Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-14 19:08:49    
Rais Bush wa Marekani kufanya ziara katika nchi tano za Afrika

cri

Rais George Bush wa Marekani anatazamiwa kufanya ziara katika nchi tano za Afrika Benin, Tanzania, Rwanda, Ghana na Liberia kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 21 mwezi huu. Wakati wa ziara yake hiyo, rais Bush atafanya mazungumzo na viongozi wa nchi hizo za Afrika kuhusu kuhimiza mageuzi ya demokrasia, biashara huria na kuharakisha maendeleo ya uchumi wa Bara la Afrika. Vyombo vya habari vya Marekani vimechambua kuwa, katika ziara hiyo rais Bush atatilia mkazo zaidi mapambano dhidi ya umaskini na magonjwa barani Afrika, atatoa mwito wa kuitaka jumuiya ya Kimataifa iongeze fedha za misaada kwa nchi za bara la Afrika kwa ajili ya kinga na tiba ya ugonjwa wa ukimwi na ugonjwa wa malaria, na atatangaza kutoa fedha za msaada za dola za kimarekani milioni 700 kwa ajili ya miradi mbalimbali kwa ajili ya bara la Afrika. Aidha Bw Bush atafuatilia matukio ya kimabavu yaliyotokea barani Afrika, pamoja na jaribio la mapinduzi nchini Chad, na hali ya msukosuko nchini Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Ziara hiyo ya Rais Bush barani Afrika ni ya pili tangu aingie madarakani, na huenda ni ziara ya mara ya mwisho atakayofanya kabla ya kuondoka madarakani mwezi Januari mwaka kesho. Wachambuzi wamedhihirisha kuwa, kujadiliana kati ya Bush na viongozi wa nchi za Afrika kutasaidia kuhimiza ushirikiano kati ya pande mbili, na kutayasaidia makampuni ya Marekani yapate nafasi katika hali ya hivi sasa ambayo nchi kubwa duniani zinafuatilia zaidi soko la Afrika.

Mjumbe msaidizi wa Marekani aliyeshughulikia mambo ya Afrika Bibi Rosa Whitaker alidhihirisha kuwa, ziara ya Bw Bush barani Afrika hii imeonesha kuwa serikali ya Marekani imeacha "sera isiyo na uhalisi" kwa Afrika na "mambo ya kidiplomasia yasiyozingatia hali halisi ya barani Afrika", badala yake imechukua sera endelevu inayotekelezwa kwa hatua mfululizo kwa Afrika. Bibi Whitaker anaona kuwa, kwa kuwa nchini Marekani kuna watu wengi wanaounga mkono maendeleo ya Afrika, Bw Bush akiwa rais atakayeondoka madarakani, huenda atachukua hatua kubwa katika sera ya Marekani kwa Afrika, na hii ni fursa inayosaidia maendeleo kwa nchi mbalimbali za Afrika. Ndiyo maana, ziara hiyo ya Bush huenda itakuwa sehemu moja ya mali ya urithi ya kisiasa atakayoacha rais Bush, ambayo itakuwa na athari kwa rais atakayemfuata wakati wa kutunga sera kwa Afrika.

Lakini baadhi ya wasomi wa Afrika wana maoni yao tofauti. Tovuti maarufu ya Afrika kwenye mtandao wa internet "allafrica.com" ilitoa makala ikisema, Bush ana makusudi ya kuonesha kuwa Marekani inashirikiana bega kwa bega na Afrika katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi na magonjwa mengine. Makala hiyo ilidhihirisha kuwa, ingawa msaada wa serikali ya Bush kwa Afrika ni mkubwa zaidi kuliko ule uliotolewa na serikali ya Marekani ya awamu iliyopita, lakini msaada uliotolewa na serikali ya Bush bado unaelekea kwa makundi yenye imani inayofanana na ile ya Marekani, ambao haufuatilii maslahi ya makundi mbalimbali. Makala hiyo inaona kuwa, wazo la serikali ya Marekani la "kuzibadilisha baadhi ya nchi ziwe ati nchi za demokrasia" bado halibadiliki; na serikali Bush inashikilia msimamo imara kuhusu Suala la kuongezeka kwa joto kote duniani, yote hayo hayataifanya ziara ya Bush barani Afrika iisaidie zaidi Marekani kuboresha sura yake katika dunia nzima.

Zaidi ya hayo, wasomaji wa tovuti kwenye mtandao wa internet walidhihirisha kuwa, rais wa Marekani wa awamu iliyopita Bw. Clinton aliwahi kuitembelea Afrika mara nyingi, hiyo Bush amechelewa kupanga ziara yake barani Afrika, hata matokeo ya ziara hiyo pia ni vigumu kusaidia siku zake za mbele. Kwa kuwa tangu Bush ashike madaraka, alikuwa na pilikapilika katika vita dhidi ya ugaidi, na sera yake ya kidiplomasia ilipuuza zaidi bara la Afrika, hivyo watu wengi wanafuatilia kama kweli ziara yake hiyo barani Afrika itakuwa na mafanikio.