Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-14 19:30:57    
Mradi wa Hongfeng unaowasaidia wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu wenye matatizo ya kiuchumi

cri

   

Leo tunawaletea maelezo kuhusu mradi unaotekelezwa na shirikisho la wanawake la mkoa wa Shanxi kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu wenye matatizo ya kiuchumi.

Kupata elimu ya ngazi ya juu ni ndoto ya watu wengi. Lakini wanafunzi kutoka kwenye familia zenye matatizo ya kiuchumi hawawezi kumudu gharama kubwa za masomo kwenye vyuo vikuu. Ili kuwasaidia wanafunzi hao, China ilichukua hatua mbalimbali kama vile kuondoa baadhi ya ada, na kutoa mikopo kwa wanafunzi hao. Na mikoa na miji kadhaa ya China pia inatoa misaada kwa wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu kutokana na hali zao.

Mkurugenzi wa ofisi ya mradi wa Hongfeng wa shirikisho la wanawake la mkoa wa Shanxi Bibi Ban Li alisema,

"Lengo kubwa ni kuwasaidia wanafunzi wa kike wa vyuo vikuu wanaotoka kwenye familia zenye matatizo ya kiuchumi wapate haki ya kupata elimu ya ngazi ya juu. Njia hii inawasaidia watu wenye matatizo ya kiuchumi kwa njia ya elimu."

Mkoa wa Shanxi ni mmoja kati ya mikoa iliyoko nyuma kiuchumi nchini China. Mwaka 1996 mradi huo ulipoanzishwa, theluthi mbili ya wilaya za mkoa huo zilikuwa wilaya zenye matatizo ya kiuchumi. Ada ya vyuo vikuu ilikuwa ni tatizo kubwa kwa familia za mkoa huo, hasa familia za vijijini.

Tangu mradi wa Hongfeng uanzishwe, mradi huo umesaidia wanafunzi wa kike zaidi elfu 2, na fedha zilizotolewa zimefikia Yuan milioni 8.6. Fedha hizo zinatoka kwa mashirika ya kimataifa, mfuko wa elimu na wafadhili wa kawaida. Bibi Ban Li alisema,

"mradi wa Hongfeng ulianzishwa kutokana na juhudi na upendo wa watu wa kawaida. Mradi huo unawahamasisha watu wengi zaidi na kuaminiwa zaidi na watu wa jamii."

   

Wakati wa kutekeleza mradi wa Hongfeng, mambo mengi ya kuvutia yalitokea. Bw. Zhang Liren alimsaidia kwa muda mrefu mwanafunzi mmoja wa kike anayetoka kwenye familia yenye matatizo ya kiuchumi. lakini alipata ugonjwa wa saratani na mke wake alipunguzwa kazini. Alihitaji fedha nyingi kwa ajili ya matibabu. Ofisi ya mradi wa Hongfeng ilimshawishi aache kumsaidia mwanafunzi huyo, lakini alikataa na kuendelea kuchangia hadi alipofariki dunia. Bw. Zhang Liren alisifiwa kuwa ni "balozi wa upendo" wa mradi wa Hongfeng.

Bw. Ban Li alisema, mradi huo siyo tu unatoa ada ya vyuo vikuu kwa wanafunzi wa kike, bali pia unatoa msaada wa kisaikolojia ili kuwasaidia kuwa na mtizamo sahihi kuhusu maisha. Kutokana na sera ya mradi huo, kama hali ya kiuchumi ni nzuri, mwanafunzi aliyepata msaada pia atapaswa kumsaidia mwanafunzi mwingine katika miaka mitano baada ya kuhitimu. Hivi sasa, wanafunzi zaidi ya 800 kati ya wanafunzi waliopata msaada wamehitimu na kupata ajira. Ingawa wengi kati yao hawana mapato makubwa, lakini wameanza kuchangia na kuwasiadia wengine.

Katika miaka 12 iliyopita tangu mradi huo uanzishwe, mradi huo umetoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya sehemu ya magharibi mwa China na maendeleo ya shughuli za wanawake. Mradi huo umekuwa njia yenye ufanisi katika sehemu zenye matatizo ya kiuchumi ya kuhamasisha nguvu ya jamii na kutegemea rasilimali ya sehemu hiyo, ili kuwasaidia wanawake kutimiza haki za kupata elimu ya ngazi ya juu. Mwaka 2006, mradi wa Hongfeng ulisifiwa kuwa ni mradi wa vielelezo unaohusu maslahi ya umma ya jamii.

Bw. Ban Li alipozungumzia maendeleo ya mradi huo alisema,

"Katika miaka ya hivi karibuni, tulifanya utafiti katika uvumbuzi wa mfumo wa mradi huo. na katika siku za usoni tutaendelea kukamilisha taratibu za mradi huo kuhusu kukusanya fedha, kutoa huduma za kutafuta ajira, na utaratibu wa kulipa, ili kutoa huduma nzuri zaidi kwa jamii."