Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-15 17:21:51    
Ni vigumu kwa Lebanon kuondokana na hali ngumu ya kisiasa

cri

Waungaji mkono elfu kumi kadhaa wa serikali ya Lebanon tarehe 14 walifanya mkutano wa hadhara kwenye katika uwanja wa mashujaa waliouawa huko Beirut, ili kumkumbuka waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Rafik al-Hariri aliyeuawa miaka mitatu iliyopita. Waziri mkuu wa Lebanon Bw. Fouad Siniora, baadhi ya mawaziri na wabunge wanaounga mkono serikali walihudhuria mkutano huo. Mtoto wa Rafik Hariri, Bw. Saad al-Hariri, ambaye pia ni kiongozi wa kundi lenye watu wengi bungeni na kiongozi wa kundi la "Future Movement", alitoa hotuba kwenye mkutano huo akisisitiza kuwa, bila kujali watatoa mchango mkubwa namna gani, wataunga mkono kithabiti kuunda mahakama ya kimataifa ya kuchunguza kesi ya kuuawa kwa waziri mkuu wa zamani Bw Rafik al-Hariri, ili kumwadhibu muuaji. Alisema anaunga mkono kumchagua kwa amirijeshi wa jeshi la Lebanon Bw. Michel Sulaiman kuwa rais mpya wa Lebanon, ili kufungua ukurasa mpya wa maafikiano, mazungumzo na ushirikiano wa Lebanon.

Siku hiyo hiyo chama cha Hezbollah cha Lebanon, pia kilifanya mazishi ya kamanda mwandamizi wa chama hicho Bw. Imad Mughnieh katika sehemu ya kusini ya Beirut, aliyeuawa huko Damascus tarehe 12. Katibu mkuu wa chama hicho Bw. Hassan Nasrallah alisema, Israel imefanya makosa makubwa kumuua Mughnieh, kwa kuwa itasababisha "maangamizi" kwa Israel. Pia alikikosoa kundi lenye watu wengi bungeni kuufanya mkutano wa kukumbuka miaka mitatu ya kuuawa kwa Hariri kuwa mkutano wa kuyatukana na kuyalaani makundi ya upinzani.

Wachambuzi wanaona kuwa, bado Lebanon inakabiliwa na masuala mengi magumu katika kuondokana na hali ngumu ya kisiasa. Kwanza, bado ni vigumu kwa kundi lenye watu wengi bungeni na makundi ya upinzani kufikia makubaliano kuhusu uchaguzi wa rais. Kutokana na mgongano mkubwa kati ya pande hizo mbili, uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 25 mwezi Septemba mwaka jana ulilazimishwa kuahirishwa mara 14. Hivyo baada ya kipindi cha madaraka ya rais wa zamani wa Lebanon Bw. Emile Lahoud kwisha tarehe 24 mwezi Novemba mwaka jana, nafasi ya rais wa Lebanon iko wazi. Ingawa baada ya pande nyingi kufanya usuluhishi, kundi lenye watu wengi bungeni lilikubali kumteua Bw. Sulaiman aliyechaguliwa na makundi ya upinzani kuwa rais mpya wa Lebanon, lakini pande hizo mbili zina migongano mingi zaidi katika masuala ya kuunda serikali mpya, mgawanyo wa viti vya bunge na marekebisho ya katiba. Hivi sasa usuluhishi unaoongozwa na Umoja wa Nchi za Kiarabu bado unaendelea, ili kuzihimiza pande mbalimbali za Lebanon kufikia makubaliano kabla ya kufanyika kwa mkutano wa wakuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu.

Pili, matukio mengi ya mauaji ya kisirisiri na migogoro ya umwagaji damu inaifanya hali ya siasa ya Lebanon kuwa ya utatanishi zaidi. Baada ya kuuawa kwa Hariri, nguvu ya kundi lenye watu wengi bungeni ya Lebanon inayopinga Syria imepungua, na wapinzani kujitoa kutoka serikali kunadhoofisha vibaya uwezo wa utendaji wa serikali upungue. Viongozi wengi wa jeshi la Lebanon na jeshi la ulinzi wa amani waliuawa katika miezi miwili iliyopita. Lakini bado haijulikani nani anaongoza mambo hayo.

Aidha, kazi ya kuunda mahakama ya kimataifa ya kuchunguza kesi ya kuuawa kwa Hariri inaendelea polepole. Tarehe 30 Mei mwaka jana, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio kuunda mahakama maalum ya kimataifa ili kuchunguza tukio hilo. Waziri mkuu wa Lebanon Bw. Siniora na kundi lenye watu wengi bungeni kinakaribisha azimio hilo, lakini rais Lahoud wa wakati ule, spika wa bunge Bw. Nabeeh Bari na chama cha Hezbollah kilitoa taarifa kikisema kuwa, azimio hilo ni uvamizi dhidi ya mamlaka ya Lebanon. Tangu mahakama hiyo ianzishwe mwezi Juni mwaka jana, utendaji wake unaendelea polepole. Ripoti iliyotolewa na kamati ya kimataifa ya uchunguzi wa kesi ya kuuawa kwa Hariri inasema, hali mbaya ya usalama nchini Lebanon imeathiri vibaya maendeleo ya kazi ya uchunguzi.

Tarehe 14 ofisi ya katibu ya Umoja wa Nchi za Kiarabu ilitoa taarifa ikiwataka watu wote wa Lebanon waimarisha ushirikiano, ili kuondokana na hali ngumu.