Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-18 16:05:27    
Wafanyabiashara wageni wa mambo ya utalii wavutiwa na Sanya

cri

Mji wa Sanya wa mkoa wa Hainan, ulioko kwenye sehemu ya kusini ya China ni maarufu katika mambo ya utalii, kisiwa hicho cha sehemu ya joto chenye mwangaza mzuri wa jua, hewa safi na fukwe zenye mchanga mweupe laini, licha ya kuvutia idadi kubwa ya watalii wa nchini China na kutoka nchi za nje, pia unawavutia wafanyabiashara wengi kwenda huko kushughulikia mambo ya utalii.

Bw. Andre ambaye ni mfanyabiashara kutoka Russia, amefungua shirika la utalii katika mji wa Sanya, na sasa anajulikana sana kwenye sehemu hiyo. Kutokana na mchango aliotoa kwa soko la utalii la mkoa wa Hainan, ametunukiwa sifa ya juu kabisa ya "tuzo la kisiwa cha minazi" na serikali ya mkoa wa Hainan. Bwana Andre kila anapotaja mkoa wa Hainan na mji wa Sanya, huusifu sana mkoa huo. Bw. Andre anajua sana Kichina, alisema kwa Kichina,

"Hainan inachukua nafasi ya kwanza katika mambo kadhaa: Kwanza, hali ya hewa. Ni mji wa Sanya peke yake katika nchi nzima ya China, ambayo ina hali ya hewa ya sehemu ya joto. Pili, Hainan ni mkoa pekee wenye idadi kidogo ya watu nchini China, watu wa huko wanaishi kwa raha bila msongamano wa watu kama miji mingine. Tatu, mazingira ya asili ya huko yamehifadhiwa vizuri, hakuna vitu vingi vinachochafua mazingira. Hainan ni eneo maalumu la kiuchumi, linatekeleza sera nafuu, hivyo linawavutia sana watalii pamoja na wanaviwanda."

Bw. Andre aliyehitimu masomo yake katika chuo kikuu cha Moscow, mwaka 1994 baada ya kusoma kitabu kimoja kinachoeleza mji wa Sanya wa mkoa wa Hainan, yeye na marafiki zake walitembelea huko. Wakati ule, sekta ya utalii ya Sanya ilikuwa bado iko katika kipindi cha mwanzo, watalii waliotembelea mji huo walikuwa wachache sana, lakini mandhari nzuri ya huko ilimvutia sana, akawa na wazo la kujishughulisha mambo ya utalii huko. Hatimaye alifungua shirika la utalii. Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya watalii walioitembelea Hainan, inaongezeka kwa zaidi ya 90% kila mwaka, Hainan imekuwa moja ya sehemu chache zenye mvuto mkubwa kwa watu wa Russia. Bw. Andre alisema, pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watalii wa Russia, biashara ya shirika lake la utalii pia imekuwa nzuri mwaka hadi mwaka:

Hivi sasa tunapata watalii wa Russia zaidi ya 1,000 kwa mwezi. Soko la utalii la Hainan linapata maendeleo ya kasi, ninachosema hapa ni kuhusu soko la watalii waliotoka Russia peke yake."

Bw. Andre alisema, idadi ya watalii wanaotoka Russia na kutembelea Sanya katika mwaka 2007, Ilikadiriwa kuzidi laki 1.5, Russia huenda itabadilika kuwa nchi inayochukua nafasi ya kwanza kwa wingi wa watu wanaoitembelea Hainan, hii ni habari nzuri. Ili kukidhi mahitaji ya watalii, hivi sasa anaendelea kuboresha kazi za shirika lake, na kuongeza shughuli katika utalii.

"Siyo tu warussia wanapenda kuota jua na kuogelea, bali pia wanataka kupata ufahamu mwingi kuhusu China, hivyo, licha ya kupanga mambo ya burudani, tunapanga shughuli za kuwafahamisha utamaduni wa China. Kwa mfano, tumeanzisha mashindano kuhusu mambo maalumu ya China, yakiwa ni pamoja na kutengeneza aina ya chakula cha kichina, Jiaozi au kujiburudisha kwa chai ya kichina, mambo kama hayo yanapendwa sana na watalii."

Hivi sasa, matarajio makubwa ya Bw. Andre ni kujenga jumba la makumbusho ya utamaduni wa China katika mji wa Sanya ili kuwawezesha warussia wengi waifahamu China na mkoa wa Hainan.

Bw. Lobin ni mwingereza, na ni maneja mkuu wa hoteli ya Crowne Holiday Inn ya Huayu, hoteli hiyo ya hali ya juu iko kwenye ghuba ya Yalong, ambayo ni sehemu maarufu kwenye mji wa Sanya. Katika miaka ya hivi karibuni, hoteli hiyo ya Huayu inawavutia watalii wengi kwa mambo ya starehe na mapumziko, ambapo watalii licha ya kuweza kuburudika kwenye ufukwe wa bahari, wanapata huduma ya kiwango cha juu hotelini.

Bw. Lobin alisema, hoteli hiyo ni hoteli nzuri zaidi aliyoiona katika kazi zake zaidi ya miaka 20, anafurahi sana kwa kuweza kupata nafasi hiyo ya kazi.

"Uzuri kabisa wa usanifu wa hoteli hiyo uko sehemu ya nje, hoteli hiyo inaonekana ni ya mtindo wa jadi wa China, lakini ndani ni zana za kisasa kabisa. Hoteli hiyo siyo tu ni kwa ajili ya kupumzika, tena hoteli hiyo inaonekana kama mji mmoja mdogo, kuna ukumbi wa chakula, baa, sehemu ya kuuza bidhaa, mambo ya starehe na madaktari, watalii wanaoishi hapa, wanaweza kuridhika kabisa."

Bw. Lobin alisema, kwa watalii wengi wanaotoka nchi za Ulaya na Marekani, Hainan bado ni sehemu ngeni, tutawafahamisha watu wa nchi mbalimbali kuhusu mvuto wa kipekee wa Hainan katika mambo ya mapumziko, yeye binafsi anajitahidi sana pia katika shughuli hizo.

Hivi karibuni hoteli ya Crowne Holiday Inn ya Huayu ilichaguliwa kuwa hoteli ya kufanya maandalizi kwa shindano la Mrembo wa dunia la mwaka 2007, warembo wa nchi mbalimbali waliokuja kushiriki kwenye fainali, walisifu sana huduma za hoteli hiyo pamoja na mandhari nzuri ya kimaumbile ya kisiwa cha Hainan. Mrembo kutoka Mongolia Aoyungerile alisema,

"Kila kitu cha hapa ni kizuri! Mandhari nzuri ya kimaumbile, wasichana wazuri pamoja na hoteli nzuri. Ni mara ya kwanza kufika hapa, nimekuwa na matarajio makubwa kuhusu mji wa Sanya wa mkoa wa Hainan!"

Kisiwani Hainan, licha ya kupata huduma nzuri, watalii pia wanaweza kuonja chakula cha kigeni.

Katika mji wa Sanya, kuna mkahawa mmoja wa chakula cha nchi za magharibi unaoitwa "Mediterranean", m-italia Bw. Mobai ni mwendeshaji wa mkahawa huo. Mara tu baada ya kuingia kwenye mkahawa huo, mtu ataona kama yuko katika sehemu ya Mediterranean. Bw. Mobai anajua sana kuongea kichina, alisema alijitahidi kadiri awezavyo wakati wa kujenga mgahawa huo, akisema,

"Vitu vyote, vikiwa ni pamoja na viti, meza, milango na taa, nilisanifu mwenyewe. Kwa sababu watu wa hapa wanapenda mtindo wa kawaida. Wateja wao wanapenda mtindo pamoja na vitoweo vya mkahawa huo, piza, nyama za kuokwa pamoja na tambi za Italia za hapa zote ni zenye jadi ya asili ya Ulaya."

Mwaka 2003, kutokana na mapendekezo ya marafiki zake za China, Bw. Mobai alijiuzulu kazi yake ya profesa na alifika kwenye mji wa Sanya kufungua mkahawa.

Sasa ni miaka kadhaa imepita, Bw. Mobai anazidi kuipenda Sanya kadiri miaka inavyopita. Anamhudumia vizuri kila mteja wake, na aliwaeleza kuhusu uzuri mbalimbali wa Sanya. Alisema watalii waliofika China kutoka mbali, baada ya kutembelea mabaki ya kiutamaduni, kama vile, ukuta mkuu, majumba ya wafalme ya zamani na njia ya hariri, wanafika Sanya kuburudishwa na mandhari ya msitu wa minazi na bahari kubwa, hapo safari yao inakamilika vizuri.

Mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, si Sanya tu, hata katika mkoa mzima wa Hainan, kuna wafanyabiashara wa sekta ya utalii wa duniani wanaojiendeleza katika mambo ya utalii. Akili na juhudi zao zimechangia maendeleo ya sekta ya utalii na kuhimiza sekta ya utalii ya Hainan kuungana na dunia.

Mkurugenzi wa idara ya utalii ya mkoa wa Hainan, Bw. Zhang Qi alisema, sekta ya utalii ya Hainan itafungua zaidi mlango na kuwakaribisha wafanyabiashara wengi zaidi wa sekta ya utalii wa duniani.

Idhaa ya kiswahili 2008-02-18