Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-18 15:46:51    
Sanaa za asili za makabila madogo madogo zahifadhiwa nchini China

cri

Nchini China kuna makabila madogo madogo 55 ambayo watu wake wanachukua asilimia 8 ya watu wote wa China. Watu wa makabila hayo ni hodari wa kueleza maisha yao kwa kuimba na kucheza ngoma. Wasikilizaji wengi wa nchi za nje wanafurahia sanaa za jadi za makabila hayo ya China na wanataka kufahamu jinsi sanaa hizo zinavyotunzwa na kurithishwa kwa vizazi vya baadaye.

Mliosikia ni wimbo ulioimbwa na mwimbaji mashuhuri wa kabila la Watibet, Bi. Zongyong Zhuona. Huu ni wimbo wa jadi unaoitwa "Binti wa Mlima wa Theluji". Mwaimbaji huyo pia ni mjumbe wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China, alisema anafurahi sana kuona kwamba sanaa za jadi za makabila madogo madogo zinathaminiwa sana na serikali na kuungwa mkono na jamii kwa kuzipatia sanaa hizo nafasi nyingi za maonesho. Sanaa za jadi za makabila madogo madogo mara kwa mara zinaoneshwa katika maonesho makubwa ya kitaifa nchini China, na sanaa hizo zimerekodiwa kwenye CD na zinanunuliwa sana katika maduka ya audio na video. Bi. Zongyong Zhuona alisema,

"Ninaridhika na jinsi serikali inavyothamini sanaa zetu za jadi za makabila madogo madogo, hivi sasa nyimbo zetu za jadi zimewekwa katika mashindano sawa na nyimbo za aina nyingine za kisasa za Kimagharibi na za kitaifa. Nimekuwa mjumbe wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China kwa miaka kadhaa, niliwahi kutoa mapendekezo ya kuthamini na kutunza sanaa za asili za makabila madogo madogo."

Bi. Zongyong Zhuona anaona kuwa sanaa za jadi za makabila madogo madogo ni lazima zitunzwe na ziinuliwe, na kusema kwamba waimbaji wa makabila madogo madogo ni lazima wafundishwe kisayansi namna ya kuimba. Alisema,

"Licha ya kuhifadhi na kurithisha, sanaa za jadi za makabila madogo madogo ni lazima ziinuliwe na ziende na wakati. Kwa mfano, waimbaji wa makabila hayo wafundishwe namna ya kuimba kwa kutoa sauti kisayansi. Nyimbo zikiimbwa kisayansi zitakuwa za kuvutia zaidi wasikilizaji wa nchini na hata duniani."

Bi. Zongyong Zhuona ni mwimbaji aliyefundishwa kuimba kisayansi, aliwahi kupata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Muziki cha Shanghai. Sauti yake baada ya kufundishwa imebadilika kuwa nene na inasikika mbali zaidi, na uimbaji wake umekuwa wa kikabila zaidi, waimbaji wengi wanamfuata na kumwomba awafundishe. Alisema,

"Ninataka sana kuanzisha shule ya kufundisha kuimba nyimbo za makabila madogo madogo, na kupokea wanafunzi kutoka makabila madogo madogo 26 yaliyoko mkoani Yunnan, kama ningeweza kumfanya mwimbaji mmoja kutoka kila kabila awe hodari, mafanikio yangu yatakuwa makubwa."

Mliosikia ni utenzi wa "Shujaa Gesar" wa Tibet. Huo ni utenzimrefu kabisa duniani uliotungwa na Watibet, unaeleza na kusifu maisha ya shujaa Gesar. Utenzi huo unaimbwa kwa miaka mingi miongoni mwa Watibet. Utenzi huo licha ya kuwa na thamani kubwa katika fasihi, historia, jiografia, pia una thamani kubwa kwa ajili ya utafiti wa mila na desturi za Watibet.

Mkoa wa Qinghai uliopo kaskazini magharibi mwa China ni mkoa wanakoishi Watibet wengi na pia ni mahali alipoishi shujaa Gesar, wazee wanaoweza kuimba utenzi huo wengi wanaishi katika mkoa huo, lakini kadiri wazee hao wanavyozidi kufariki dunia ndivyo hali ya kukosa watu wenye uwezo wa kuimba utenzi huo inavyozidi kuwa mbaya.

Ili kuhifadhi sanaa za Kitibet, mkoani Tibet kimeanzishwa kituo cha utafiti wa utamaduni wa Kitibet. Mkurugenzi wa kituo hicho ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China Bw. Dong Norde amekusanya na kuhifadhi utenzi wa shujaa Gesar kwa miaka mingi. Alisema,

"Tumegundua wasanii 50 wanaoweza kuimba utenzi wa shujaa Gesar, kati yao watu 30 ni mashuhuri. Tumerekodi sauti zao na tumekusanya vitabu vya utenzi huo vilivyonukuliwa kwa mikono."

Kuhusu mafanikio hayo Bw. Dong Norde alisema,

"Serikali imetenga fedha nyingi katika kuhifadhi, kukusanya na kurithisha utamaduni wa kikabila. Utenzi wa shujaa Gesar umeorodheshwa kwenye orodha ya urithi wa utamaduni usioonekana wa China."

Kabila la Wamongolia lililopo kaskazini mashariki mwa China ni kabila hodari kwa kuimba na kucheza ngoma. Mtindo wa nyimbo zao unaokokota sauti ni johari katika hazina ya muziki duniani, unasifiwa kama ni ua lisilonyauka siku zote. Mjumbe wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China ambaye pia ni mwimbaji mashuhuri wa kabila la Wamongolia Bi. Dodoma alisema,

"Serikali imefanya kazi nyingi katika juhudi za kuhifadhi utamaduni wa jadi wa makabila madogo madogo. Mtindo wa nyimbo za kabila la Wamongolia zinazoimbwa kwa kukokoteza sauti umeorodheshwa na UNESCO kwenye orodha ya urithi wa utamaduni duniani. Mimi ni mwimbaji wa kabila la Wamongolia ninawajibika kuendeleza mtindo huo."

Bi. Dedema anaona kuwa vijana wa siku hizi wanapendelea zaidi muziki wa kisasa na kupuuza muziki wa makabila yao, kwa hiyo alianzisha shule katika mji mkuu wa mkoa wa Mongolia ya Ndani, Huhhot, kuwafundisha watoto wa kabila lake, lakini juhudi za mtu mmoja zina kikomo chake, anapendekeza kuanzisha semina na makongamano katika shule za sekondari na vyuo vikuu kwa lengo la kuwarithisha vijana sanaa na utamaduni ulio bora wa kikabila.

Bw. Wang Sidai wa Mkoa wa Yunnan naye ni mjumbe wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China ambaye pia ni naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Makabila Madogo Madogo mkoani Yunnan. Mkoani humo wanaishi watu wa makabila 25 kati ya makabila yote 56 ya China, kuanzia mwaka 1994 aliandaa wasanii vijana wengi wa makabila madogo madogo. Alisema,

"Njia nzuri ya kuhifadhi utamaduni wetu wa jadi ni kuingiza utamaduni huo kwenye elimu ya kufundisha katika shule hasa vyuo vikuu na kuwafahamisha wanafunzi wetu thamani ya utamaduni huo wenye historia ndefu."

Kila kabila lina utamaduni wake, na tamaduni tofauti za makabila zimeifanya dunia yetu iwe na rangi mbalimbali za kupendeza. Juhudi tunazozifanya leo ni kwa ajili ya kuifanya dunia ya kesho iwe ya kupendeza zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2008-02-18