itaendelea kufanya juhudi za kuhifadhi mazingira na kuboresha maisha ya wafugaji wa kabila la Watibet kwenye sehemu hiyo.