Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-19 17:30:10    
Barua 0210

cri
Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Mbarak M.Abucheri kwa barua yake ya kutueleza usikivu wake wa matangazo yetu kuhusu Mkutano mkuu wa 17 wa Chama cha kikomunisti cha China wa mwaka jana. Kutokana maelezo yake tunaona yeye kweli alisikiliza kwa makini sana matangazo yetu, hii inatutia moyo wa kuchapa kazi zaidi kwa ajili ya kuwahudumia wasikilizaji wetu.

Na msikilizaji wetu wa Kenya ambaye hakuandika jina lake ametuletea barua inayozungumzia jinsi ya kuboresha matangazo ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Katika barua yake hiyo msikilizaji wetu huyo anasema, yeye ana mapendekezo kadhaa ili kuboresha matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Kwanza kabisa, anakumbuka siku moja mwaka 2007 alipokuwa akisikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, alisikia habari ya kuwa wenzao nchini Tanzania wana tatizo la kupokea matangazo ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kwani kuna tatizo la kuwa na mitambo. Hii imewafanya Watanzania wengi kukosa matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Yeye anaona ni vyema serikali za Tanzania na China zikaondoa tatizo hili inayowakumba wasikilizaji wa Tanzania kwa kurekebisha mitambo. Hii itawawezesha Watanzania wengi kuyapokea matangazo ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwa njia nzuri.

Njia ya pili anaona ni kuwa, wale wanaopokea maoni, maswali na mapendekezo kutoka kwa wasikilizaji wa matangazo yetu, kuhakikisha kuwa hawawaachi wasikilizaji wenyewe vivyo hivyo. Ingekuwa vizuri ikiwa wasikilizaji wangepewa zawadi ili kuwatia moyo. Wakati wa kuchagua wale wa kupewa zawadi, ni vizuri vilevile wawe na usawa yaani wasikilizaji wanaowasiliana kwa tovuti au barua wote wachukuliwe kwa usawa.

Anasema pia ingekuwa ni vizuri kama idadi ya washindi wanaopewa fursa kuitembelea China ingeongezwa. Anatoa mfano kuwa, mwaka 2002 alipoanza kusikiliza matangazo ya Kiswahili ya Radio China kimataifa na wenzake kumi na mmoja, hawakuacha hata siku moja kusikiliza matangazo yetu hayo. Ilikuwa tu hadi mwaka uliopita wakati walipopokea habari kwa redio ya kuwa msikilizaji mmoja tu ndiye amepata ushindi na kuchaguliwa kuja kutembelea China. Habari hiyo iliwakatisha tamaa kiasi, na wasikilizaji kadhaa wakapunguza moyo wa kusikiliza matangazo yetu. Yeye na wenzake wanne ambao hawakuwaunga mkono, wamekuwa wakiwahimiza hao wenzao waendelee kusikiliza matangazo yetu bila mafanikio makubwa. Mmoja wao pia alisema, Mtu mmoja au hata watano kuchaguliwa kati ya watu milioni sabini hapa Afrika mashariki, ni idadi ndogo mno na nafasi ya kuchaguliwa ni ndogo, na yeye hana uwezo wa kutumia tovuti kama washindi ambao wamekuwa wakiwasikia.

Pia anataka kutuambia kuwa, wiki iliyopita alipokea barua kutoka Radio China kimataifa na mara moja akaenda kuwaonesha hao wenzake, na wote wakashtuka ya kuwa hata hao wanaotuma barua, pia hujibiwa, na sasa wote wamerejea kusikiliza makala kutoka China na kwa sababu wengi wao hawana uwezo wa kutuma maoni yao kupitia internet, wamemwachia jukumu lote, na ili kuwatia moyo amekubaliana nao ya kuwa, kama atapata zawadi yoyote, basi atagawana nao kwa usawa.

Mwisho anasema ni vizuri kama wanaotangaza makala kutoka China kama Fadhili Mpunji, Chen na wengineo wawe wanakwenda kuwatembelea wasikilizaji kila mwaka ili kuonana na wasikilizaji. Anasema sio vizuri kutembelea miji mikubwa peke yake, ni vizuri pia wakitembelea hata vijiji kama Maragoli. Kwa kuwa watu wa maeneo kama hayo mara kwa mara wanakuwa na pilikapilika za kujitafutia riziki, wakati mwingine wanakosa kusikia matangazo ya barua zao zikisomwa, anaona ni vizuri kama kila siku, mwanzoni na mwisho wa kipindi, majina ya wasikilizaji ambao barua zao zilisomwa yawe yanarudiwa.

Tunakushukuru sana msikilizaji wetu kutoka Maragoli Kenya, ingawa hukutaja jina lako lakini maoni yako na maswali yako tumeyapokea vizuri. Msikilizaji wetu tunapenda ufahamu kuwa idhaa yetu ina wasikilizaji wengi sana kutoka kila pembe ya dunia, na wasikilizaji hao wote ni watiifu kama wewe. Tunapotoa shindano la chemsha bongo kwa wasikilizaji wetu, lengo letu kubwa ni kuwafanya wawe na ufahamu mkubwa kuhusu mambo ya China, na zawadi tunazowapa ikiwa ni pamoja na nafasi ya ushindi maalum, ni sehemu tu ya kuonesha kuwa tunathamini usikilizaji wa wasikilizaji wetu. Lakini ukumbuke kuwa wasikilizaji ni wengi sana, na tungependa kutoa zawadi kwa kila mmoja, kutokana na hali hiyo tumeamua kutumia chemsha bongo ili kugawa zawadi chache kwa wasikilizaji wetu kwa njia ya haki na usawa, lengo letu kuu ni kuwafanya wasikilizaji wetu wapate ufahamu, zawadi tunazotoa ni kama motisha tu. Ukumbuke kuwa mbali na idhaa ya Kiswahili, idhaa za lugha nyingine pia zinashiriki kwenye chemsha bongo, kwa hiyo kuna ushindani mkubwa sana katika kutoa zawadi, sisi mara kwa mara tunawapigania wasikilizaji wetu, na sio rahisi kutoa zawadi kwa mamilioni ya wasikilizaji wetu. Pia tunapenda mfahamu kuwa wasikilizaji wetu wote wanaowasiliana nasi kwa njia yoyote, iwe kupitia internet au barua wote wana uzito na umuhimu sawa. Kama ulivyosema mwenyewe, baada ya kutuandikia barua mara moja ulipata majibu kutoka kwetu, kwa hiyo wasikilizaji wetu msio na nafasi ya kutembelea tovuti yetu au kutuandikia e mail, msiwe na wasiwasi mawasiliano yetu yanaendelea kama kawaida, ukituandikia barua tutakujibu haraka, kama tulivyofanya siku zote!

Na kuhusu kuwatembelea wasikilizaji wetu walioko sehemu mbalimbali, nafasi inapopatikana tunajitahidi kufanya hivyo kama tulivyofanya kwenye miaka iliyopita tulipokutana na wasikilizaji wetu wa Kenya na Tanzania.