Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-15 18:09:32    
Mawasiliano na ushirikiano kati ya China na Afrika

cri

Balozi wa China nchini Sierra Leone Bw. Cheng Wenju na waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa wa Sierra Leone Bi. Bangula, mwezi Januari huko Freetown walisaini makubaliano ya ushirikiano wa kiteknolojia na kiuchumi kuhusu China kuipatia serikali ya Sierra Leone mkopo usio na riba.

Kwenye sherehe ya kusaini makubaliano hayo, Bi. Bangula aliishukuru serikali ya China kwa niaba ya rais Ernest Koroma na serikali ya Sierra Leone, akisema Sierra Leone itatumia mkopo huo kwa msingi wa makubaliano kati ya nchi hizo mbili, ili kuufanya utoe mchango kwa ukarabati wa jamii na uchumi nchini Sierra Leone. Bi. Bangula alisisitiza kuwa Sierra Leone inatilia maanani uhusiano kati yake na China, na inaichukulia China kuwa ni mwenzi wake mwaminifu wa maendeleo. Alisema Sierra Leone itaendelea kushikilia sera ya kuwepo kwa China moja bila kulegalega, na haitakuwa na uhusiano wowote wa kiserikali na Taiwan.

Bw. Cheng Wenju alisema, China imetoa mkopo usio na riba kwa Sierra Leone kwa mara nyingine, hii inaonesha kuwa serikali ya China inatilia maanani kuimarisha na kuendeleza uhusiano kati yake na Sierra Leone, na inaelewa na kumwunga mkono rais Koroma na serikali ya Sierra Leone kutokana na juhudi zao za ukarabati wa jamii na uchumi. China ina matumaini kuwa nchi hizo mbili zitashirikiana kufanya juhudi, na kuhimiza maendeleo ya uhusiano kati yao.

Habari nyingine zinasema, shirikisho la makampuni ya China lilianzishwa hivi karibuni nchini Ghana. Balozi wa China nchini Ghana Bw. Yu Wenzhe na wawakilishi karibu 300 wa makampuni ya China nchini Ghana walihudhuria mkutano wa kuanzishwa kwa shirikisho hilo. Bw. Yu Wenzhe alitoa hotuba akiyahimiza makampuni ya China nchini Ghana yaendelezwe vizuri na kwa kasi. Alisema ubalozi wa China nchini Ghana utazingatia na kuunga mkono kazi ya shirikisho hilo. Maneja wa kampuni ya umeme wa maji ya China Bw. Xie Dahu alichaguliwa kuwa mkurugenzi wa shirikisho hilo. Wajumbe waliohudhuria mkutano huo waliona kuwa kuanzishwa kwa shirikisho hilo kutasaidia usimamizi wa kampuni, kuimarisha mshikamano wa wanachama wa shirikisho hilo, kuepusha ushindani mbaya, kulinda maslahi ya haki ya kampuni, kuweka mfano mzuri wa kampuni za China, na kuhimiza maendeleo ya uchumi na biashara kati ya China na Ghana. Shirikisho la biashara la makampuni ya China nchini Ghana hivi sasa lina makampuni wanachama zaidi ya 40.

Balozi wa China nchini Senegal Bw. Lu Shaye na waziri wa utamaduni na mali ya urithi wa Senegal Bw. Mame Birame Diouf mwezi Januari huko Dakar walisaini makubaliano ya utamaduni kati ya serikali za China na Senegal. Balozi mdogo wa China nchini Senegal anayeshughulikia mambo ya utamaduni Bw. She Mingyuan alisema, tangu tarehe 25 mwezi Oktoba mwaka 2005 China na Senegal ziliporudisha uhusiano wa kibalozi, mawasiliano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika mambo ya utamaduni umeanza kwa pande zote. Mwezi Oktoba mwaka 2007, kutokana na mwaliko kikundi cha sarakasi cha Tianjin kilikwenda Senegal kuonesha sarakasi, na kufurahiwa sana na watazamaji wa Senegal. Mwezi Desemba mwaka 2007, ujumbe wa utamaduni wa serikali ya China ulioongozwa na naibu waziri wa utamaduni wa China Bw. Chang Keren ulifanya ziara nchini Senegal, hii ilizidisha maelewano na urafiki kati ya maofisa wa utamaduni wa nchi hizo mbili, na kuhimiza mawasiliano ya utamaduni kati ya nchi hizo mbili.

Bw. She Mingyuan alisema, kusainiwa kwa makubaliano hayo kutatoa uhakikisho wa kisheria kwa mawasiliano na ushirikiano kati ya China na Senegal katika mambo ya utamaduni, hakika kutahimiza zaidi mawasiliano na ushirikiano huo, na kuhimiza kwa pande zote maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Mwezi Januari zana za kilimo zenye dola za kimarekani zaidi ya milioni moja zilikabidhiwa na China kwa Benin. Balozi wa China nchini Benin Bi. Li Peifen alisema, mashine hizo ni msaada wenye thamani kubwa kabisa katika historia ya ushirikiano wa kilimo kati ya China na Benin, ambazo pia ni matokeo muhimu ya ziara alizofanya rais Thomas Boni Yayi wa Benin nchini China mwaka 2006. Alisema serikali ya China inaunga mkono pendekezo lililotolewa na rais Yayi kuhusu kutimiza matumizi ya mashine kwenye kilimo, na ina matumaini kuwa mashine hizo zitatumika mapema na kuwanufaisha watu wa huko. Rais Yayi aliishukuru China kwa misaada ya muda mrefu, alizitaka nchi hizo mbili zishirikiane kufanya juhudi ili kuimarisha uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati yao siku hadi siku.

Habari nyingine zimesema, makubaliano ya ushirikiano kuhusu China kuisaidia Cameroon kujenga vituo vya vielelezo vya ufundi wa kilimo yalisainiwa mwezi Januari huko Yaoundé. Balozi wa China nchini Cameroon Bw. Huang Changqing na naibu waziri mkuu wa Cameroon ambaye pia ni waziri wa kilimo na maendeleo ya vijiji Bw. Jean Nkuete walisaini makubaliano hayo kwa niaba ya serikali za nchi hizo mbili.

Bw. Huang Changqing alisema, wakati wa kuadhimisha mwaka mmoja tangu rais Hu Jintao wa China afanye ziara nchini Cameroon, kusaini makubaliano hayo kwa nchi hizo mbili kuna maana muhimu. Makubaliano hayo ya kiserikali ni ya kwanza kuhusu China kusaidia kuanzisha vituo vya vielelezo vya ufundi wa kilimo barani Afrika, amezitaka pande hizo mbili zishirikiane kufanya juhudi ili ujenzi wa kituo hicho ukamilike mapema, na kuwanufaisha wananchi wa Cameroon.

Bw. Nkuete aliishukuru China kwa kuisaidia Cameroon kujenga kituo cha kielelezo cha wa kilimo, alisema kituo hicho kitaisaidia Cameroon kujifunza ufundi wa ufanisi na uzoefu wa usimamizi wa maendeleo ya kilimo ya China, kitawasaidia wakulima wa Cameroon kuinua kiwango cha uzalishaji na maisha, na ni muhimu kwa maendeleo ya kilimo ya Cameroon na utimizaji wa utoaji wa vyakula. Bw. Nkuete alisema anaamini kuwa mustakabali wa ushirikiano wa kilimo kati ya nchi hizo mbili ni mzuri.

Kuzisaida nchi za Afrika kujenga vituo vya vielelezo vya ufundi wa kilimo ni moja ya hatua alizoahidi rais Hu Jintao kwenye mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka 2006 hapa Beijing. Cameroon itatoa ardhi yenye hekta 100 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, na China itatuma wataalamu kutoa mafunzo ya usimamizi na ufundi. Serikali za China na Cameroon zitachagua pamoja kampuni moja ya China kushughulikia ujenzi wa kituo hicho, na uendeshaji na usimamizi wa kituo hicho katika miaka kumi ijayo baada ya kuanzishwa kwa kituo hicho, ili kuhakikisha maendeleo endelevu ya kituo hicho.